Kila la kheri Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes

02Dec 2017
Mhariri
Nipashe
Kila la kheri Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes

MASHINDANO ya kuwania ubingwa wa Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati yanatarajiwa kufanyika kuanzia kesho Desemba 3 hadi 17 mwaka huu huko nchini Kenya.

Katika mashindano hayo, Tanzania itawakilishwa na timu mbili ambazo ni Kilimanjaro Stars inayotoka upande wa Tanzania Bara na Zanzibar itawakilishwa na timu yake ambayo maarufu inajulikana kwa jina la Zanzibar Heroes.

Mbali na timu hizo za Tanzania ambayo Zanzibar hutambulika kama nchi mwanachama, timu nyingine zinazotarajiwa kuchuana kwenye michuano hiyo ni pamoja na Rwanda, Libya (wageni) na  wenyeji Harambee Stars ya Kenya ambazo zimepangwa katika Kundi A.

Nyingine ni mabingwa watetezi Uganda (The Cranes), Burundi, Ethiopia na Sudan Kusini ambazo zimepangwa katika Kundi B, huku ratiba ya michuano hiyo ikionyesha kuwa kila kundi litatoa timu mbili zitakazosonga mbele kucheza hatua ya nusu fainali huku.

Kilimanjaro Stars inayonolewa na Kocha Mkuu, Ammy Ninje, itaanza kampeni za kuwania ubingwa huo mwaka huu kwa kucheza na timu ya Libya hapo kesho wakati Zanzibar yenyewe itashuka dimbani kwa mara ya kwanza Jumanne Desemba 5 kuchuana na Rwanda (Amavubi).

Katika kuhakikisha kuwa Kilimanjaro Stars inapata muda wa kujiandaa na mashindano hayo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lililazimika kusimamisha mechi za Ligi Kuu Bara sambamba na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) ligi zao  ili kuzipa timu nafasi ya kujiimarisha kabla ya kuelekea kwenye michuano.

Gazeti hili tunaamini wachezaji na benchi la ufundi la Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes watapeperusha vyema bendera ya nchi katika michuano hiyo na hatimaye kurejea nchini na kombe.

Kama ambavyo tunatarajia kuona ushindani pale timu hizi mbili zitakapokutana katika mchezo utakaofanyika Desemba 7 mwaka huu, hali hiyo ya kucheza kwa bidii na jihadi inatakiwa ionekane katika mechi zote ambazo watashuka uwanjani.

Wachezaji wa Kilimanjaro Stars ambao walipewa baraka za kufanya vizuri na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, mnatakiwa kila dakika mkumbuke kauli yake kwamba mnakwenda kwenye michuano hiyo kwa niaba ya Watanzania na hivyo mnatakiwa kupambana.

Waziri huyo aliwaambia kuwa nchi inataka kikombe na wakifanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali, atawafuata ili kuongeza nguvu. 

Ni muda mrefu umepita kwa Tanzania kushinda kombe la mashindano hayo, mara ya mwisho ikiwa ni mwaka 2010 wakati ikiwa chini ya Kocha Mkuu wa Taifa Stars/ Kilimanjaro Stars, Jan Poulsen.

Mbali na kuiletea nchi sifa, michuano hiyo ni nafasi nyingine kwa wachezaji wa Tanzania kutangaza vipaji vyao na hatimaye kuzivutia klabu mbalimbali za nje ya Tanzania kuwasajili.

Maandalizi mazuri zikiwamo posho, ni moja ya masuala ambayo tunaamini wachezaji watatakiwa kupambana ili kulipa deni la kurejea na ubingwa na kuwapa furaha Watanzania.

Kufanya vizuri kwa timu za Tanzania kwenye mashindano hayoa kutasaidia kuwapunguzia "machungu" mashabiki wa soka nchini ambao wanaiona michuano hiyo kama AFCON -ndogo ambayo timu yetu ya Taifa (Taifa Stars) haijashiriki kwa zaidi ya miaka 37 sasa.