Kauli ya Majaliwa fedha za Ukimwi ifanyiwe kazi

30Nov 2017
Mhariri
Nipashe
Kauli ya Majaliwa fedha za Ukimwi ifanyiwe kazi

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ametoa kauli kuhusu fedha za Ukimwi, ambayo kama itafanyiwa kazi na wadau wote, fedha hizo zitawanufaisha walengwa ambao ni waathirika wa ugonjwa huo.

Waziri Mkuu amesema kuna umuhimu kwa nchi kupitia Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), kuwa na vyanzo vyake vya kifedha ikiwamo kupanua mifumo ambayo itasaidia kupatikana kwa njia sahihi ya kupambana na tatizo la ugonjwa wa Ukimwi.

Akizungumza wakati akifungua kongamano la kitaifa la maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani juzi, Majaliwa alisema mpaka sasa asilimia 80 ya fedha za kupambana na ugonjwa huo zinatoka kwa wadau na kwamba kuna umuhimu wa kubadilika kwa kuhakikisha kunakuwapo na mfumo mbadala wa kupatikana vyanzo vingine vya uhakika vya fedha badala ya kutegemea wadau pekee.

Alisema kupatikana kwa vyanzo vya uhakika kutasaidia kupambana na tatizo hilo kwa urahisi kuliko kusubiri zichangwe na wadau.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, zaidi ya asilimia 80 ya fedha hizo zinatokana na michango kutoka kwa wadau, huku  asilimia 20 tu ikitoka nchini.

Takwimu hizo zilizotolewa na Waziri Mkuu zinaonyesha kuwa licha ya athari kubwa za Ukimwi kwa Taifa letu, ikiwamo  kupoteza nguvu kazi, bado jamii haijaona umuhimu wa kujijengea uwezo wa kutafuta rasilimali zetu za kukabiliana na ugonjwa huo hatari.

Kama wadau au kwa lugha nyingine washirika wetu wa maendeleo wanachangia asilimia 80 ya fedha za kupambana na Ukimwi, maana yake ni kwamba bila wao hatuwezi kufanya chochote.

Ikumbukwe kwamba taifa lolote haliwezi kuendelea ikiwa linaishi kwa kutegemea fedha za wahisani. Hiyo ni kwa sababu ikitokea wanasitisha misaada kwa sababu zozote zile ikiwamo kuchoka, basi kila jambo linasimama.

Kwa hiyo hali ilivyo nchini katika suala la fedha za kukabiliana na Ukimwi tunapaswa kuchukua hatua sasa za kubuni vyanzo vingine vya kupata fedha za kupamba na gonjwa hilo.

Ushauri wa Waziri Mkuu unapaswa kuwa changamoto kwamba hatua mbalimbali zinapaswa kuchukuliwa ikiwamo kupanua mifumo na wigo katika kupata fedha hizo ambazo zinapaswa kutumiwa vizuri na kuwasaidia walengwa.Huko nyuma washirika wetu wengi wa maendeleo walikuwa wakitoa fedha nyingi kwa ajili ya mapambano dhidi ya Ukimwi, lakini kiasi hicho kimekuwa kikipungua kulingana na vipaumbele vyao.

Hata hivyo, yamekuwapo malalamiko kadhaa kwamba fedha za Ukimwi zimekuwa zikitumika isivyo na kwa kiasi kikubwa kutokuwasaidia walengwa ambao wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) na wagonjwa wa Ukimwi. TACAIDS kikiwa chombo kikuu kinachosimamia mapambano dhidi ya Ukimwi bila shaka imeisikia changamoto ya Majaliwa, na itaifanyia tathmini ya kutosha kabla ya kuanza utekelezaji wake.

Ushauri wetu kwa TACAIDS ni kwamba ikae chini na kupanga namna ya kusaka fedha kwa ajili ya kujiendesha pamoja na kuratibu na kusimamia shughuli zote za Ukimwi. Fedha hizo zitafutwe ndani na nje ya nchi kupitia mikakati mbalimbali badala ya kusubiri kupatiwa fedha za serikali.

Kwa kutumia ubunifu, ni matarajio yetu kuwa fedha za kutosha zitapatikana kwa ajili ya mapambano ya Ukimwi. Suala la msingi ni kuwapo kwa nidhamu ya matumizi ya fedha hizo ili kuwajengea imani ya wanaochangia kuamini kuwa fedha hizo ziko salama.

Jambo la msingi ni kuwa fedha hizo zionyeshe kwamba zinawasaidia walengwa na sio watu wachache wanaotumia fursa ya Ukimwi kwa maslahi yao binafsi.

Tunatoa wito kwa jamii na wadau wote kujitokeza kusaidia kwa kuchangia chochote ili kuchochea mapambano dhidi ya Ukimwi, hivyo kuleta mabadiliko chanya katika jamii yetu.

 

Habari Kubwa