Kilimo kiboreshwe kuunga mkono uchumi wa viwanda

09Aug 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kilimo kiboreshwe kuunga mkono uchumi wa viwanda

JANA wakulima nchini waliadhimisha siku yao ya Nanenane, ambayo ilikwenda sambamba na maonyesho ya kilimo, mifugo na uvuvi katika ngazi za wilaya, mikoa kanda huku kitaifa yakifanyika Mkoa wa Lindi.

Mambo mbalimbali yalizungumzwa na wataalamu wa kilimo, viongozi wa kisiasa pamoja na wadau takribani wiki nzima kabla ya kilele chake jana, wakitoa na ushauri kwa wakulima pamoja na mambo mengine, kuwahimiza matumizi ya zana bora katika kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji.

Bila shaka wakulima walioshiriki katika maonyesho hayo aidha kwa kupeleka bidhaa zao na wengine waliotembelea mabanda watakuwa wamenufaika na watautumia ujuzi na ushauri walioupata kuzalisha bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi kwa njia za kisasa sambamba na kuongeza uzalishaji.

Kwa kuwa mpango wa Serikali ni Tanzania kuingia katika uchumi wa kati kupitia viwanda, ni wakati mwafaka sasa kuelekeza jitihada zote katika kuboresha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuwa kuboreshwa kwa sekta hiyo ndiyo njia ya kuelekea katika viwanda.

Mapinduzi ya viwanda yaliyotokea kwa mara ya kwanza Uingereza katikati ya karne ya 18 na baadaye nchi kadhaa za Ulaya katika karne ya 19 yalichochewa na mambo kadhaa, kubwa ni mapinduzi ya kilimo ambayo yalisababisha kuzalisha malighafi za kutosha kwa ajili ya kutumiwa na viwanda kuzalisha bidhaa.

Kwa kuzingatia umuhimu wa kuboresha kilimo kuelekea uchumi wa viwanda, katika hotuba yake ya kilele cha sikukuu ya Nanenane jana mjini Lindi, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alihimiza uzalishaji wa bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi zilizoongezwa ubora ambazo zitatumika kama malighafi za kutengeneza bidhaa kupitia viwanda vidogo.

Makamu wa Rais alihimiza viwanda vidogo vizalishe bidhaa kwa ajili ya masoko ya nje kwa ajili ya kuingiza fedha za kigeni na kusaidia kutengeneza ajira asilimia 40 kupitia sekta ya viwanda.

Alieleza jitihada kadhaa ambazo zimekuwa zikifanywa na serikali katika kuboresha kilimo ikiwamo kuongeza bajeti ya wizara kutoka Sh. bilioni 433.4 mwaka 1995/96 hadi Sh. trilioni 1.16 mwaka 2015/16, kuongeza idadi ya maofisa ugani pamoja na idadi ya vituo vya utafiti wa kilimo sambamba na kuviongezea bajeti na rasilimali watu. Hata hivyo,
zinahitajika jitihada zaidi katika kuboresha kilimo ili kufanikisha mpango wa kuingia uchumi wa kati kupitia viwanda.

Sekta ya kilimo imeajiri Watanzania zaidi ya asilimia 75, lakini kiuhalisia hawa sio wazalishaji wanaoweza kuzalisha na kutosheleza mahitaji ya viwanda ambavyo Serikali inaahidi kuwa vitajengwa. Wakulima wengi tulio nao ni wale wanaozalisha kwa ajili ya kujikimu na ziada kidogo ndiyo wanayoiuza.

Katika kuhakikisha kwamba tumedhamiria kuzalisha kisasa kwa ajili ya viwanda, kuna haja ya kubinafsisha kilimo kwa wawekezaji makini kutoka nje pamoja na kuwawezesha wazalishaji wakubwa wazalendo ili wazalishe malighafi kwa ajili ya viwanda.

Kilimo ni sekta inayohitaji mtaji mkubwa na muda mrefu wa kupata faida, tofauti na sekta nyingine na ndiyo maana hadi leo hawajitokezi wawekezaki katika kilimo.

Tunakubaliana na ushauri wa baadhi ya wataalamu wa kilimo kwamba ni lazima mfumo wa kilimo kinachofanywa nchini ubadilishwe na watu wachache wawe wanalima kwa njia za kisasa na kutosheleza soko huku wengine wakiwa wanafanya kazi za kusaidia wakulima hao.

Tunaishauri Serikali kwamba ni wajibu wake kuweka mazingira bora ya kuwavuta wawekezaji wakubwa na makini wajitokeze na wajikite katika kilimo kwa ajili ya kuzalisha ili kutosheleza mahitaji ya viwanda.

Habari Kubwa