Hongera Yanga, lakini bado kuna kazi kubwa mbele

21May 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Hongera Yanga, lakini bado kuna kazi kubwa mbele

KIKOSI cha Yanga kimerejea nchini jana mchana kikitokea Angola huku wawakilishi hao wa taifa kwenye michuano ya kimataifa kwa ngazi ya vilabu wakirejea kishujaa baada ya kufanikiwa kutinga hatua ya makundi ya michuano ya kombe la Shirikisho.

Yanga imetinga hatua hiyo baada ya kuitupa nje ya michuano hiyo timu ya Sagrada Esperanca ya nchini humo kwa jumla ya magoli 2-1.

Nipashe tunaungana na mashabiki wa Yanga na watanzania kwa ujumla kuwapongeza wachezaji na viongozi kwa hatua ambayo klabu hii imefikia.

Tunaamini ushindi na mafanikio yao pia ni sifa ya nchi yetu katika anga la kimataifa kwenye mchezo huu wa soka.

Pamoja na sifa hiyo bado klabu ya Yanga inasafari ndefu kuelekea kwenye kilele cha mafanikio kwa mashindano haya kwa kuwa hatua ya makundi waliyofikia pengine ni hatua ngumu zaidi kutokana na ukweli kuwa timu zote zilizoingia kwenye hatua hii ni timu bora na imara.

Kwa kuzingatia hilo, Nipashe tunatoa wito kwa wachezaji, viongozi na benchi zima la ufundi la timu hiyo kufanya maandalizi na kuelekeza akili na nguvu zao kwenye hatua hiyo ambayo droo ya makundi ya michuano hiyo itapangwa wiki ijayo.

Tunaamini kwa hatua ambayo Yanga imefikia bado inauwezo wa kufika mbali zaidi ya hapo na ndilo ambalo mashabiki na watanzania wanasubiri kuona.

Kwa wachezaji kikubwa ni kuzingatia kile ambacho kocha anakifundisha pamoja kuhakikisha wanakuwa na nidhamu ya mazoezi.

Hakuna kinachoshindikana kama kunakuwa na dhamira ya kweli ya kutaka kufika mbali, na kwa hilo wachezaji na uongozi mzima wa Yanga wameonyesha tangu timu hiyo ilipokuwa inashiriki michuano ya klabu bingwa Afrika kabla ya kutolewa na Al Ahly na kutupwa kwenye michuano hii ambayo sasa wamefikia hatua ya makundi.

Ugumu wa michuano hii ni kutokana na ukweli kuwa miongoni mwa timu nane zilizofuzu hatua ya makundi, timu tano zote zinatoka nchi za kiarabu ambazo zimekuwa kizingiti kikubwa kwa timu za Tanzania pindi zinapokutana kwenye michuano mbalimbali.

Na hata timu nyingine mbili ukiiondoa Yanga, zinatoka kwenye mataifa ambayo yamepiga hatua kubwa kwenye mchezo huu wa soka ukilinganisha na Tanzania (Ghana na DR Kongo).

Lakini bado soka unabaki kuwa mchezo wa wazi ambapo maandalizi, kujituma na kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja kunaweza kukatoa matokeo mazuri kwa Yanga.

Nipashe tunawatakia maandalizi mema Yanga, na tunaamini wanaweza wakafika mbali kwenye michuano hii na kuitangaza vyema nchi yetu nje ya mipaka yetu.

Na kwa kuzingatia ndio klabu pekee iliyobakia kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa msimu huu baada ya Azam kutolewa, ni vyema Yanga wakapata sapoti kutoka kwa viongozi wa Serikali kwa kuwasaidia pale watakapoitaji msaada kutokana na umuhimu na uzito wa jukumu lao.

Bila kujali timu yenyewe imejiandaa vipi, sapoti ya nchi ni muhimu ili kuipeperusha vyema bendera ya nchi yetu kwenye michuano hii ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya vilabu Afrika.

Nipashe tunasema, hongera Yanga na tunawatakia kila la heri kwenye hatua ya makundi ya michuano hii.

Habari Kubwa