Kitendo cha Ukawa kumkubali Naibu Spika ni cha kupongezwa

11Sep 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kitendo cha Ukawa kumkubali Naibu Spika ni cha kupongezwa

WABUNGE wa kambi ya upinzani chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hatimaye wamebadili uamuzi wao wa kususia vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.

Uamuzi wa wabunge hao ulitolewa wakati wa mkutano wa nne wa Bunge (Bunge la Bajeti) lililomalizika Juni, mwaka huu. Ukawa walitangaza mgomo huo kwa kile walichodai kupinga kitendo cha Dk. Tulia cha kuipendelea serikali na kuinyima kambi hiyo kutoa maoni yao.

Katika kufanya hivyo, wabunge hao kila Naibu Spika alipokuwa akiingia kuongoza vikao vya Bunge, walikuwa wakitoka na zaidi ya hayo kuna wakati walifunga bandeji midomoni na hata kususa kuwasalimia wabunge wenzao wa CCM.

Kwa ujumla, hatua hiyo ilitoa doa chombo hicho ambacho ni mhimili wa dola wenye jukumu la kutunga sheria, kupitisha bajeti ya serikali na kuishauri na kuisimamia serikali juu ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya nchi. Kugoma kwao kushiriki vikao vya Bunge, pia kulisababisha hata bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 na miswada mbalimbali kupita bila kupata upinzani kutoka kambi hiyo.

Kurejea kwa wabunge hao, yamkini, ni matunda ya juhudi za Spika wa Bunge, Job Ndugai, ambaye muda mfupi baada ya kurejea kutoka kwenye matibabu nchini India, aliahidi kumaliza tofauti hizo na kuwasihi kambi ya upinzani kurejea bungeni kuendelea na majukumu yao kwa mujibu wa sharia, kanuni na taratibu zinazoongoza chombo hicho.

Hatua hiyo ilijidhihirisha juzi, baada ya wabunge wa upinzani kuhudhuria kikao cha bunge kilichoongozwa na Dk. Tulia huku wakitoa maoni ya kambi yao juu ya miswada iliyowasilishwa siku hiyo.

Hali hiyo ilikuwa tofauti na wakati wa mkutano wa Bunge la Bajeti, kwani wapinzani walikuwa wakiwasilisha mezani taarifa zao na kutaka ziingie kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge na hatimaye kuondoka.

Hatua ya wabunge hao wa Ukawa kurejea bungeni na kuhudhuria vikao vilivyo chini ya Dk. Tulia ni ya kupongezwa kwani ni ishara kwamba nongwa zilizokuwa zimetawala wakati wa mkutano uliopita, zimemalizika na wote, bila kujali tofauti zao, wamerejea kwenye majukumu yao.

Tunapongeza kitendo hicho kwa sababu kama wahenga wasemavyo wapiganapo tembo nyasi ndizo ziumiazo, vivyo hivyo tofauti baina ya naibu Spika na Ukawa ziliwaathiri zaidi wananchi ambao waliwachagua wabunge kuwawakilisha katika chombo hicho cha kutunga sheria.

Hatua ya kutunishiana misuli baina ya pande hizo ilikuwa na athari kubwa kwa wananchi kwani walikosa uwakilishi wa kweli.

Ni ukweli usiopingika kwamba mijadala wakati wa Bunge la Bajeti ilipoa kutokana na kuwa ya upande mmoja. Hata kashkashi zilizozoeleka ndani ya chombo hicho kutokana na baadhi ya mawaziri kubanwa juu ya masuala mbalimbali, hazikiwapo.

Kwa mantiki hiyo, kurejea kwa wabunge hao, ni imani ya wananchi kwamba mijadala motomoto ambayo hushuhudiwa au kusikika, sasa itaendelea na wadau wanaamini kuwa bunge hilo litakuwa na uhai katika kujadili mambo ya msingi na yenye maslahi kwa taifa.

Pamoja na bunge kurejea katika hali yake, ni vyema wawakilishi hao wa wananchi wakajua kwamba panapokuwa na tofauti, tena zinazowahusu viongozi waliopewa dhamana ya kutunga sheria, njia pekee ya kuzimaliza ni maridhiano na si kuvutana kama ilivyokuwa.

Katika kurejesha uhai huo wa Bunge, pongezi pekee zinapaswa kumwendea Spika Ndugai kwani alichoahidi kimeonekana kuzaa matunda. Maridhiano hayo yanapaswa kuendelea kwa manufaa ya Watanzania.

Jambo jingine ambalo wabunge na wanasiasa wanapaswa kulitambua ni kwamba moja ya misingi ya demokrasia katika jamii yoyote ile ni kuvumiliana, hivyo panapotokea tofauti kama zilizojitokeza wakati wa Bunge la Bajeti zilipaswa kuchukuliwa katika mwelekeo huo.

Kutokana na hatua iliyofikiwa baina ya pande zilizohusika na vuta nikuvute ndani ya Bunge, ni hakika kwamba mambo yatakwenda vizuri na Watanzania wanatarajia kuwapo kwa matokeo chanya katika mkutano wa sasa unaoendelea mjini Dodoma.

Habari Kubwa