Kilio cha wafanyakazi kipate jawabu Mei Mosi

14Apr 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kilio cha wafanyakazi kipate jawabu Mei Mosi

JUZI Rais wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (TUCTA), alieleza matarajio makubwa waliyonayo kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kuelekea maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Mei Mosi.

Matarajio ambayo yamekuwa kilio cha muda mrefu ni nyongeza ya mishahara ambayo haijafanyika kwa miaka mitano, huku bei za bidhaa na vyakula zikipanda na kushuka kila wakati, jambo ambalo limechangia kupungua kwa morali ya kazi.

Kwa miaka mitano serikali haijaongeza mishahara ya wafanyakazi na ahadi kubwa ilikuwa ni kufanya hivyo.

Februari 8,2019, Waziri Mkuu akijibu swali la aliyekuwa Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga, juu ya ongezeko la mishahara kwa watumishi, aliwataka kuwa na subira wakati serikali inaendelea na mchakato wa kuwatambua watumishi wa umma halali na kufanya ulinganifu katika kada mbalimbali, ili waanze kulipwa mishahara stahiki.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2020, aliyekuwa mgombea urais wa CCM, ambacho ndiyo kimeunda serikali, katika moja ya ahadi zake ni ongezeko la mishahara kwa watumishi.

Februari 11, mwaka huu, akijibu swali la Mbunge wa Konde, Khatibu Said Haji, katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, aliwataka watumishi wasikate tamaa kwa vile mishahara mipya haijatangazwa na badala yake wachape kazi kwa kuwa maslahi yao yanaendelea kuboreshwa.

Kwamba serikali ya awamu ya tano ilivyoingia madarakani ilibaini kwamba ikitangaza kupandisha mishahara, itaumiza watu wengi kwa kuwa gharama za bidhaa hupandishwa haraka. Pia, inapotangaza mishahara kupanda inapelekea ugumu wa maisha kwa kuwa huduma nyingine kwenye masoko ama usafiri wa mabasi zinapanda.

Lakini pia, kupandisha mshahara kwa Sh. 20,000 au 30,000 hakuna tija kwa watumishi bali kupunguza kodi kunamsaidia zaidi mfanyakazi.

Kwa sasa kodi ya mshahara (PAYE) ni imeanzia digiti moja yaani asilimia 9 kutoka digiti mbili za awali, huku ikitofautiana kwa kiwango cha mishahara jambo ambalo limetoa ahueni kubwa kwa wafanyakazi, huku kilio cha nyongeza ya mishahara kikiwa pale pale.

Mfumuko wa bei umedhibitiwa kwa kiasi kikubwa, lakini gharama za maisha zimepanda hasa kwenye makazi na huduma nyinginezo ambazo mfanyakazi atahitaji kugharamia.

Mara nyingi utaratibu wa kupandisha mishahara uko zaidi serikalini, huku sekta binafsi, ikiwa ni kwa mujibu wa taratibu za kampuni husika, ambazo mara nyingi hutegemea na hali ya uchumi na ukuaji wa mzunguko wa fedha pamoja na ushindani.

Kilio cha Rais wa TUCTA ni cha watumishi wote wa umma ambao kwa muda mrefu wamesubiri kusikia nyongeza ambayo italeta mabadiliko kwa mtu mmoja mmoja kwa sasa na hata baada ya kumaliza muda wa utumishi wake.

Ni muhimu serikali ikatilia maanani kilio hiki na kufikiria uwezekano wa kuongeza mshahara, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yao kwa watumishi.

Hali hiyo ina manufaa mengi zaidi kwa kuwa kama hakuna nyongeza kwa miaka mitano na sasa ikiongezeka maana yake itaongeza morali ya kazi.

Tunatarajia hata sekta binafsi italitazama suala hili kwa mtazamo chanja ili kuongeza morali ya kazi kwa wafanyakazi wake.

Matarajio ya wafanyakazi ni makubwa kwamba baada ya kilio cha muda mrefu, sasa faraja inakuja kwa kutangaziwa nyongeza ya mishahara au kuoungua kwa kodi ambayo nayo itatoa ahueni kubwa kwao.

Habari Kubwa