Kasi zaidi itatakiwa katika baraza jipya la mawaziri

08Oct 2017
Mhariri
Nipashe Jumapili
Kasi zaidi itatakiwa katika baraza jipya la mawaziri

RAIS John Magufuli jana alifanya mabadiliko makubwa katika Baraza la Mawaziri kwa kuteua sura mpya, kuwaacha baadhi ya mawaziri na naibu mawaziri na kuwahamisha baadhi pamoja na kuongeza idadi ya wizara.

Mabadiliko hayo ya jana ni makubwa ya kwanza kufanyika tangu Rais alipotangaza baraza lake la kwanza Desemba 10, 2015 baada ya kuingia madarakani.

Hata hivyo alifanya mabadiliko madogo kujaza nafasi kutokana na baadhi kuwa wazi baada ya uteuzi wa baadhi ya mawaziri kutenguliwa.

Katiba mabadiliko hayo kupitia taarifa ya Kurugenzi ya mawasiliano ya Rais Ikulu, mawaziri wameongezeka kutoka 19 hadi 21 na namba ya mawaziri sasa watakuwa 21 kutoka 16 waliokuwapo awali.

Ongezeko hilo la wizara pamoja na mawaziri na manaibu limetokana na kugawanywa kwa wizara mbili na baadhi ya wizara kuwa na naibu mawaziri wawili.

Wizara zilizogawanywa ni iliyokuwa ya Nishati na Madini na sasa kila sekta itakuwa na wizara yake na ile iliyokuwa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Kutokana na mabadiliko hayo kutakuwa na Wizara ya Kilimo na nyingine ikiwa ya Mifugo na Uvuvi.

Pamoja na kugawanywa kwa wizara, kumekubwa na mabadiliko pia ya mawaziri kwa baadhi waliokuwa manaibu kuwa mawaziri kamili na wengine wakiachwa na sura mpya nyingi zikichomoza.

Miongoni mwa walioachwa ni aliyekuwa Waziri wa maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na Mhandisi Gerson Lwenge wa Maji na Umwagiliaji huku George Mkuchika aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora katika serikali iliyopita, akirejea kwenye wadhifa huo.

Waliopanda ni Selemani Jafo (Tamisemi), Dk. Medard Kalemani (Nishati), Luhaga Mpina (Mifugo na Uvuvi), Isack Kamwelwe (Maji na Umwagiliaji), Dk. Hamis Kigwangalla (Maliasili na Utalii).

Aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumushi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, amekuwa Waziri wa Madini.

Kufanyika kwa mabadiliko hayo, mbali na kujaza nafasi kutokana na kutenguliwa kwa uteuzi wa Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini) na George Simbachawene (Tamisemi) na Mhandisi Edwin Ngonyani (Naibu Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano) waliojiuzulu, yameonyesha kuwa Rais amedhamiria kulisuka baraza kwa ajili ya kuimarisha utendaji serikalini.

Tunasema hivyo kwa sababu mosi, wizara zilizogawanywa zilikuwa na majukumu mengi kiasi cha kuwa na mzigo mkubwa katika utekelezaji wa shughuli ikiwamo kuwahudumia wananchi kwa ujumla.

Wizara ya Nishati na Madini, mathalan, imekuwa ikilalamikiwa na wadau kuwa inapaswa kutenganishwa kutokana na kusimamia sekta nyeti za madini, mafuta na gesi asilia. Hata wakati wa mabadiliko ya baraza la mawaziri Mei, 2012, Rais (mstaafu) alielezea umuhimu wa kugawanywa kwa wizara hiyo lakini haikufanyika hadi mabadiliko ya jana, licha ya kuteua naibu mawaziri wawili- mmoja akisimamia nishati na mwingine madini.

Pili, kuingizwa kwa damu changa (vijana) katiba nafasi za naibu mawaziri kama vile Juliana Shinza (Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo), Abdallah Ulega (Mifugo na Uvuvi), Jumaa Awesso (Maji na Umwagiliaji) na Dk. Faustine Ndugulile (Afya) ni ishara tosha ya dhamira hiyo ya Rais Magufuli katika kutatua kero za wananchi kupitia sekta husika.

Kwa mantiki hiyo, kupitia mabadiliko hayo, wananchi wanatarajia kuwa utendaji serikalini utakuwa wa kasi zaidi kuliko sasa, hivyo kero zilizokuwa zikipigiwa kelele huenda zikapungua kwa kiasi kikubwa au kumalizika.

Tunawatakiwa kila la heri wateule hawa ambao wataapishwa kesho tayari kuanza majukumu mapya kwa wale walioingia na kuhamishiwa wizara nyingine pamoja na waliobaki kwenye nafasi zao.