Kijiti hiki cha Dk. Mengi kienziwe Serengeti Boys

13May 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kijiti hiki cha Dk. Mengi kienziwe Serengeti Boys

HATIMAYE kwa majonzi makubwa Alhamisi ya Mei 9, mwaka huu familia, wafanyakazi wa IPP na Watanzania kwa ujumla wakiongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, waliupumzisha mwili wa mpendwa wao, aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi katika nyumba yake ya milele.

Dk. Mengi ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia Alhamisi Mei 2, mwaka huu huko Dubai, Falme za Kiarabu, alizikwa kijini kwao, Nkuu Sinde, Kata ya Machame Mashariki wilayani Hai, Kilimanjaro.

Pamoja na mengi mema ya kukumbukwa ya Dk. Mengi, familia ya soka itabaki kumlilia na kumkumbuka daima kutokana na mchango wake mkubwa katika michezo.

Moja ya mambo ya kukumbukwa ambayo hata hayahitaji kuvuta kumbukumbu ya mbali ni jukumu kubwa alilokuwa amekubali kulibeba takriban miezi mitatu iliyopita la kuwa mlezi wa timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys.

Dk. Mengi aliisaidia mengi Serengeti Boys ikiwa ni pamoja na maandalizi ya michuano ya Mataifa ya Afrika chini ya miaka 17 (Afcon U-17) iliyomalizika hapa nchini kwa Cameroon kutwaa ubingwa huo.

Hakika katika hilo, sote tunakubali kwamba Dk. Mengi ameacha alama muhimu katika medali ya soka nchini na Watanzania wataendelea kumkumbuka daima.

Hivyo, wakati huu tukiendelea kuomboleza msiba wa Dk. Mengi na kumuoba mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, hatuna budi kutafakari na kujitoa kwa hali na mali kwa kuenzi yale yote mema aliyokuwa akiyatenda kwa maendeleo ya taifa letu.

Na kwa wadau wa soka, huu ni wakati sasa wa kujitokeza mapema kupokea kijiti chake cha mlezi wa Serengeti Boys ili kuenzi kazi yake ya kukuza soka nchini.

Nipashe tunatambua lengo la Dk. Mengi lilikuwa ni kuona siku moja Tanzania inatisha katika medali ya soka Afrika na duniani kwa ujumla. Na katika hilo, ndiyo maana bila kuombwa, kwa moyo wake aliamua kuwa mlezi kwenye mzizi wa soka, Serengeti Boys.

Alitambua Tanzania haiwezi kupiga hatua kisoka kama haitawekeza katika soka la vijana ambako ndiko chimbuko lilipo.

Kwa mantiki hiyo, huu ni wakati sasa kwa wadau wa soka kujitokeza kupokea kijiti hicho alichokiachia Dk. Mengi baada ya mauti kumkuta.

Tunatambua wapo Watanzania wengi wenye uwezo wa kubeba jukumu hilo, lakini pia pamoja na wingi huo inawezekana ni wachache wenye moyo wa kuguswa kama ilivyokuwa kwa Dk. Mengi.

Hivyo, Nipashe tukiwa kama wadau wakubwa wa soka nchini, tunawaomba Watanzania wenye mapenzi mema kwa maendeleo ya soka letu kuguswa kwa kukunjua mioyo yao kama Dk. Mengi na kujitokeza kuwa mlezi wa Serengeti Boys.

Ni matarajio yetu wadau wengi watajitokeza kugombania nafasi hiyo na haitasubiri hadi Shirikisho la Soka nchini (TFF) lipige mbiu.

Hilo likitendeka tutakuwa tumemuenzi Dk. Mengi kwa vitendo na hakika tutawafuta majonzi Serengeti Boys ambao ni miongoni mwa Watanzania wengi wanaoendelea kumlilia. Mungu ailaze roho ya Marehemu Dk. Mengi mahali pema peponi.

Habari Kubwa