Kila la kheri watahiniwa mtihani darasa la saba

06Sep 2017
Mhariri
Nipashe
Kila la kheri watahiniwa mtihani darasa la saba

WANAFUNZI zaidi ya 900,000 wa darasa la saba wanatarajiwa kuanza mitihani yao ya elimu ya msingi leo na kukamilisha kesho.

Kwa mujibu wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), idadi ya wanafunzi hao imeongezeka kwa kuwa na ziada ya wanafunzi 200, 000 kulinganisha na wale waliofanya mitihani hiyo mwaka jana, sababu ikiwa ni pamoja na kuanza kuonekana kwa matokeo chanya ya mpango wa serikali ya awamu ya tano wa kutoa elimu bure kwa kila mtoto kuanzia wa msingi hadi kidato cha nne.

Sisi tunawatakia kheri wanafunzi wote wanaofanya mitihani hiyo kuanzia leo, tukiamini kuwa watafanya vizuri na kuvuka daraja hilo muhimu kuelekea sekondari na mwishowe katika vyuo vya elimu ya kati na ya juu.

Ni imani yetu kuwa hadi kufikia leo, kila mmoja miongoni mwa watahiniwa amejiandaa vya kutosha. Miaka saba ya kujifunza na kufanya majaribio mbalimbali kabla ya mitihani inayoanza leo inatosha kwa kila mmoja wao kufanikisha lengo la kufaulu na kuvuka hatua hiyo salama.

Jambo pekee la kukumbuka kwa kila mtahiniwa, ni kuhakikisha kwamba hofu haiwi sehemu ya mambo ya kuyapa kipaumbele. Wajiamini juu ya waliyofundishwa na kuyapokea kwa ukamilifu katika miaka saba ya kupata elimu hiyo.

Kama ilivyo kwa mitihani mingine mingi waliyoifanya hapo kabla, ndivyo wanavyopaswa pia kufanya ndani ya vyumba vyao vya mitihani leo.

Na ili kufikia malengo yao, hakuna namna nyingine isipokuwa ni kutulia, kuweka kando hofu na kusoma maswali kwa umakini ili wayaelewe kabla ya kuanza kuyajibu.

Aidha, ni muhimu pia kwa kila mmoja wao kujiepeusha na vitendo vya ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za mitihani.
Wajiepushe na vitendo vya udanganyifu kwenye mitihani na badala yake watumie maarifa yao wenyewe, kwa kujua kuwa hakuna litakaloulizwa nje ya kile kilichomo kwenye muhtasari wao wa masomo.

Kinyume chake, kujihusisha na vitendo vyovyote vile vya ukiukaji wa sheria za mitihani, ni sawa na kujiweka katika hatari ya kufutiwa matokeo yao na hivyo kujiharibia uwezekano wa kuvuna matunda mema ya kazi kubwa ya maandalizi waliyofanya kwa ajili ya mitihani hiyo.

Aidha, Nipashe tunaona kuwa angalizo lingine muhimu linapaswa pia kwenda kwa wazazi wenye watoto wanaofanya mitihani leo na pia walimu wao.

Kwamba, wazazi au walezi wa watahiniwa hao wajitahidi kuwapa maneno ya kuwafariji na siyo kuwatisha juu ya kile wanachokwenda kukifanya kwenye vyumba vya mitihani.

Kwa walimu, lililo muhimu zaidi kwao katika kila shule ni kuona kuwa hakuna ukiukwaji wa sheria ambao mwishowe unaweza kusababisha madhara kwa shule yao, ikiwamo kwa watoto wao kufutiwa mitihani na NECTA.

Nao wanapaswa kujiamini juu ya kazi kubwa waliyoifanya katika kuwaandaa watoto wao na hivyo, wawaache sasa wafanye mitihani kwa uwezo wao.

Mathalani, haitakuwa busara hata kidogo kusikia kuwa kuna walimu wamejipanga kufanya udanganyifu kwa kuwasadia watoto wao kujibu maswali ya mitihani.

Kwa maadili ya ualimu, jambo hilo kamwe halikubaliki. Na kisheria, hilo ni kosa kubwa la jinai linaloweza kuwatia matatani wahusika wote, achilia mbali athari mbaya kwa shule zitokanazo na uwezekano wa kufutwa kwa matokeo ya mitihani yao. Bali, walimu waridhike juu ya maandalizi waliyowapa watoto wao katika kipindi chote cha miaka saba na sasa kuwaachia uwanja wa kuvuna kile walichopanda.

Kila la kheri darasa la saba. Mungu awajaze maarifa ili mfanye vyema katika mitihani yenu ya kuhitimu elimu ya msingi.

Habari Kubwa