Karibu bajeti 2019/20, uzalendo wahitajika

13Jun 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Karibu bajeti 2019/20, uzalendo wahitajika

MAKADIRIO ya bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha yanatarajiwa kuwasilishwa bungeni jijini Dodoma baadaye leo jioni.

Mpango wa Maendeleo ya Taifa na ukomo wa bajeti ya mwaka 2019/20, unaonyesha bajeti hiyo ya nne kwa serikali ya awamu ya tano, inatarajiwa kuwa Sh. trilioni 33.1. Kwa mujibu wa mpango huo, mapato ya ndani yakijumuisha yatokanayo na halmashauri yanatarajiwa kuwa Sh. trilioni 23.Mpango huo unabainisha kuwa Serikali Kuu inatarajia kukusanya Sh. trilioni 22.2. Kati yake, mapato yatokanayo na kodi Sh. trilioni 19.1 na mapato yasiyo ya kodi Sh. trilioni 3.1.

Nipashe tunaipongeza serikali kwa jitihada zake katika kuongeza makusanyo na kudhibiti mianya ya ufujaji wa fedha za umma kwa lengo la kutekeleza miradi ya maendeleo.

Takwimu za makusanyo zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato (TRA), zinaonyesha serikali ya awamu ya tano imefanikiwa kuongeza makusanyo kwa wastani Sh. bilioni 450 kwa mwezi.Takwimu hizo zinaonyesha kuwa serikali ya awamu ya tano imeongeza makusanyo kutoka wastani wa Sh. bilioni 850 kabla ya Novemba 2015 hadi kufikia Sh. trilioni 1.3 kwa mwezi.Hata hivyo, pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali kuimarisha makusanyo ya nchi kwa kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato, taarifa za kamati mbalimbali za Bunge na ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zinaonyesha utekelezaji usioridhisha wa miradi ya maendeleo kutokana na ukosefu wa fedha.Hii inatokana na ukweli kwamba kiwango kikubwa cha makusanyo kinatumika kulipa Deni la Taifa na mishahara ya watumishi wa umma.Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, serikali inatumia wastani wa Sh. bilioni 600 kulipa Deni la Taifa na Sh. bilioni 550 kwa mishahara ya watumishi wa umma kila mwezi, hivyo katika makusanyo yake ya Sh. trilioni 1.3, hubakiwa na Sh. bilioni 150 pekee.Ni kutokana na hali hii, Nipashe tunaona ipo haja kuongeza juhudi zaidi katika ukusanyaji wa mapato ya nchi ili kutekeleza miradi muhimu kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kijacho.Tunapoelekea kufunga mwaka wa fedha 2018/19 siku 18 zijazo, mamlaka zinazohusika na ukusanyaji wa mapato, zinapaswa kujipanga kuhakikisha zinatatua changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu ili zisijirudie mwakani.Tunaamini hatua kali zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya wanaojihusisha na kadhia ya ukwepaji kodi na uhujumu uchumi kwa ujumla.Baadhi ya nchi za Amerika, kosa la kukwepa kodi halina faini. Yeyote anayepatikana na hatia hiyo hulazimika kutumikia kifungo gerezani.Hata Tanzania, wanaohukumiwa kifungo kwa makosa ya ukwepaji kodi, wamekuwa hawajumuishwi kwenye utaratibu wa msamaha wa Rais. Yote haya yanaonyesha jinsi suala la ulipaji kodi lilivyo muhimu kwa maendeleo ya nchi.  Tanzania ina takribani watu milioni 50 sasa, lakini takwimu za ulipaji wa kodi zinaonyesha walipakodi hawafiki hata robo ya watu wote waliopo nchini. Tunaamini hamasa na elimu ya ulipaji wa kodi itaisaidia nchi kuongeza mapato yake na hatimaye kutekeleza miradi muhimu kwa fedha za ndani badala ya kutegemea misaada na mikopo kutoka nje.Hatupingi utaratibu wa serikali kukopa kwa lengo la kutekeleza miradi ya maendeleo, lakini tunaona ni muhimu wananchi wakahamasishwa zaidi kulipa kodi na kusaidia jitihada hizo za serikali kuimarisha uchumi wa nchi. Tunaamini huo ndiyo uzalendo unaohitajika kutimiza ndoto za kuijenga Tanzania yenye uchumi wa kati kufikia mwaka 2025.

Habari Kubwa