Iwe bajeti jumuishi, kuondoa umaskini

12Jun 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Iwe bajeti jumuishi, kuondoa umaskini

KESHO Watanzania wanangoja kwa hamu kusikia bajeti yao ambayo ni andiko la serikali linaloonyesha na kuainisha maamuzi ya vipaumbele vya maendeleo ya nchi kwa mwaka 2019/2020.

Ni jambo jema kuwa bajeti itazungumzia maendeleo ya nchi kwenye uchumi, jamii, miundombinu na kwa ujumla kufikia malengo na matarajio ya kuwa na Tanzania ya viwanda na ya uchumi wa kati ifikapo 2025.

Tunapenda kusisitiza kuwa ni vyema kueleza kuwa ni muhimu bajeti isizungumzie maendeleo kiujumla kwenye uchumi na kwenye sekta za kipaumbele bali iwe jumuishi ikimfikia kila mmoja.

Bajeti ya jumla faida zake hubakia kwa maeneo kadhaa bila kugusa makundi maalumu ya wanyonge wakiwamo wanaoishi pembezoni, ambao si rahisi wakanufaika moja kwa moja na vipaumbele vinavyogusiwa.

Ndiyo maana tunahimiza kuwapo bajeti jumuishi na shirikishi inayowagusa masikini hasa wanawake vijijini, yatima, wajane, wazee na kaya maskini zisizo na msaada ambazo mara nyingi haziwezi kunufaika moja kwa moja na matokeo ya bajeti ya taifa.

Bajeti jumuishi hiyo tunayotarajia ni ile inayowapa kipaumbele mabinti wa kaya maskini ambao wazazi na walezi wao, hawana kipato cha kuwawezesha kununua huduma muhimu kama taulo za wanawake za kujisitiri kila mwezi.

Kukosekana fedha za kununua huduma muhimu kunawalazimisha wasichana kukosa masomo kila mwezi angalau kwa siku tano kwa vile hawawezi kwenda shule kwani hawana kitu cha kujisitiri wakati wa hedhi.

Bajeti hii tunatarajia haitawasahau watu maskini kama hao kwa kuondoa kodi ya pedi na kutoa ruzuku ya kununulia taulo hizo shuleni, ili kuwawezesha mabinti hao kusoma.

Pamoja na vipaumbele vya jumla tunategemea kuona bajeti ikiwakumbatia pia wenye mahitaji maalumu kama wanawake na mabinti kwa kuwekeza zaidi kwenye elimu kwa wote.

Hii itawawezesha wanyonge kusoma na kubadili maisha yao kupitia elimu.

Kadhalika ni tegemeo letu kuwa bajeti ya serikali itaelekeze nguvu kwenye elimu, itakuwa na kipaumbele kwenye kuhakikisha upatikanaji wa madarasa ya kutosha, mabweni, maji na vyoo shuleni iwe msingi au sekondari kwa ajili ya mahitaji mbalimbali.

Hayo ni pamoja na mahitaji ya wasichana na wanaoishi na ulemavu wa aina mbalimbali.

Aidha, tunatarajia bajeti itakayofikisha huduma muhimu, wataalamu na vifaa tiba hospitalini ili kupunguza vifo vya wanawake na watoto.

Ikumbukwe kuwa idadi ya wanawake wanaokufa katika matatizo yanayohusiana na uzazi sasa ni takribani 556 suala ambalo linaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi hatarishi kwa wanawake wajawazito na wazazi.

Masuala ya kufikisha huduma muhimu kwa wananchi kama maji nayo ni muhimu yakaonekana kwenye bajeti, ili kulinda afya za mamilioni ambao huathirika kutokana na magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa maji safi na salama mijini na vijijini.

Bajeti hii jumuishi tunatarajia iwakumbuke watu wanaoishi na magonjwa sugu kama VVU na Ukimwi hasa wa familia maskini ambazo zinahitaji mkono wa serikali kuzisaidia kumudu maisha yao.

Mambo ni mengi, lakini bajeti inayoyakumbuka makundi ya wanyonge na kuinua maisha yake ni muhimu kwa kuwa ni vigumu kupunguza pengo la maskini na matajiri kama serikali haitakuwa na bajeti inayobadilisha maisha ya kila mwananchi.