Kipaumbele kielekezwe kwenye kilimo cha ufuta

21Sep 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kipaumbele kielekezwe kwenye kilimo cha ufuta

ZAO la ufuta linalimwa kwa wingi katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani, Morogoro, Dodoma, Tanga na ukanda wa chini katika mikoa ya Rukwa na Mbeya kwa ajili ya chakula na biashara.

Kuna kampuni mbalimbali ambazo hununua ufuta kwa ajili ya soko la ndani na nyingine husafirisha zao hilo kwenda kuuza nje ya nchi, hali inayoonyesha kuwa kilimo cha ufuta kinalipa.

Mfano mzuri ni wa wakulima wa zao hilo Lindi ambao wamepata Sh. bilioni 120.6 baada ya kuuza kilo 49,885,228 za zao hilo kupitia mfumo wa stakabadhi gharani katika msimu wa mwaka huu.

Takwimu hizo ni za Mshauri wa Kilimo na Rasilimali Watu, Majid Myao, wakati akiwasilisha taarifa ya mauzo ya zao hilo katika mkutano uliowakutanisha wadau wa zao hilo.

Kwamba, Mkoa wa Lindi uliweka malengo ya kuzalisha kilo 68,500,000 za ufuta, lakini kutokana na hali ya hewa kutokuwa mzuri na idadi ya ukubwa wa mashamba wamekusanya kilo 49,885,228 sawa na asilimia 72.8, hivyo kushindwa kufikia lengo lililokusudiwa.

Hatua ya wakulima kupata kiasi hicho cha fedha katika mazingira hayo, ni wazi kwamba ipo haja kwa serikali kuweka mkazi kwenye kilimo cha ufuta, ili wakulima waweze kunufaika huku serikali nayo ikipata kodi.

Mbali na serikali kuliwekea mkazo zao hilo kwa kuhamasisha wakulima kujikita katka kulizalisha, pia serikali hainabudi kuweka mazingira mazuri na wezeshi kama kichocheo na hamasa.

Tunaamini kwamba kwa kilimo cha ufuta, wakulima wanaweza kuwa na maisha mazuri kwa kujenga nyumba bora, kusomesha watoto wao na hata kujiwekea akiba ya kutosha.

Kwa muda mrefu tumekuwa tukishuhudia wakulima hasa wa mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara wakiweka nguvu zao zaidi kwenye kilimo cha zao la korosho ambalo wakati mwingine soko lake halina uhakika kutokana na wakati mwingine huporomoka.

Hivyo, kwa jinsi ambavyo ufuta umeanza kunufaisha wakulima, tunaona kuna haja wakahamasishwa kuongeza kasi katika kilimo cha ufuta ambacho nacho kimeanza kuonyesha wazi kuwa kinaweza kuwanufaisha.

Hatusemi kwamba, waache korosho, bali kasi inayotumika katika kilimo cha zao, iwe ni hiyo pia kwenye ufuta, ili kuboresha zaidi maisha yao, kutokana na kwamba nalo lina soko kama yalivyo mazao mengine na chakula na biashara.

Tunatambua kutegemea zao moja kwa ajili ya biashara, ni vigumu mkulima kufikia hatua nzuri ya maendeleo, bali kulima mazao mengi inaweza kuwa njia rahisi na mbadala kujiongezea kipato kupitia kilimo.

Wakati tunashauri serikali kuweka mkazo kwenye kilimo cha ufuta, si vibaya wakulima wenyewe nao wakajiongeza kwa kutambua umuhimu wa zao hilo na kuamua kuelekeza nguvu zao hilo.

Ufuta hutoa mafuta yanayotumika katika mapishi mbalimbali ili kuongeza ladha na pia huleta nguvu na joto mwilini, na mbegu zake huchanganywa na vyakula kama mikate, keki, mboga na kadhalika.

Jambo lingine linalothibitisha umuhimu wa zao la ufuta, ni jitihada za sasa za serikali kuhimiza uzalishaji wa mazao mbadala kwa lengo la kukabiliana na uhaba wa mafuta ya kupikia, hali inayosababisha bei kupanda kila uchao.

Kwa mtazamo wetu ni kwamba, wakulima wakihamasishwa na kutambua thamani ya zao hilo, wanaweza kuongeza kasi ya kilimo chake na kuwa na mashamba mengi, ambayo uzalishaji wake utakuwa mkubwa kisha kuwainua na taifa kwa ujumla kiuchumi.