Kila la kheri Yanga, hakuna kisichowezekana katika soka

16Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kila la kheri Yanga, hakuna kisichowezekana katika soka

LEO ni siku nyingine tena wawakilishi pekee wa Tanzania waliobakia katika mashindano ya kimataifa, Yanga ya jijini Dar es Salaam wanatarajia kushuka kwenye Uwanja wa Taifa kucheza mechi yake ya tatu ya hatua ya makundi.

Katika mechi ya leo ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga inawakaribisha Medeama kutoka Ghana, mchezo utafanyika kuanzia saa 10:00 jioni.

Yanga itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi mbili zilizopita. Ilianzia ugenini Algeria kwa kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa wenyeji Mo Bejaia na iliporejea nyumbani ikapoteza mchezo wa pili dhidi ya mabingwa wa zamani wa Afrika TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

TP Mazembe ambayo iliongozwa na mshambuliaji Mtanzania Thomas Ulimwengu pia iliwafunga Yanga bao 1-0 na kufanikiwa kuongoza kundi hilo baada ya kufikisha pointi sita.

Mechi ya leo Yanga inatakiwa iwe makini zaidi kuhakikisha inashinda ili iweze kurejesha matumaini ya kuwa kwenye mbio za kusaka ubingwa huo unaoshikilia na timu ya Etoile du Sahel ya Tunisia.

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm anatakiwa kuhakikisha anapanga wachezaji walio tayari kupambana kwa ajili ya kusaka ushindi na si matokeo mengine.

Pamoja na safari hii Yanga haikusafiri kwenda nje ya nchi kujifua, gazeti hili linaamini kwamba mazoezi yaliyofanyika chini ya Mdachi huyo yatakuwa yamerekebisha makosa yaliyojitokeza katika mechi mbili zilizopita na sasa ni wakati wa kuanza kuwakimbiza wapinzani wake na hatimaye kusonga mbele.

Kwenye soka hakuna kisichowezekana, kupoteza mechi mbili za mwanzo sio mwisho wa mashindano. Pluijm alisema pia baada ya kumalizika kwa mechi dhidi ya TP Mazembe kuwa bado kikosi chake kina nafasi 'kimahesabu' endapo itafanya vizuri katika mechi nne zilizobakia na hatimaye kutinga nusu fainali.

Kama ilivyoweza kushinda vikombe viwili msimu uliomalizika (Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara 2015/16 na Kombe la Shirikisho (FA), Yanga inatakiwa kushuka uwanjani leo ikiwa na kasi na uchu wa kushinda kombe hilo la Afrika.

Ushindani waliouonyesha kwenye mechi za ndani, wanatakiwa kuuendeleza katika mashindano haya na hatimaye kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Wachezaji wapya waliosajiliwa nao wanatakiwa kuongeza nguvu ili usajili wao uonekane kuwa na tija kwa kusaidia kupatikana kwa ushindi kama ilivyokusudiwa na benchi la ufundi.

Pia hamtakiwi kuingia uwanjani huku mnawadharau wapinzani wenu, hilo litakuwa ni kosa na litawapa nafasi Medeama kuonekana wako nyumbani.

Huku timu ikisaka rekodi mpya ya kutinga nusu fainali, wachezaji wa Yanga wanatakiwa kufahamu kupitia michuano hiyo wataweza kujinadi na kujiweka sokoni.

Nahodha wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) Mbwana Samatta sasa anacheza soka la kulipwa kwenye klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, hiyo ilitokana na juhudi alizozionyesha wakati akiwa na TP Mazembe.

Hii ni nafasi yenu wachezaji wa Yanga ambao kweli kwenye mioyo yao walisema kwamba klabu hiyo ni daraja la kuwapeleka Ulaya.

Watanzania bila kujali mapenzi na klabu zetu, tuungane kuwatakia kila la kheri wawakilishi hawa wa nchi katika mashindano hayo ya CAF na hatimaye kufuta jina la kuwa wasindikizaji kwenye michuano ya kimataifa.

Habari Kubwa