Karibu Mwaka 2020

01Jan 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Karibu Mwaka 2020

LEO tumeuanza Mwaka Mpya wa 2020. Tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupatia uzima, hivyo kuvuka mwaka 2019.
Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa wenzetu wengi hawakufanikiwa kuuvuka mwaka uliopita, kutokana na sababu mbalimbali kama ajali na magonjwa.

Mwaka jana ulikuwa na mafanikio na changamoto kadhaa. Kwa mfano baadhi ya majanga yaliathiri baadhi ya watu ikiwamo ajali ya lori la mafuta iliyoua zaidi ya watu 100 katika Manispaa ya Morogoro.

Aidha, mwaka jana mvua kubwa zilizonyesha kuanzia Septemba hadi jana ziliua watu kadhaa, wengine kukosa makazi na kuharibu mazao pamoja na miundombinu kama madaraja na barabara.

Mvua hizo kwa mujibu wa wataalamu, chanzo chake ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaendelea kusababisha athari maeneo mbalimbali duniani.

Hata hivyo, kuna mafanikio lukuki ambayo nchi yetu imeyapata kiuchumi, kijamii na kisiasa. Tulishuhudia uchumi wa taifa ukiendelea kukua, kuwa imara na kuwa tulivu. Mbali na athari za mvua, maeneo mengi ya nchi yalikuwa na chakula cha kutosha, hivyo kuwaepusha wananchi kuathiriwa na uhaba.

Kadhalika, tulishuhudia serikali ikiendeleza kasi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, ikiwamo mikubwa. Itakumbukwa kuwa mwaka jana ndipo ulipozinduliwa ujenzi wa bwawa kubwa la kuzalisha umeme wa megawati 2,100 wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani.

Mwaka huo huo tulishuhudia pia serikali ikizindua rada nne za kisasa kwa ajili ya usalama wa anga katika viwanja vya ndege kadhaa nchini sambamba na barabara za lami, miradi ya maji, vituo vya afya na hospitali katika mikoa kadhaa.

Vita dhidi ya rushwa iliendelea ambapo kesi kadhaa za watuhumiwa wa makosa makubwa zilifunguliwa mahakamani, huku wengine kukiri na kulipa faini kisha kuachiliwa.

Tanzania kwa mwaka jana iliendelea kung’ara kisiasa na kidiplomasia baada ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mwaka wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), ambapo Rais John Magufuli alishika nafasi ya uenyekiti kwa mwaka mmoja.

Vilevile, mwaka jana nchi yetu ilifanya uchaguzi wa serikali za mitaa, ambao uliwahusisha viongozi wa vijiji, mitaa na vitongoji walipatikana. Hata hivyo, kasoro iliyojitokeza na kuzua malalamiko mengi ni vyama vya upinzani kususia kwa madai ya kukiukwa kwa taratibu zilizosababisha wagombea wao wengi kuenguliwa.

Tunapouanza mwaka 2020, hatunabudi kujitafakari upya ili kuzika tofauti zilizojitokeza mwaka jana zinazikwa, ili nchi yetu iendelee kuwa na umoja, amani na mshikamano.

Tunasema hivyo kwa sababu mwaka 2020 utakuwa ni wa uchaguzi, ambapo vyama vya siasa vitakuwa vinashindanisha sera, ilani, mikakati na mipango kwa ajili ya kupata ridhaa ya wananchi.

Ili uchaguzi huo wa madiwani, wabunge na rais uwe huru na haki pamoja na kuendeleza umoja, amani na mshikamano wa kitaifa, mamlaka zinazohusika zihakikishe haki inatendeka kwa kila upande na mazingira ya ushindani yanakuwa sawa.

Wananchi kwa upande wao hawanabudi kutimiza wajibu kwa kuheshimu na kufuata sheria za nchi. Ni matarajio yetu kuwa kila mmoja akitimiza wajibu wake, uchaguzi wetu utakuwa mfano katika jumuiya ya kimataifa.

Suala lingine la msingi ni kila mmoja kwa nafasi yake kufanyakazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo binafsi na taifa kwa ujumla. Wote wanaostahili kulipakodi wahakikishe wanafanya hivyo kwa hiari ili kuiwezesha serikali kuongeza wigo wa mapato, na kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na huduma za msingi kwa wananchi wake.

Habari Kubwa