Kiswahili sasa kiwe uwekezaji wetu nje

12May 2017
Mhariri
Nipashe
Kiswahili sasa kiwe uwekezaji wetu nje

MARA nyingi Watanzania tumekuwa tukijivunia sana kuwa na lugha ya Kiswahili ambayo ndiyo iliyosaidia katika kutuunganisha na kuwa na taifa moja.

Kutokana na lugha ya Kiswahili kuwaunganisha Watanzania zaidi ya makabila 120, hali hiyo ilichangia Tanzania ipate uhuru wake mapema.

Lugha ya Kiswahili imekuwa ikipewa umuhimu mkubwa ikiwamo kuwa lugha rasmi ya taifa, lakini pia kuwapo taasisi kadhaa za kuipanua na kuiendeleza.

Aidha, kumekuwapo na mpango wa kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu, ingawa utekelezaji haujaanza.

Kutokana na Kiswahili kueleweka na kuzungumzwa na watu wengi nchini, tena kwa ufasaha kabisa, Tanzania imekuwa ikichukuliwa kuwa ndiyo chimbuko la lugha hiyo.

Vile vile, raia wengi wa kigeni waliopata fursa ya kuishi Tanzania hususani waliokuja kusoma kwenye vyuo kadhaa na wapigania uhuru kutoka nchi za kusini mwa Afrika walibahatika kufahamu Kiswahili.

Pamoja na tunu hiyo ya Kiswahili ambacho kwa sasa kinazungumzwa katika nchi nyingi za Bara la Afrika, nchi yetu haikuitumia ipasavyo fursa hiyo kama mtaji wa kuwekeza nje; kwa maana ya kupeleka wataalamu wa kukifundisha.

Udhaifu huo ulitumiwa na nchi nyingine ambazo hazikuwa na historia wala weledi wa lugha hiyo kwa kuchangamkia fursa za kupeleka watu wao wakijiita wataalamu wa kufundisha Kiswahili.

Ni kosa ambalo tulilifanya kama taifa, lakini tunapaswa kujifunza kutokana na makosa hayo na kujisahihisha sasa kwa kuchukua hatua bila kuchelewa.
Jitihada zilizofanywa na serikali ya awamu ya tano za kukubaliana na Afrika Kusini kupeleka wataalamu wa Kiswahili nchini humo zinadhihirisha kusahihisha makosa hayo.

Rais John Magufuli alisema jana kuwa wakati wowote kuanzia sasa Tanzania itapeleka walimu wa Kiswahili Afrika Kusini kwa ajili ya kufundisha somo hilo kwenye shule na vyuo vikuu nchini humo.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo Ikulu, jijini Dar es Salaam, baada ya kukutana na Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma na kusaini mikataba ya ushirikiano katika sekta mbalimbali.

Rais alisema amewakaribisha waje kuchukua walimu wa Kiswahili na kwamba watapelekwa wakati wowote na kwamba Rais Zuma amemhakikishia kuwa nchi yake iko tayari katika hilo.

Habari kuhusu nafasi za ajira kwa wataalamu wetu wa Kiswahili Afrika Kusini zitawafurahisha Watanzania wengi kwa kuzingatia kuwa wamekuwa wakijivunia tunu hiyo bila kuona manufaa yake kwao na kwa taifa kwa ujumla.

Sisi tunaiona fursa ya Afrika Kusini kuwa ni mwanzo kwa kuwa kuna nchi nyingi Afrika na nje ya bara hili ambako Kiswahili kinahitaji wataalamu.

Nchi kama Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ni maeneo ambayo yanahitaji wataalamu wa Kiswahili kwa upande wa Afrika na nchi zingine kama China ambayo raia wake wengi wanakuja kwa wingi nchini kwa ajili ya uwekezaji.

Baada ya kutambua umuhimu wa fursa ya lugha ya Kiswahili, tunaamini kuwa serikali itaichangamkia zaidi kupitia makubaliano mbalimbali ambayo inaingia na nchi nyingine.

Pia mabalozi wetu wanaotuwakilisha nje ya nchi watapaswa kupewa suala hilo kuwa sehemu ya majukumu ya kutekeleza katika shughuli zao za kila siku zikiwamo za kutangaza fursa zilizoko nchini.

Hakika, kwa kufanya hivyo, hapatakuwapo tena malalamiko kuwa nchi zingine zinapeleka watu wao nje kufundisha Kiswahili bila kuwa na ujuzi wala weledi.

Kimsingi tukubaliane kuwa Kiswahili sasa kiwe uwekezaji wetu nje. Wakati wenzetu wanakuja kuwekeza nchini, sisi twende kuwekeza lugha hiyo kwao.