Kila la heri Kilimanjaro, Zanzibar Queens Cecafa

09Nov 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kila la heri Kilimanjaro, Zanzibar Queens Cecafa

MASHINDANO ya kuwania ubingwa wa Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati yanatarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 16 hadi 25 hapa jijini Dar es Salaam.

Michuano hiyo itashirikisha timu nane kutoka katika nchi wanachama wa Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati maarufu Cecafa.

Nchi hizo wanachama ambazo zimethibitisha kushiriki mashindano hayo ni pamoja na wenyeji Tanzania Bara (Kilimanjaro Queens), Zanzibar (Zanzibar Queens), Sudan Kusini, Burundi, Ethiopia, Kenya na Uganda.

Kwa maana hiyo, katika mashindano hayo ambayo hatua ya awali yamepangwa katika makundi mawili, Tanzania itawakilishwa na timu mbili (Kilimanjaro Queens na Zanzibar Queens).

Kama ilivyo kawaida, timu hizo mbili zinahitaji kupata ushirikiano kutoka kwa wadau wa soka nchini, kama ambavyo hufanya kwa kaka zao, Taifa Stars.

Mbali na kuwa wenyeji wa mashindano hayo, Kilimanjaro Queens, ndiyo timu pekee ambayo imeshinda kombe la michuano hiyo ambayo kwa mara ya kwanza ilianzishwa mwaka 2016, ikichezwa katika jiji la Jinja, Uganda.

Kilimanjaro Stars iliweza kushinda kombe hilo kwa kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza na ikafanikiwa kulitetea katika michuano mingine iliyofanyika mwaka jana jijini Kigali, Rwanda. Huu ni mwaka wa tatu na endapo wenyeji hao watafanikiwa kulichukua, itakuwa wanakibakisha jumla kikombe hicho hapa nchini.

Itakuwa si fahari au sifa kwa wachezaji, benchi la ufundi la Kilimanjaro Queens au wasimamizi wa mpira (Shirikisho la Soka Tanzania -TFF), itakuwa ni fahari kwa Watanzania wote na hasa wanamichezo kwa ujumla.

Kilimanjaro Queens na Zanzibar Queens, zinahitaji kupewa hamasa ya kiwango kile kile wanachopewa Taifa Stars, kwa sababu kazi wanayoifanya ya kupeperusha bendera ya Tanzania ni moja.

Zikiwa zimebakia siku chache kabla ya kuanza kwa mashindano hayo, yatakayochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, huu ndio wakati sahihi wa kuona wadau wataisadia timu hiyo na kuacha kusubiri kuwapa zawadi baada ya kulibakisha kombe hilo hapa nchini.

Ili wachezaji wafanye vizuri katika mashindano hayo, wanatakiwa kuandaliwa vema, kuiachia TFF peke yake jukumu la kuiandaa Kilimanjaro Queens na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), kwa kuwaandaa Zanzibar Queens si jambo sahihi.

Kitendo cha kuwa wenyeji wa mashindano hayo kwa mara ya kwanza na kushinda kombe hilo mara mbili, tayari kila timu itakayoshuka dimbani itakuwa imejipanga kuhakikisha inapata matokeo mazuri dhidi ya Kilimanjaro Queens.

Hata hivyo, ili kuendeleza rekodi nzuri, Nipashe linawataka wachezaji na benchi la ufundi la Kilimanjaro Queens, kutobweteka na matokeo waliyopata katika mashindano yaliyopita, na badala yake kujipanga kuwakabili vema wapinzani wao na kulichukua tena kombe hilo.

Kama Kilimanjaro Queens imeweza, Zanzibar Queens pia wanaweza kupambana kuhakikisha wanafanya vema katika mechi zake na hatimaye ndugu hao wawili wakakutana fainali, na hapo tayari watakuwa wamejihakikishia kulibakiza kombe kwenye aridhi ya Tanzania.

Tunasema, hakuna kisichowezekana, kama timu ya vijana ya wanawake (Tanzanite), iliweza kuchukua ubingwa wa COSAFA ugenini Afrika Kusini, Kilimanjaro Queens na Zanzibar Queens, mnaweza pia kulibakisha kombe hili nyumbani kwa Rais John Pombe Magufuli.

Kila la heri Kilimanjaro Queens, Kila la heri, Zanzibar Queens.

Habari Kubwa