Klabu ligi kuu zisikurupuke kutimua makocha

30Dec 2017
Mhariri
Nipashe
Klabu ligi kuu zisikurupuke kutimua makocha

MIKIKIMIKIKI ya ligi kuu Tanzania Bara imerejea tena ambapo jana ilianza raundi ya 12 baada ya kusimama kwa muda wa wiki tatu kupisha michuano ya kombe la Chalenji.

Raundi ya 12 imeanza huku vinara wa ligi hiyo, Simba wakiwa bila kocha wao mkuu, Joseph Omog ambaye litimuliwa na mabosi wa timu hiyo kufuatia kuondolewa kwenye michuano ya kombe la FA raundi ya pili.

Simba imeumia na vitu viwili ambavyo bila shaka vimefanya mabosi wao kutopepesa macho na kuamua kumtupia virago kocha wao huyo.

Cha kwanza Simba sasa inafahamu fika wamebakia na tiketi moja tu ya kushinda taji la ligi kuu hili kupata nafasi ya kushiriki tena michuano ya kimataifa ya CAF, lakini pia Simba wameumia kutolewa kwenye raundi ya pili huku wakiwa mabingwa watetezi, na mbaya zaidi wameondolewa na timu isiyofahamika inayocheza ligi daraja la pili Green Warriors.

Nipashe tunafahamu katika soka mabadiliko ya benchi la ufundi ni jambo la kawaidia hasa pale timu inapofanya vibaya sana.

Lakini kwa hili la Simba, vilabu vingine ni lazima vijitathmini kabla ya kufanya maamuzi kama waliyoyafanya Simba.

Kimsingi, Nipashe tunaona kama Simba walichukua maamuzi ya haraka sana, hasa ukizingatia timu bado inafanya vizuri kwenye ligi, inaongoza kileleni (kabla ya mchezo wa jana wa Azam FC dhidi ya Stand United).

Ni ngumu kuelewa, kocha ambaye timu yake ipo kileleni kwenye ligi huku mzunguko wa kwanza ukiwa unakaribia kumalizika anatimuliwa.

 

Inawezekana, Simba walikuwa na sababu zao za msingi zaidi, lakini Nipashe tunazishauri timu zetu za ligi kuu kuangalia mara mbili maamuzi ya kutimua kocha katikati ya msimu tena timu ikiwa kwenye nafasi nzuri kwenye ligi.

 

Kutimua kocha aliyekaa na timu muda mrefu kuna mambo mawili yanaweza yakatokea, kwanza kocha mpya atakayechukua mikoba yake anaweza akaifanya timu ikasogea kutoka ilipo ikaenda mbele zaidi, lakini pia anaweza akaididimiza zaidi timu kwa kuwa naye atahitaji muda wachezaji wake wazoee mbinu na mifumo yake.

 

Tunashauri, viongozi kuwa makini katika mabadiliko ya makocha wao ili kuepuka kubolonga zaidi kwenye ligi na michuano mingine ambayo timu inashiriki.

 

Kwa sasa Simba inatakiwa kuwa makini na kujipanga katika kutafuta kocha mpya kwa kuwa timu inakabiliwa na michuano ya kimataifa ambayo wataanza kushiriki Februari mwakani.

 

Simba kama itaamua kutafuta kocha mpya inapaswa kutafuta kocha ambaye atakuwa na uwezow a juu ya Omog na atakayetumia muda mfupi kuwafanya wachezaji wamuelewe na kushika mbinu zake.

 

Michuano ya kimataifa si ya kuijaribu, kama Simba hawatakuwa wametulia na kujipanga wanaweza wakaishia hatua za awali kwenye kombe la Shirikisho Afrika.

 

Na hili hata kwa wawakilishi wetu wengine kwenye michuano ya CAF, Yanga ambao watatuwakilisha katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, nao wanapaswa kujipanga.

 

Yanga inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu, bado wanaendelea na kocha wao, George Lwandamina, lakini bado wanatakiwa kujipanga imara kama wanataka kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.

 

 

 

 

Habari Kubwa