Kila la heri Serengeti Boys

13May 2017
Mhariri
Nipashe
Kila la heri Serengeti Boys

VIJANA wetu wa timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 'Serengeti Boys' keshokutwa Jumatatu itaanza rasmi kampeni ya kutwaa ubingwa wa Vijana wa Afrika itakapocheza mchezo wake wa kwanza wa fainali za Afrika dhidi ya Mali.

Timu hii ya Serengeti Boys imekuwa kwenye maandalizi ya nguvu kwa muda mrefu na kwa hapa ni lazima tuwe wa kweli kwa maandalizi na kwamba timu hii ilivyoandaliwa na Shirikisho la soka nchini (TFF) wanapaswa kupewa pongezi za dhati kwa kuwekeza kwa timu hii.

Nipashe tunafahamu kufanya vizuri kwa timu hii sifa hazitakwenda kwa TFF peke yake, bali taifa zima la Tanzania.

Maandalizi ya timu hii yamefanyika kikamilifu, kwa kuanzia, Serengeti Boys imecheza michezo mingi ya kirafiki na timu mbalimbali katika kuelekea kwenye fainali hizi za Afrika.

Ikumbukwe Serengeti Boys imecheza na timu tano tofauti na zote imecheza nao mara mbili ukiondoa Ghana.

Ilianza kwa kucheza na Burundi mara mbili mjini Bukoba, na kupata ushindi katika michezo yote, ikarejea jijini Dar es Salaam na kucheza na Ghana kwenye uwanja wa Taifa na kufanikiwa kupata sare ya bao 2-2.

Kisha ikaelekea Morocco ambako huko ikacheza michezo miwili na wenyeji wa fainali hizi za vijana za Gabon na kufanikiwa kupata ushindi katika michezo yote miwili kabla ya kuelekea Cameroon ambako nako walicheza michezo miwili dhidi ya timu ya vijana ya nchi hiyo na kufanikiwa kushinda mchezo mmoja na kupoteza mchezo mmoja.

Kwa mantiki hiyo Nipashe tunaamini timu yetu hii ya vijana imepata maandalizi mazuri na kuleta matumaini ya kufanya vizuri kwenye michuano hii ya Afrika.

Kwa ratiba ya michuano hii, Serengeti Boys itatupa karata yake ya kwanza keshokutwa Jumatatu dhidi ya Mali, kiujumla vijana wetu wataingia uwanjani huku wakiwa wameondolewa uoga wa kukutana na timu za mataifa makubwa.

Kikubwa Nipashe tunashauri Watanzania kwa ujumla wetu kuiunga mkono timu yetu ili iweze kufanya vizuri katika michuano hii.

Kikubwa Watanzania wanapaswa kufahamu, endapo Serengeti Boys watafanya vizuri kwenye michuano hii na kufika angalau hatua ya nusu fainali pamoja na kuwa itakuwa imeweka historia ya aina yake lakini pia itakuwa imekata tiketi ya kushiriki fainali za vijana za Dunia.

Nipashe tunaamini jambo hilo linawezekana kama tu vijana wetu wataenedelea kupambana kwenye fainali hizi zinazoanza kesho nchini Gabon.

Ikumbukwe Tanzania haijawahi kushiriki fainali hizi, mwaka 2004 ilifanikiwa kufuzu kwenye michuano hii lakini iliondolewa kutokana na kashfa ya kuchezesha 'kijeba' ambapo mchezaji wa zamani wa klabu za Simba na Yanga, Nurdin Bakari ndiye aliyebainika kuwa na umri mkubwa na hivyo Tanzania kuondolewa kwenye michuano hiyo.

Kwa pamoja tuendelee kuiunga mkono timu yetu na kwa wale wenye uwezo wa kuungana nao nchini Gabon itakuwa jambo jema na kuwatia moyo wachezaji wetu.

Kwa kufahamu ushindi wa Serengeti Boys ni ushindi wa Watanzania wote, Nipashe tunaitakia kila heri timu yetu kwenye fainali hizi zinazoanza kesho nchini Gabon.

Kwa pamoja tunasema Gabon mpaka kombe la Dunia kwa Serengeti Boys inawezekana, tunaitakia kila la heri na dua zetu tutaelekeza kwa Serengeti Boys.