Kila aliyehusika sakata la Kessy achukuliwe hatua

10Dec 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kila aliyehusika sakata la Kessy achukuliwe hatua

JANA kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi ya wachezaji ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) ilitoa hukumu ya juu ya sakata la muda mrefu la beki wa pembeni wa Yanga, Hassan Kessy na kutoa adhabu kwa klabu ya Yanga.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Yanga imepatikana na hatia ya kutuma jina la Kessy kwa Shirikisho la soka Afrika (CAF) wakati wakijua kuwa mchezaji huyo bado alikuwa na mkataba na klabu ya Simba.

Kutokana na kosa hilo, Yanga imetakiwa kulipa Sh.3,000,000 kama adhabu ya kosa hilo huku pia ikitakiwa kulipa fidia ya Sh. milioni 50 kwa wapinzani wao hao.

Kimsingi, kwa hatua hiyo kamati husika imelimaliza na kulifunga rasmi sakata hilo lililodumu kwa muda mrefu.

Nipashe tunapenda kuipongeza kamati hiyo kwa kulimaliza sakata hilo, lakini pia tungependa kuona mapendekezo ya kamati hiyo waliyoyatia juu ya kiongozi wa juu wa TFF ambaye anahusika na kadhia hiyo anachukuliwa hatua stahiki.

Ni kweli mawasiliano ya Yanga na CAF hayawezi bila kupitia kwa TFF ambaye ndiye mwanachama wa Shirikisho hilo la Afrika.

Kama ambavyo kamati hiyo imeeleza, kiongozi anayetajwa hapo ambaye ni Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwe, alikuwa na uwezo wa kuishauri au kuielekeza Yanga juu ya mchezaji huyo ambaye jina lake lilikuwepo kwenye fomu za klabu hiyo zilizotumwa na TFF kwenda CAF.

Kwa akili ya kawaida kabisa, ni wazi Katibu Mkuu huyo aidha kwa makusudi au bila kukusudia amechangia kutengeneza mgogoro uliokuwa umejitokeza kwa timu hizo mbili kongwe nchini juu ya mchezaji Kessy.

Kama ambavyo haki imetendeka kwa upande wa timu hizi mbili na adhabu iliyotolewa kwa Yanga, ni vyema kwa kamati iliyorudishiwa sakata la Katibu Mkuu nayo ikatenda haki kwa kosa hilo.

Ni wazi Katibu Mkuu kwa nafasi yake angeweza kulimaliza suala hili mapema kwa kuishauri Yanga juu hatua ya kutuma jina la Kesy kwenda CAF wakati bado walikuwa hawajamalizana na Simba waliokuwa na mkataba halali na mchezaji huyo.

Ni aibu kwa chombo kama TFF, mtendaji wake mkubwa ambaye anabeba taswira nzima ya chombo hicho akawa sehemu ya mgogoro huu ambao umemalizwa juzi.

Kasoro kama hizi sio tu zinachafua taswira nzima ya TFF, lakini pia zinaondoa imani ya wanachama wake.

Nipashe tunaona kama kuna yoyote atakayekuwa amehusika na jambo hili mbali na Katibu Mkuu, adhabu itolewe hili kuwa fundisho kwa viongozi wengine wanaokuwa na dhamana juu ya soka letu.

Katibu Mkuu kwa nafasi yake anafahamu zaidi pengine kuliko viongozi wa klabu, juu ya utaratibu na kanuni za usajili wachezaji kwenye michuano ya kimataifa inayoandaliwa na CAF, ili hali akijua mgogoro wa usajili wa Kessy, ingemgharimu kiasi gani kuishauri Yanga juu ya hatua ya kutuma jina la Kessy bila kumalizana na Simba? Au ni ile hali ya kufanya kazi kwa mazoea?, hii ni aibu na si vyema aibu hii ikaendelea au ikajitokeza tena siku za usoni.

Nipashe, tunashauri kama kamati iliyokaa juzi ilivyoamua na kupendekeza, basi haki itendeke na kwa kila aliyehusika ndani ya TFF kuchukuliwa hatua za kinidhamu ili iwe fundisho.

Habari Kubwa