Klabu, wachezaji Bara wasisahau lala salama

21Mar 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Klabu, wachezaji Bara wasisahau lala salama

AFYA ya wachezaji na maofisa mbalimbali wanaosimamia michezo ni moja ya mambo muhimu katika maendeleo ya michezo husika sehemu yoyote hapa duniani.

Kufuatia kuwapo kwa janga la maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona (COVID 19), Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupitia Bodi ya Ligi Kuu nalo lilitangaza kusimamisha ligi zake zote mpaka pale hali ya maambukizi ya ugonjwa huo yatakapodhibitika au kumalizika.

Moja ya ligi iliyosimamishwa na TFF ni Ligi Kuu ambayo ndiyo ligi ya juu hapa nchini na ndio hutoa mwakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ligi hiyo pia ndiyo inayotoa idadi kubwa ya wachezaji wengi katika kikosi cha Timu ya Taifa (Taifa Stars), ambayo inakabiliwa na mechi za mashindano mbalimbali, ikiwamo fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), ambazo nazo zimesimamishwa hapo hapo itakapotangazwa tena.

Tamko hilo la kusimamisha ligi ambalo lilifuata mwongozo uliotolewa na serikali wa kusimamisha mikusanyiko, limetoka katika hatua ya lala salama.

Ili kurejea wakiwa imara, ni vema timu zikahakikisha zinawaandalia programu maalumu wachezaji wao kwa sababu ya kuendeleza ushindani katika mechi zilizosalia pale ligi hizo zitakapoanza tena.

Wachezaji wanatakiwa kuendelea na mazoezi binafsi kwa timu ambazo zimevunja kambi, huku wale ambao wanaendelea na mazoezi ya pamoja, kuhakikisha wanajifua ili waweze kutimiza malengo yao ya kufanya vizuri msimu huu.

Kwa kuangalia msimamo wa Ligi Kuu Bara, bado nafasi kwenye mbio za kuwania ubingwa iko wazi kutokana na timu tano zilizopo juu zinaweza kulitwaa kombe hilo endapo, vinara na mabingwa watetezi Simba watapoteza michezo yao.

Klabu zinatakiwa kutumia muda huu kurekebisha upungufu waliyoubaini katika mechi zilizopita na mara watakapoanza kucheza tena, vikosi vyao kushuka dimbani wakiwa na nguvu na wanaoonyesha ushindani kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho ya mchezo husika.

Hakuna kisichowezekana na ni makosa kwa timu kukata tamaa. Timu isiyotarajiwa inaweza kutwaa ubingwa na vile vile timu isiyotarajiwa inaweza kuteremka daraja kama itazembea katika michezo yake iliyobakia kama ambavyo tunashuhudia klabu ya KMC FC ya jijini Dar es Salaam ilivyozinduka na kuanza kuvuna pointi.

Nipashe inawakumbusha wachezaji na waamuzi kuwa makini katika muda uliobakia ambao ni muhimu kwao kujiweka sokoni kuelekea maandalizi ya msimu mpya kwa kuonyesha ubora wa hali ya juu.

Tunahitaji kuona msimu ujao wachezaji wanaocheza soka la kulipwa wanaongezeka pamoja na waamuzi watakapopata beji za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), wanakwenda kupeperusha vema bendera ya Tanzania katika mechi zote watakazopangiwa.

Haipendezi kuona kila msimu idadi ya waamuzi wanaochezesha Ligi Kuu Bara au mashindano ya Kombe la FA wanafungiwa kwa sababu ya kushindwa kumudu michezo au wachezaji wanakosa namba katika vikosi vya kwanza kufuatia kushuka viwango vyao.

Kama wachezaji watautumia vema muda wa siku 30 ambao hawatacheza mechi za mashindano, watarejea na nguvu mpya na hatimaye mwisho wa msimu timu bora itatwaa ubingwa wa Bara sambamba na timu zitakazopanda daraja.

Ni wazi mchezaji atakayeonyesha kiwango bora katika mechi zilizosalia atakuwa na nafasi nzuri ya kusajiliwa na klabu nyingine kwa dau nono au kuboreshewa maslahi yake katika timu aliyopo.

Habari Kubwa