Intelijensia ya Polisi ipunguze uhalifu wa kutisha Mwanza

25May 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Intelijensia ya Polisi ipunguze uhalifu wa kutisha Mwanza

MATUKIO ya vitendo mbalimbali vya uhalifu yakiwamo mauaji yameendelea kushamiri katika Mkoa wa Mwanza kwa miaka kadhaa sasa.

Matukio hayo ya mauaji, watu kumwagiwa tindikali na ya imani za kishirikina yakekuwa yakitokea kila uchao katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mwanza.

Katika toleo letu la jana, tuliripoti tukio la kuuawa kwa kupigwa risasi Mwenyekiti wa Mtaa wa Bulale, Kata ya Buhongwa, Nyamagana jijini Mwanza, , Alphonce Mussa (48), kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana, wakati akiwasuluhisha wanandoa.

Mauaji hayo yametokea zikiwa wiki mbili tangu kutokea kwa mauaji ya watu saba wilayani Sengerema, hivyo kuwa tukio la tatu katika kipindi cha wiki mbili na kusababisha vifo vya watu 11 katika wilaya za Sengerema na Nyagamana.

Tukio lingine la uhalifu wa kutisha lilitokea Jumatano iliyopita wakati wa usiku ambalo watu wasiojulikana waliwaua watu watatu na mmoja kujeruhiwa akiwamo imamu walipokuwa wakisali katika msikiti uliopo eneo la Mkolani, jijini Mwanza.

Watu hao waliuawa kwa kuchinjwa kwa mapanga, baada ya wahalifu kuuvamia msikiti huo na kuwaamuru waumini kulala chini kisha kuwaua watu hao.

Oktoba 14, 2012 aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Liberatus Barlow, aliuawa kwa kupigwa risasi kati ya saa saba na saa nane usiku katika maeneo ya Kitangiri.

Mwaka 1995, aliyewahi kuwaMbunge wa Mwanza Mjini, Said Shomari alimwagiwa tindikali na na watu wasiojulikana. Mei 14, 2010, Katibu wa CCM Kata ya Isamilo, wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza, Bahati Stephano (49), aliuawa kwa kuchomwa kisu kifuani na tumboni, baada ya kuvamiwa ofisini kwake na kijana mmoja majira ya mchana.

Tukio hilo lilimhusisha aliyekuwa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Leonard Bihondo na watu wengine wawili, lakini Oktoba 12, 2013, waliachiwa huru na mahakama.

Itakumbukwa pia kwamba Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa ambayo imekuwa na matukio mengi ya mauaji yanayotokana na imani za ushirikina. Watu kadhaa wenye ulemavu wa ngozi wamekuwa wakiuawa kwa kasi mkoani humo pamoja na mauaji ya vikongwe.

Kimsingi, kuna matukio mengi ya uhalifu ambayo hatuwezi kuyataja yote, lakini inatosha kusema kuwa matukio ya uhalifu wa kutisha yanayotokea mkoani humo ni tishio kwa usalama wa raia na mali zao.

Hali hiyo inaweza kusababisha wananchi kuishi maisha yasiyo ya amani na utulivu kutokana na hofu kwamba wanaweza kukumbwa na vitendo hivyo wakati wowote. Tunashindwa kuelewa sababu za kuendelea kwa kasi kwa matukio hayo badala ya kudhibitiwa. Tunavikumbusha vyombo vya dola kwamba ingawa suala la ulinzi na usalama ni la kila raia, lakini ndivyo vilivyopewa dhamana hiyo.

Itakuwa vizuri kama vyombo vyetu vya ulinzi na usalaha hususan Jeshi la Polisi vitachukua tahadhari wakati wote kuhakikisha kwamba matukio kama haya yanaendelei kutokea katika Mkoa wa Mwanza na ikiwezekana watu wanaopanga kutekeleza uhalifu huo wanakamatwa mapema na kupelekwa kwenye mkono wa sheria.

Mara kadhaa Jeshi la Polisi limekuwa likielekeza nguvu zaidi kudhibiti shughuli za vyama vya siasa ikiwamo mikutano na maandamano kwa maelezo kuwa intelijensia yao imebaini kuwa shughuli hizo zingeweza kuhatarisha amani.

Tunashauri kwamba taarifa za intelijensia ya Polisi ni vizuri sasa zikatumika ili kusaidia kudhibiti kasi ya matukio ya kutisha ya uhalifu mkoani Mwanza, ili wakazi wake waishi katika mazingira ya amani na utulivu.

Habari Kubwa