Kila la kheri wawakilishi wetu michuano ya CAF

11Sep 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kila la kheri wawakilishi wetu michuano ya CAF

WAWAKILISHI wengine wa Tanzania Bara kwenye michuano ya kimataifa; Azam FC na Yanga, watashuka dimbani leo na kesho katika viwanja tofauti kuipeperusha bendera ya nchi baada ya jana Biashara United kubeba jukumu hilo kwa kuvaana na Dikhil ya Djibouti kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Biashara yenyewe ilianzia ugenini nchini Djibouti wakati Azam FC ambayo nayo inaiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, leo majira ya saa 1:00 usiku ikitarajiwa kuikaribisha Horseed FC ya Somali katika Uwanja wao wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.

Kwa upande wa Yanga inayoiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kesho itashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa majira ya saa 10: 00 jioni kuikaribisha Rivers United ya Nigeria katika mechi ya awali ya mashindano hayo yanayoongoza kwa utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu Afrika.

Tukiachana na matokeo iliyoyapata Biashara United, jana, macho yote ya mashabiki wa soka nchini na Watanzania kwa ujumla, sasa yanaelekezwa kwa Azam FC leo na Yanga kesho, kila mmoja hususan wapenda maendeleo ya mpira wa miguu nchini akitaka kuona zinapata ushindi wa kishindo ili kurahisisha kazi kwenye mechi za marudiano mwishoni mwa wiki ijayo.

Ndiyo, tunaamini hivyo kwa kuwa Nipashe ni mdau namba moja wa sekta ya michezo nchini, kwa mantiki hiyo daima malengo yetu nikuona soka kama ilivyo michezo mingine ikipiga hatua kuanzia ile inayoshirikisha mchezaji mmoja mmoja, klabu hadi timu za taifa.

Tunafahamu kama mchezaji yeyote ama klabu atapata/itapata matokeo chanya pamoja na sifa kuelekezwa kwao, lakini bado itajenga heshima kubwa kwa soka la Tanzania kwa ujumla na kuzidi kupandisha viwango kuanzia ngazi ya klabu hadi nchi kwa mchezo husika.

Wote tunatambua kwamba hadi Tanzania inafikia hatua ya kuingiza timu nne kwenye michuano ya kimataifa, ilitokana na Klabu ya Simba kufanya vizuri kwa kufika hatua ya robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa kuanzia msimu wa 2018/19 hadi 2020/21, hivyo kuiongezea Tanzania pointi na kuwa moja kati ya nchi 12 zenye sifa ya kuingiza idadi hiyo katika mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF, yaani mbili Kombe la Shirikisho na mbili Ligi ya Mabingwa.

Kwa mantiki hiyo, tukiweka itikadi zetu za klabu mbali, ushindi wa timu yoyote kwenye michuano ya kimataifa si mafanikio tu kwa klabu husika, bali ni kwa Tanzania kwa ujumla, hivyo huu ni wakati sahihi kwa Watanzania wote kuwaunga mkono wawakilishi wetu hao kimataifa.

Tunatambua tayari CAF imepiga maarufu mashabiki kuhudhuria uwanjani kutokana na janga la ugonjwa wa COVID-19, unaoukabili duniani kwa sasa, lakini hiyo haiwezi kuwa sababu ya kushindwa kuwapa sapoti wachezaji na timu zetu hizo kimataifa.

Katika hilo, leo tungependa kuona nchi yote ikibadilika rangi na kuwa bluu na machungwa kwa kuvaa jezi za Azam FC huku kesho rangi hizo zikibadilika na kuwa kijani na njano ambazo zinazovaliwa na Yanga.

Kwa kufanya hivyo, kila wanapopita wachezaji na kushuhudia hali hiyo, watatambua kuwa mashabiki na Watanzania kwa ujumla wapo nyuma yao, hivyo wanadeni kubwa la kuwalipa kwa kuhakikisha wanapata matokeo uwanjani.

Hivyo, kubwa kwa sasa tunawatakia kila la kheri wawakilishi wetu hao kimataifa, lakini kuanzia viongozi wa klabu, benchi la ufundi hadi kwa wachezaji, hawana budi kutambua Watanzania wote wapo nyuma yao na wanachokitaka ni matokeo chanya kwa kupata ushindi wa kishindo na si vinginevyo.

Habari Kubwa