Kila la kheri uchaguzi TFF leo, 'wasaka tonge' waepukwe

07Aug 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kila la kheri uchaguzi TFF leo, 'wasaka tonge' waepukwe

WADAU wa soka nchini na Watanzania kwa ujumla, leo wanatarajia kupata uongozi mpya wa juu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), katika Uchaguzi Mkuu wa shirikisho hilo utakaofanyika jijini Tanga.

Viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi huo, ni Rais wa TFF pamoja na wajumbe wa sita wa Kamati ya Utendaji huku wajumbe wengine watano wa kamati hiyo ya utendaji wakipatikana kwa kuteuliwa na rais baada ya uchaguzi huo kufanyika.

Kiongozi mwingine wa juu katika shirikisho hilo atakayeingia madarakani leo ni makamu wa rais, ambaye atapatikana kwa kuteuliwa na rais na kisha kupigiwa kura na wajumbe wa mkutano mkuu.

Hata hivyo, Rais wa TFF, Wallace Karia, anayetetea nafasi yake, anachosubiri ni kuidhinishwa tu kuendelea kukalia kiti hicho kutokana na kuwa mgombea pekee aliyekidhi vigezo vyote katika mchakato wa uchaguzi huo ulioanza tangu Juni 8, mwaka huu kabla ya kuhitimishwa baadaye leo.

Hata hivyo, hadi kufikia hatua hii ya kufanyika uchaguzi huo, tunatambua mchakato mzima uligubikwa na mvutano mkubwa na hadi sasa wapo baadhi ya wagombea ambao wamekwenda mahakamani wakipinga namna ulivyoendeshwa kutokana na kutokukubaliana na baadhi ya kanuni ambazo ziliwaengua.

Lakini mahakama haikuona sababu ya msingi ya kuzuia uchaguzi huo kufanyika na kutoa baraka zote, jambo ambalo leo wadau wa soka na Watanzania kwa ujumla watashuhudia viongozi wao watakaokabidhiwa dhamana ya kusimamia mpira wa miguu nchini kwa kipindi kingine cha miaka minne.

Nipashe hatutaki kuingilia uhalali wa waliofikisha kesi mahakamani ama ambao hawakuridhishwa na mchakato mzima wa uchaguzi hadi viongozi hao wanapatikana leo jijini Tanga.

Cha msingi tunachotaka kukiweka wazi kwa wadau wote wa soka na Watanzania kwa ujumla, ni kila mmoja kuona haja ya kushirikiana vema na uongozi utakaopatikana leo katika juhudi za kuhakikisha soka letu linapiga hatua zaidi kutoka hapa lilipo sasa.

Tunatambua hata ambao walienguliwa awali katika mchakato wa uchaguzi huo na wale watakaokosa kura za kutosha leo, wote lengo lao lilikuwa moja tu, kuhakikisha soka la Tanzania linapiga hatua zaidi na kuwa katika viwango vya juu barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Hivyo, kama dhamira yao ilikuwa hiyo, hawatasita kuendelea kuwaunga mkono viongozi watakaochaguliwa leo kwa kutoa michango kwa hali na mali na zaidi mawazo yao kuwa muhimu katika uboreshaji wa soka Tanzania.

Kinyume cha kufanya hivyo, kinatufanya kutambua dhamira na malengo yao makubwa ilikuwa ni kuusaka uongozi huo kwa maslahi yao binafsi na haikuwa kuusaidia mpira wa Tanzania kwa ajili ya maslahi mapana ya taifa letu.

Tunafahamu wazi, wapo 'wasaka tonge' na si kwa ajili ya kuusaidia mpira wa Tanzania, hivyo Nipashe tunawataka wajumbe wa mkutano mkuu kutowapa kura na hata kama wamefanikiwa kupenya kwa kuchaguliwa ama kuteuliwa katika uchaguzi huo wa leo, basi huu ni wakati sasa wa kuziacha fikra zao 'mfu' na kubadilika mara moja kwa kuwa na mawazo chanya ya kulisaidia soka la Tanzania kwa maslahi mapana ya taifa kwa ujumla.

Aidha, ni wakati sasa wa kuvunja makundi na kambi zote za uchaguzi, na wote kuungana kwa kuwa kitu kimoja katika kulijenga soka la Tanzania, kwa sababu watakaochaguliwa au kuteuliwa leo katika nafasi mbalimbali na wale watakaoshindwa ama waliokosa nafasi hiyo tangu kuanza kwa mchakato huo, wote lengo lao lilikuwa ni kujenga nyumba moja ya soka, hivyo hawana sababu ya kuanza kugombania fito.

Habari Kubwa