Kamati za maadili maofisa mahakama zinahitaji bajeti

14Feb 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kamati za maadili maofisa mahakama zinahitaji bajeti

SERIKALI imeombwa kutenga fedha kwa ajili ya kamati za Maadili za Maofisa wa Mahakama za Mikoa na Wilaya ili ziweze kutekeleza majukumu yake kama sheria inavyozitaka.

Ombi hilo lilitolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Augustine Mahiga, kwa ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kwa ajili ya kuwawezesha maofisa hao kutekeleza wajibu wao kama inavyotakiwa.

Kamati za Maadili za Maofisa wa Mahakama zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya kutotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, kutokana na upungufu wa bajeti.

Kamati hizi ziliundwa baada ya kutungwa kwa sheria ya Usimamizi wa Mahakama namba 4 ya mwaka 2011, na sheria hiyo pia inazitaka mahakama hizo kukutana na kuwasilisha taarifa zake kwa Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Waziri Mahiga alitoa ombi hilo alipokuwa akizindua mwongozo wa uendeshaji wa kamati za maadili za maofisa wa Mahakama juzi jijini Dodoma, na kusema wizara yake itahakikisha Tume ya Utumishi wa Mahakama inapatiwa rasilimali fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli zake ikiwamo Kamati za Maadili za Maofisa wa Mahakama kwa ufanisi unaotakiwa.

Chombo hiki kina umuhimu mkubwa kwa muhimili huo katika utekelezaji wa majukumu yake ya kutoa haki. Ikumbukwe kuwa suala la maadili lina umuhimu wa pekee kwa watumishi wa Mahakama.

Kazi ya kutoa haki inahitaji watu wenye maadili, uaminifu, weledi na uadilifu wa hali ya juu, hivyo wajumbe wa kamati na maofisa wa mahakama hawanabudi kutekeleza majukumu yao katika mazingira bora, wezeshi na rafiki.

Ili waweze kutekeleza wajibu wao inavyotakiwa, hawanabudi kuwezeshwa kwa bajeti, ambayo inahusisha fedha na vifaa.

Kama inafikia hatua Waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria kulitolea jambo hilo kilio kuwezeshwa kwa bajeti, ina maana kuwa shughuli za chombo hicho hazitekelezwi inavyopaswa kama sheria na kanuni zilizokianzisha zinavyoelekeza.

Kutokana na umuhimu wa kuimarisha dhana ya utawala bora kupitia sheria ya uendeshaji wa Mahakama, ndio maana Serikali iliamua kuruhusu uwapo wa kamati za maadili za maofisa wa Mahakama ambazo ni ya Maadili ya Majaji, Kamati ya Maadili ya Maofisa wa Mahakama na Kamati ya Maadili ya Mahakama ya Mkoa na Wilaya.

Kutokana na umuhimu huo, ndio maana Waziri Mahiga anasema kuwa kamati hizi zina nafasi kubwa katika kusimamia, kuendeleza na kudumisha maadili ya utumishi wa mahakama.

Tunaona kuwa umuhimu wa kamati hizi haunabudi kuishawishi serikali kupitia Tamisemi kutenga bajeti kwa ajili hiyo ili majukumu yao yatekelezwa kama sheria inavyotaka.

Kwa kufanya hivyo, bila shaka majukumu hayo yatatekelezwa kama inavyotakiwa, na ni imani yetu kuwa hatua hiyo itasaidia kuwakumbusha watumishi wote kuzingatia maadili.

Aidha, hatua hiyo itawafanya watumishi wachache wanaoendelea na vitendo vya ukiukaji wa maadili kuacha mara moja ili kulinda heshima ya mhimili wa Mahakama kwa jamii sambamba na usalama wa ajira zao.

Tunakubaliana kabisa na kauli ya wakuu wa mikoa nchini ambao ni walezi wa kamati hizo kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi, kuwa palipo na maadili pana amani, haki, uaminifu katika utendaji kazi, umoja na ushirikiano, na kwamba kuwapo kwa maadili pia ni ni kichocheo cha maendeleo ya Taifa.

Habari Kubwa