Idadi wachezaji wa kigeni nchini isitumiwe vibaya

16May 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Idadi wachezaji wa kigeni nchini isitumiwe vibaya

BARAZA la Michezo la Taifa (BMT), limeanza kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka kuhusu idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa na timu za hapa nchini ndani ya msimu mmoja.

Kwa sasa kanuni zilizopitishwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na klabu za Ligi Kuu Bara, zinataka timu moja kusajili wachezaji wa kigeni wasiozidi 10.

Lakini kanuni hiyo hiyo, ilielekeza klabu hizo kusajili wachezaji wageni ambao wanazitumikia nchi zao (Timu za Taifa), kwa malengo ya kuwapa changamoto ya kuwania namba kwenye kikosi cha kwanza.

Kipengele hiki kilizingatia kuifanya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ndio ina wachezaji wengi kutoka nje ya nchi kutokuwa 'jalala' la wachezaji walioachwa na timu nyingine na vile vile kuiongezea thamani.

Wachezaji wa kigeni wenye viwango vya juu, mbali na kulipatia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kipato kupitia ada ya Dola za Marekani 2,000 (zaidi ya Sh. milioni nne), wanatakiwa wawe ni wenye uwezo wa kuzisaidia timu husika kufanya vizuri katika mashindano yote, timu yake iliyomsajili wanayoshiriki.

Lakini wachezaji wageni ambao watasajiliwa bila kufuata vigezo, huenda wakazigharimu klabu husika badala ya kuwapa kile walichokitarajia wakati wanawasajili.

Mbali na ushindani wa kuwania namba, pia usajili wao unalenga kuwapa 'kiu' wachezaji wazawa nao kujituma na kuongeza bidii ili kuwindwa na timu za mataifa mengine au kwa walioko katika madaraja ya chini kutakiwa na timu za ngazi ya juu.

Idadi hiyo iliongezeka kutoka wachezaji watano iliyokuwa awali, baada ya viongozi wa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi Daraja la Kwanza kuridhia uamuzi huo.

Hata hivyo, bado katika kipengele hicho, klabu zimekuwa hazitekelezi vema usajili huo, kwa kuingia mikataba na wachezaji ambao hawachezi katika Timu za Mataifa wanayotoka kama ilivyopitishwa.

Tumeshuhudia klabu zikiwasajili wachezaji ambao hawajawahi kuchezea timu zozote za mataifa wanayotoka au wengine wakiwa wamekaa bila ya timu kwa muda mrefu, na matokeo yake kutumia Ligi Kuu Tanzania Bara kama sehemu ya kufanya mazoezi na kuinua upya viwango vyao.

Nipashe inazikumbusha klabu zenye uwezo na nia ya kusajili wachezaji wageni, kuhakikisha zinafanya mchakato huo kwa umakini wa kiwango cha juu.

Wachezaji wa kigeni ambao watakuwa na viwango bora kama ilivyo kwa Mzambia Clatous Chama anayeichezea Simba, Haruna Niyonzima kutoka Rwanda wa Yanga au Nicholas Wadada anayeitumikia Azam na Timu ya Taifa ya Uganda (Cranes), ndio aina ya nyota wanaotakiwa.

Haipendezi kuona klabu inasajili mchezaji wa kigeni, halafu yenyewe ikiwa haijiamini na ilichokifanya huku ikipa moyo kwa kumpa muda wa kuzoea ligi.

Kama ambavyo wachezaji wetu wa Tanzania wanafanya kwanza majaribio kabla ya kusajiliwa huko ughaibuni wanakokwenda kusaka timu, pia klabu za hapa nchini zisione vibaya kuwafanyia kwanza majaribio nyota wanaokuja na kuacha tabia ya kuwapa mikataba kabla ya kuwaona viwango vyao.

Utaratibu wa kuwafanyia majaribio uko duniani kote, kama mchezaji ana uwezo ataonekana kwenye majaribio, lakini kama 'sanaa' zitaendelea kuhusishwa kwenye usajili, safari ya mafanikio kwenye Ligi Kuu Bara itaendelea kukumbwa na changamoto ya kupokea wachezaji 'mizigo'.

Nipashe inawakumbusha viongozi wa klabu kutorudia makosa kwa kutoa mapendekezo yatakayoendana na mazingira na mahitaji halisi ya timu zao na vile vile kuweka mbele maslahi ya soka la Tanzania.

Habari Kubwa