Kibano hiki kitasaidia kudhibiti utoro shuleni

17Dec 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kibano hiki kitasaidia kudhibiti utoro shuleni

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imesema kwamba ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha waraka kudhibiti utoro shuleni ambao pamoja na mambo mengine, utapunguza siku na kuwa chini ya 90.

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Msaidizi Msingi na Uendelezaji wa Sera wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Yesse Kanyuma, alibainisha kuwa siku zitapunguzwa ili kuwe na siku kidogo mwanafunzi asipoonekana shule hatua zichukuliwe haraka.

Kayuma aliyasema hayo alipomwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Akwilapo wakati wa kufunga kongamano la 14 la Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSA).

Hatuna budi kuipongeza serikali kwa hatua hii kwani ni wazi inalenga kudhibiti tatizo la utoro katika shule zetu, na si kumfukuza mtoto bali ni kuwataka wamalize masomo yao.

Inaeleweka kila mzazi, mlezi makini na serikali kwa ujumla wanatamani kuona wanapoanza darasa la kwanza wafike wasome hadi la saba, na watakapoanza kidato cha kwanza wafike kidato cha nne.

Siku 90 zilizokuwa zimewekwa kwa mtoto asipoonekana basi anafukuzwa shule, ndiyo sasa zinatarajiwa kupunguzwa ili kudhibiti utoro ambao unasababisha hasara kwa jamii na serikali kwa ujumla.

Sasa waraka huo utaangalia ni namna gani mwalimu wa darasa, mkuu wa shule, mwalimu wa nidhamu wanaweza kutimiza wajibu wao katika suala zima la usimamizi katika suala zima la utoro shuleni.

Hivyo wakuu wa shule wametakiwa kuwa na kamati hai za nidhamu na ushauri, ili kuondoa hali ya sasa ya fukuza fukuza ya wanafunzi.

Serikali imeona mbali katika jambo hili kwa kuwa licha ya kwamba sekta ya elimu inakabiliwa na changamoto kadhaa, lakini utoro ni miongoni mwa mambo ambayo yanarudisha nyuma taaluma ya elimu.

Tunaamini utoro ukidhibitiwa katika shule zetu, ni wazi kiwango cha ufaulu kitaongezeka, hivyo taifa litaongeza idadi ya wasomi kwa ujumla.

Tunasema hivyo kwa sababu yawezekana kabisa kwamba utoro umesababisha baadhi ya walimu kuvunjika moyo, kuwa wavivu, lakini hali hatua hiyo sasa italeta mabadiliko.

Ni wazi kwamba baadhi ya shule zimekuwa zikitajwa kufanya vibaya kwenye mitihani ya taifa, zikichunguzwa kwa karibu miongoni mwa sababu za matokeo hayo mabaya ni utoro.

Tunafurahi kuona utoro ukidhibitiwa kwa sababu licha ya kuharibu fursa ya watoto hao kupata elimu, lakini umekuwa ni miongoni mwa vyanzo vya kuzalisha makundi ya uhalifu katika maeneo mbalimbali.

Kuna makundi ya vijana wanaovuta bangi na kutumia dawa za kulevya, wengine wanajihusisha na ukabaji, uporaji na vitendo vya ukahaba, wengi wameibukia huko wakianzia kwenye utoro shuleni.

Kadhalika, utoro umekuwa ukikwamisha walimu katika programu zao za kuwafundisha wanafunzi wale ambao hawawi shuleni kwa kipindi kirefu.

Hali hiyo pia imekuwa ikiwaathiri walimu wakati wa kupimwa ufundishaji wao na wakaguzi kutoka serikalini, hivyo ni matumaini yetu kuwa hatua hiyo italeta tija katika maendeleo ya taaluma.

Kimsingi, siku 90 ni muda mrefu sana kwa mwanafunzi kukosekana shuleni, hivyo kutumia udhaifu huo kwenda kufanya shughuli nyingine zikiwamo za kilimo, uvuvi na nyingine ambazo hazimsaidii zaidi ya kumpotezea uwezo kitaaluma.

Tunatamani kuona taifa letu linakuwa ni taifa lenye kiwango kikubwa cha wasomi, ambao watakuwa wanamudu ushindani katika soko la ajira, hivyo kusaidia kuleta maendeleo kwa nchi yetu.

Habari Kubwa