Kanuni Ligi Kuu msimu ujao ziboreshwe kisasa

13Jul 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kanuni Ligi Kuu msimu ujao ziboreshwe kisasa

KUMALIZIKA kwa msimu huu wa mwaka 2019/20, ni ishara sahihi kuwa maandalizi ya msimu mpya wa 2020/21 yanatakiwa kuanza mapema.

Tayari kila timu inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, imeshacheza mechi 34 kati ya michezo 38 ambayo inatakiwa kuchezwa kwa kila klabu.

Simba ya jijini, Dar es Salaam tayari imeshatwaa ubingwa wa ligi hiyo wakati vita iliyobaki ni ya timu zinazopambana kujinasua na janga la kushuka daraja.

Ushindani huo umekuwa mkubwa kutokana na mabadiliko ya kanuni yaliyofanywa kabla ya kuanza kwa msimu, kati ya timu 20, nne zitakazoburuza mkia zitashuka moja kwa moja wakati mbili zitacheza mechi za mtoano na klabu nyingine mbili za Ligi Daraja la Kwanza.

Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza, tayari Gwambina FC kutoka Misungwi ya jijini, Mwanza na Dodoma Jiji FC tayari zimeshapanda daraja, zitacheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Moja ya mambo muhimu yanayotakiwa kuwekwa sawa ni kanuni za Ligi Kuu Bara na kanuni hizo huandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa kufuata mapendekezo ya wadau wake, ambao ni klabu.

Timu zote zinatakiwa kutumia muda wa maandalizi ya kanuni vizuri ili msimu mpya utakapoanza, kusiwe na malalamiko yoyote ya kuburuzwa au kuonewa na TFF.

Nipashe inaamini klabu zikitumiwa vizuri nafasi ya kuwasilisha maoni yake, tutashuhudia kutosikia malalamiko ya mara kwa mara wakati safari ya kusaka mfalme mpya wa Tanzania Bara atakavyoanza kusakwa.

Klabu zinatakiwa kutoa mapendekezo kuhusiana na idadi ya nyota wa kigeni watakaoruhusiwa kusajiliwa kwa kuzingatia hali halisi walizonazo na si kukubaliana kwa kuzifaidisha klabu chache.

Tunawakumbusha kanuni ya wachezaji wa kigeni ifanyiwe kazi kwa kuzingatia maslahi ya nchi na vile vile ikiwaangalizi nyota chipukizi ambao wanahitaji nafasi ya kukuzwa pamoja na kuendelezwa.

Kwa sasa kanuni zilizopitishwa na TFF, zinataka timu moja kusajili wachezaji wakigeni wasiozidi 10, je, kipindi hiki ambacho Timu ya Taifa (Taifa Stars), ambayo inategemea zaidi wachezaji wanaoshiriki Ligi Kuu, inastahili kuwa na wageni zaidi au wapungue?

Klabu pia zinatakiwa ziwe mfano kwa kusajili wachezaji wa kigeni wenye viwango vya juu na kuacha kuzifanya klabu zao kuwa sehemu ya majaribio.

Wachezaji wageni watakaosajiliwa wawe ni wenye kuleta ushindani na watakaowapa changamoto ya kuwania namba wazawa ambao ndio wengi zaidi.

Mbali na ushindani wa kuwania namba, pia usajili wao unalenga kuwapa changamoto wachezaji wazawa ili wajitume na waongeze bidii, hatimaye nao kuwindwa na timu za mataifa mengine au kwa walioko katika madaraja ya chini kutakiwa na timu za ngazi ya juu.

Klabu zisione aibu kuwafanyia majaribio wachezaji wao kama ambavyo tunashuhudia klabu za Ulaya zinavyowafanyia nyota inaotaka kuwapa mikataba mpya na kwa kufanya hivyo, Ligi Kuu Bara itapanda thamani na hapo itakuwa ni mwisho wa kusajili 'wababaishaji'.

Pia kuna suala la mgawanyo wa mapato, hii imeonekana kusumbua baadhi ya klabu za mikoani pale wanapokuja Dar es Salaam na kushuhudia timu mwenyeji akivuna kiasi kikubwa tofauti na wanavyokwenda ugenini. Suluhisho ni kuridhia kurudi kwenye mgawanyo wa zamani ambao mwenyeji anapata asilimia 60 na mgeni ataondoka na asilimia 40.

Habari Kubwa