Tanzania imebakiza timu moja tu inayoshiriki katika mashindano hayo ambayo ni Simba baada ya Yanga, Azam FC, Biashara United zote za Bara kutolewa mapema katika michuano hiyo ya kimataifa.
Kwa upande wa Zanzibar, timu za KMKM na JKU pia zilitolewa mapema katika michuano hiyo na kuifanya Simba kuwa wawakilishi pekee wa Tanzania waliobakia kwenye mashindano hayo ya juu kwa Afrika kwenye ngazi ya klabu.
Simba iko katika Kundi D ikiwa pamoja na RS Berkane ya Morocco, ASEC Mimosas (Ivorry Coast) na USGN ya Niger.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba walioko chini ya Kocha Mkuu Mhispania Pablo Franco walihamia katika michuano hiyo baada ya kutolewa na Jwaneng Galaxy ya Botswana kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba inaingia katika hatua hiyo ya makundi kwa kuwawakilisha Watanzania wote na kufanya kwao vizuri kutaendelea kuitangaza na kuipa heshima nchi yetu ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa pia ikiiwakilisha vyema Afrika Mashariki.
Wadau na mashabiki wa soka huu ni wakati wa kuungana na kuiombea Simba mafanikio kwa sababu kusonga kwao mbele kwenye michuano hiyo kutasaidia kuipa nchi nafasi ya kupata tiketi nne katika msimu ujao wa mashindano hayo yanayoandaliwa na kusimamiwa na CAF.
Tunaamini kama wadau watashirikiana kwa dhati kuhakikisha Simba inafanya vizuri kwenye mechi zake za nyumbani na ugenini kwenye hatua hii ya makundi, basi nafasi ya kusonga mbele itakuwa nyepesi na haitakuwa na mabonde kama ambavyo inatarajiwa.
Kimsingi kila mdau anafahamu kusonga mbele kwa Simba hakutaifaidisha klabu hiyo peke yake, bali matunda ya matokeo chanya yatakayovunwa kwenye hatua hiyo, yatailetea nchi faraja ya kupata wawakilishi wengi zaidi katika msimu ujao wa michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.
Licha ya Simba kuwa na uongozi wake, naamini viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wameshakutana na wawakilishi hao ili kuhakikisha kila jambo linalotakiwa kutekelezwa kuelekea hatua hiyo muhimu limekamilika kwa sababu ya kuweka mbele maslahi ya nchi na si kuonekana wanaipendelea.
Inajulikana wazi Simba ikiendelea kusonga mbele, itavuna fedha zaidi kutoka CAF, hali kadhalika TFF pia hupata fungu lake lakini wafanyabiashara mbalimbali kuanzia wa usafiri, hoteli na vyakula hupata fedha kutokana na uwapo wa michezo hiyo ya kimataifa.
Vitendo vya kuendelea kuwashangilia wageni tuone ni vya kishamba kwa sababu mbali ya kujiombea wenyewe dua mbaya, lakini vinaendelea kulidhalilisha taifa kwa sababu mashabiki wa nchi nyingine hawafanyi hivyo.
Pia tunawakumbusha wachezaji wa Simba kuhakikisha wanacheza kwa viwango vya juu ili kuhakikisha timu yao inafikia malengo iliyojiwekea ya kutinga hatua ya nusu fainali, lakini wafahamu hatua hii ni daraja lingine linaloweza kuwaweka sokoni na hatimaye kununuliwa na klabu za nje ya Tanzania au bara la Afrika.
Tunawashauri wachezaji watakaopata nafasi ya kucheza mechi za hatua hii ya makundi, wajue si wanafuatiliwa na makocha wa ndani, michuano hii hufuatiliwa na mawakala na makocha kutoka sehemu mbalimbali duniani ikiwa inafuata kwa ngazi ukiondoa Ligi ya Mabingwa Afrika na baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Tuungane pamoja kuiombea dua njema Simba kwa faida ya Tanzania na kusahau upinzani wa hapa kwa faida ya kizazi kijacho ambacho kinajifunza kutokana na yale wanayoshuhudia sasa kutoka kwa wakubwa zao.