Iwapo tulimaliza plastiki, ukatili hautatushinda

01Nov 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Iwapo tulimaliza plastiki, ukatili hautatushinda

TAARIFA za ukatili kwa binadamu zilizoripotiwa jana na gazeti letu zinaonyesha jinsi ambavyo vitendo vya udhalimu huko Shinyanga vilivyosababisha mwana familia kufungwa minyororo mikononi na miguuni kwa zaidi ya miezi miwili.

Aidha, Nipashe inavitaja vitendo vingine vya ukatili kwa watoto vinavyohusisha ubakaji na ulawiti, ambavyo vimewaumiza mamia ya watoto mkoani Kilimanjaro.

Tukiangalia zaidi ukatili dhidi ya watoto, inaelezwa kuwa tangu kuanza mwaka huu takribani watoto 127 wamefikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi kutibiwa kutokana na ukatili dhidi yao, unaohusisha ubakaji na ulawiti.

Wataalamu kutoka Mawenzi wanasema kesi (visa) za ubakaji zilizofikishwa hospitalini hapo ni 90 wakati za ulawiti ni 37. Hayo ni matukio kutoka mkoa wa Kilimanjaro na kwenye hospitali moja pengine idadi ni kubwa zaidi kutoka hospitali mbalimbali na kwenye vituo vya polisi vingine nchini kote.

Tunaona kuwa hili si jambo la kupuuzwa hata kidogo. Ni kama kuliangamiza taifa na kusababisha mlolongo wa matatizo kwa watoto wetu.

Ikumbukwe kuwa unyanyasaji na mateso dhidi ya watoto wetu ni chanzo kikuu cha umaskini kwenye jamii zetu pia ni kikwazo cha kufikia maendeleo endelevu ambayo taifa linayatazamia na kuwa na mikakati ya kuyafikia inayoandaliwa kila wakati.

Ukatili huu unawatia watoto wetu ulemavu. Aidha, unawatumbukiza kwenye kitanzi cha umaskini kwa kuwa mabinti hawa wanaobakwa na kulawitiwa ni wazi kuwa watashindwa kusoma na matokeo yake wanazidi kuwa mbumbumbu na maskini.

Tukumbuke kuwa kuwanyanyasa watoto kingono kunawaingiza kwenye kukosa haki za msingi kama kukua na kuwa na viungo na akili timamu. Kunawanyima pia haki ya kuwa na afya njema na kuwasababishia msongo wa mawazo unaotokana na uharibifu wa maumbile yao na zaidi huwaongezea umaskini katika maisha yao.

Tunaona kuwa watoto kutoka kaya maskini na zile zenye walezi au wazazi maskini au wenye ulemavu ndiyo wanaokuwa na hali mbaya zaidi.

Kutokana na ugumu wa maisha wanashindwa pengine hata kutoa taarifa polisi au kufika hospitalini. Hawa ndiyo ambao kutokana na kukosa ulinzi na umaskini nyumbani kwao wanazidi kunyanyaswa na kudhulumiwa kingono. Kutokana na uovu huo wanazidi kuwa maskini na kwa vyoyote vile wanaendelea kuishi katika umaskini mkubwa.

Kwa upande wa wasichana ukatili huu unasababisha washindwe kusoma shuleni na pengine hupata maradhi yakiwamo ya kujamiiana mfano kaswende, pangusa, maambukizi ya mkojo na hata VVU na Ukimwi.

Yote haya kwa vile hawawezi kupata matibabu husababisha waendelee kuugua na kushindwa kwenda shuleni. Kwa wengine unyanyasaji huo ni chanzo cha kufeli mitihani yao, kukimbia shule, utoro na kurudi tena kwenye uteja wa adui ujinga.

Kwa watoto wote bila kujali kuwa ni wakike au wa kiume athari hizo ni wazi kuwa kubakwa au kulawitiwa kutasababisha washindwe kusoma, wataishi kwenye umaskini kwa vile hawatakuwa na fursa za kupata kazi bora wala mafunzo ya kuendeleza maisha yao.

Ndiyo maana tunaona kuwa ni lazima kuwa na mikakati ya kuwalinda watoto wetu. Tunahitaji kuwa na utaratibu ndani ya vijiji, mitaa, vitongoji na kila mahali kuwasaidia watoto wasinyanyaswe kingono.

Tunahofu kuwa tusipofanya hivyo tutaendelea kubakia na umaskini na ujinga na maradhi maadui ambao tangu uhuru walilitesa na wanaendelea kuliumiza taifa letu.

Kama taifa tunahitaji kuandaa mikakati ya ulinzi endelevu wa watoto kwani Tanzania isiposimamia na kumaliza janga hili, haitakuwa tofauti na msemo kuwa ukicheza na nyani utavuna mabua. Ni sawa na kusema tusipolinda watoto taifa hili litaangamia. Hebu tuchukue hatua.

Habari Kubwa