Kamanda Mambosasa apewe ushirikiano kudhibiti uhalifu Dar

31Aug 2017
Mhariri
Nipashe
Kamanda Mambosasa apewe ushirikiano kudhibiti uhalifu Dar

WIKI iliyopita Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, alifanya mabadiliko madogo ya makamanda wa polisi wa mikoa.
Miongoni mwa mikoa iliyoguswa na mabadiliko hayo ni Kanda Maalum ya Dar es Salaam na Dodoma.

Aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, alihamishiwa katika Mkoa wa Mtwara kuendelea na wadhifa huo wakati aliyekuwa Kamanda wa Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, alihamishiwa Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Mabadiliko hayo ni ya kawaida, lakini lengo ni kuboresha utendaji wa jeshi hilo, katika kutimiza jukumu lake la kulinda usalama wa raia na mali zao.

Hata hivyo, Kanda Maalum ya Dar es Salaam bila shaka IGP Sirro atakuwa amezingatia changamoto za kiusalama zinazolikabili Jiji la Dar es Salaam ambao ni kubwa kwa eneo, idadi kubwa ya watu na shughuli nyingi.

Kwa kuzingatia kuwa Kanda Maalum ya Dar es Salaam inaundwa na mikoa mitatu ya kipolisi ya Temeke, Ilala na Kinondoni, ni dhahiri ni eneo kubwa na lenye changamoto nyingi za uhalifu, hivyo inahitaji kuongozwa na kamanda mwenye weledi, mchapakazi, mwadilifu na mzoefu.

Ndiyo maana baada ya kanda hiyo kuanzishwa imekuwa ikiongozwa na makamanda wenye wadhifa wa Kamishna kuanzia kwa Alfred Tibaigana, Suleiman Kova kisha Sirro.

Tunampongeza Mambosasa kwa uteuzi huo ambao una changamoto nyingi, ingawa tunaamini kuwa ana sifa zote na uwezo mkubwa wa kukabiliana nazo, na ndiyo maana IGP Sirro amemuamini na kumkabidhi jukumu hilo.

Juzi alipokutana na vyombo vya habari kujitambulisha wakati akianza kutekeleza majukumu yake rasmi, aliitaja ajenda yake kuu kuwa ni kudhibiti uhalifu na wahalifu katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Ombi alilolitoa ni kwa wananchi na vyombo vya habari kumpa ushirikiano wa kutoa taarifa zihusuzo uhalifu na wahalifu, ili kufanikisha lengo hilo la kudhibiti uhalifu na wahalifu.

Kwa kufahamu kuwa kupambana na kufanikiwa kuudhibiti uhalifu katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam ndicho kigezo kitakachompa fursa ya zaidi katika utumishi wake, ndiyo sababu iliyomfanya Mambosasa kuomba ushirikiano wa kupewa taarifa za uhalifu na wahalifu ili aweze kupaa na kanda hiyo.

Kama alivyosema kamanda huyo, kuwa ushirikiano wa wakazi wa Dar es Salaam ndio utakaowezesha kudhibiti matukio ya uhalifu na hakuna mhalifu atakayesalia, tunawahimiza wakazi wote wa jiji kuhakikisha wanampa Kamanda Mambosasa ushirikiano wa taarifa.

Siyo siri kwamba Jiji la Dar es Salaam lina rekodi ya uhalifu wa matukio mbalimbali kama ujambazi yakiwamo mauaji, uporaji wa kutumia silaha, ukwapuaji unaofanywa na vibaka na utapeli. Haya yote ni matukio yanayohitaji kudhibitiwa kwa nguvu zote.

Kabla Mkondya hajaondoka Dar es Salaam alianzisha operesheni ya kuwakamata na kuwaondoa wapigadebe katika vituo vya daladala jijini kisha kuwafikisha mahakamani, kutokana na kuwa chanzo cha wizi na ukwapuaji wa mali za watu. Hata hivyo, baada ya kuondoka operesheni hiyo imesitishwa.

Tunaamini kuwa Mambosasa atairejesha opereshehi hiyo na kubuni mikakati mbalimbali endelevu ambayo itasaidia kuudhibiti uhalifu, ikiwamo kuendeleza mpango wa ulinzi shirikishi wa polisi na jamii pamoja na kujenga vituo vidogo vya polisi kutokana na vilivyopo kutokidhi mahitaji ya idadi ya watu ambayo inaongezeka kwa kasi kila uchao.

Ni matarajio yetu kuwa Mambosasa atalifanya jiji kuwa sehemu salama na tulivu ya kuishi kutokana na uwezo wake wa kudhibiti wahalifu katika maeneo mbalimbali alikofanya kazi, kama alivyosema juzi.

Habari Kubwa