Jeshi la Polisi liongeze nguvu kupambana na uhalifu nchini

13Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Jeshi la Polisi liongeze nguvu kupambana na uhalifu nchini

HIVI karibuni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, alisema Jeshi la Polisi limefanikiwa kunyamazisha majambazi kimya kimya kwenye maeneo mengi.

Aidha, alithibitisha kuibuka kwa wimbi la ujambazi katika miji ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza, na kwamba operesheni ya kwanza kupambana na majambazi hao imefanikiwa kwa ufanisi mkubwa na sasa awamu ya pili imeanza huku akituma salamu kwa wanaodhani kufanya ujambazi ni njia sahihi ya kujipatia kipato waache mara moja.

Kauli ya Waziri imekuja wakati kwenye maeneo mengi ujambazi na wizi umekuwa kero kubwa na sasa waporaji wa kutumia pikipiki wamerejea, jambo linalohitaji nguvu ya ziada kwa jeshi hilo.

Uporaji unaofanyika kwa kutumia pikipiki ni kupora pochi, simu za watu kwenye vituo vya daladala, barabarani au kwenye vyombo vya usafiri.

Pia, wizi wa vioo na vifaa vingine huku magari yakitembea umerudi hasa yakiwa kwenye foleni, jambo linaloashiria kuwa bado inahitajika nguvu kubwa kukabiliana na wahalifu hawa ambao waziri amesema wanaijaribu serikali.

Mathalani, kwa sasa kwenye mitaa mingi watu wanaibiwa majumbani kwa maana ya kuvunja kuiba TV na vitu vingine vya ndani, pamoja na wizi wa magari ambao ulibaki historia.

Jana limetokea tukio eneo la Temeke baada ya wezi kuingia nyumbani kwa mtu na kujaribu kuiba gari, lakini wahusika waliwashtukia mapema, huku matukio ya watu kuibiwa vifaa vya magari yakiongezeka kwa kasi.

Mathalani, eneo la Kaseni, Kifula, Kisanjuni na Msangeni wilayani Mwanga, umeingia wizi mpya wa kuvunja madirisha kupuliza dawa na kuiba vitu vya ndani kama TV na vinginevyo umeshika kasi, na ndani ya wiki moja kuna matukio sita yameripotiwa kutokea kwenye nyumba tofauti.

Hivi karibuni, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, lilieleza kukamata watuhumiwa zaidi ya 100 wa wizi wa vifaa vya magari na vyombo vya usafiri na kuonyesha vifaa vilivyodaiwa kuibiwa maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Wizi unaripotiwa pia maeneo ya Tegeta, Salasala, Boko, Mikocheni, Tabata na kwingine, na kwa sasa ni kawaida mnapokuwa watu 10 kwenye kundi moja watatu au wanne utawasikia wakieleza kuwapo kwa matukio ya wizi kwenye nyumba zao.

Ndani ya miaka sita matukio ya uhalifu yalipungua nchini na kwisha kabisa hasa uporaji, lakini kwa sasa umerudi kwa kasi kubwa.

Ni muhimu sana mbinu zilizotumika kudhibiti hali hiyo kwa miaka sita ikatumika kuhakikisha matukio haya yanakuwa historia.

Kuna miaka vikundi vya ujambazi vilikuwa vingi ikiwamo kuwa na wafadhili na kulifanyika operesheni ya kukamata wafadhili wake na vinara hasa kwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam, Mbeya na Mwanza, na kufanikiwa kudhibiti wizi wa magari.

Aidha, ni muhimu kurudi kwenye polisi jamii katika kudhibiti uhalifu kwenye mitaa, ikiwamo askari wa pikipiki maarufu kama Tigo, kufanya kazi hiyo, ikiwamo kumaliza mtandao wa uhalifu ambao wakati mwingine baadhi ya askari hulaumiwa kwa madai ya kuhusika kutoa taarifa za watoa siri.

Wajibu wa kulinda raia na mali zao ni wa Jeshi la Polisi, ni muhimu kutimiza kwa ufanisi mkubwa kuhakikisha kuwa jamii inakuwa salama muda wote.

Habari Kubwa