Klabu, wachezaji waheshimu mikataba kuepusha mvutano

08Aug 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Klabu, wachezaji waheshimu mikataba kuepusha mvutano

KLABU za Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza na la Pili, tayari zipo mawindoni kwa ajili ya kuimarisha vikosi vyao kuelekea msimu mpya unaotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao.

Ligi Kuu ndiyo itakayokuwa ya kwanza kuanza kutimua vumbi katika viwanja 18 nchini hapo Septemba 6, mwaka huu kabla ya ligi hizo nyingine kuanza, na tayari klabu zimeshaanza kusajili baada ya dirisha kufunguliwa tangu Agosti Mosi mwaka huu, huku likitarajiwa kufungwa mwishoni mwa mwezi huu.

Tunatoa pongezi kwa klabu ambazo tayari zimetangaza mapema wachezaji isiyowahitaji kuelekea msimu mpya, hivyo kuwapa nafasi ya kutafuta timu nyingine kabla ya dirisha hilo kufungwa, hivyo zile ambazo hazijafanya hivyo, tunasisitiza kuzingatia hilo mapema.

Hata hivyo, kanuni na umakini zaidi kwa klabu na hata wachezaji unahitajika hususan kwa kulinda mikataba yao kwa wale ambao wameshaingia ama wanatarajiwa kuingi ili kuepusha migogoro kati ya pande husika.

Tunatoa tahadhari hiyo hasa kwa kutambua kwamba ni nadra sana kwa dirisha la usajili Tanzania Bara kumalizika bila kusikia mvutano kwa klabu na klabu ama klabu, mchezaji na klabu nyingine kuvutana kuhusu kusajili mchezaji wao kinyume cha taratibu.

Hivyo, hatutaki kusikia ama kuona mchezaji akilazimika kufungiwa ama kupotezewa muda wake wa kushuka dimbani kutokana na ukiukwaji huo wa kanuni ambao unaweza kuepukika.

Miaka iliyopita tulishuhudia mivutano kama hiyo kwa mchezaji kama Athumani Iddi 'Chuji' katika usajili wake wa kutoka Simba kwenda Yanga, lakini Ramadhani Singano kutoka Simba kwenda Azam FC.

Hao ni baadhi tu ya wachezaji ambao sakata lao la usajili lilifikia hatua hadi wachezaji kudai mikataba na saini zao zimeghushiwa hatua iliyosababisha kufikishana katika vyombo vya dola.

Kadhalika, tulishuhudia pia mchezaji wa Mbao FC, Pius Buswita, akijisajili klabu mbili tofauti jambo ambalo Shirikisho la Soka nchini (TFF), lilichukua hatua ya kumfungia kucheza soka kwa kipindi cha mwaka mmoja kutokana na kosa hilo, adhabu ambayo hatutaki kuona ikitokea tena kwani inadumaza kiwango cha mchezaji husika na kumpotezea mipango yake kisoka.

Hata hivyo, tunasikitishwa na mvutano ambao unaendelea kati ya Yanga na kiungo mshambuliaji wao raia wa Ghana, Bernard Morrison ambaye amedai saini yake imeghushiwa katika mkataba mpya ambao anadaiwa kuingia na klabu hiyo baada ya ule wa miezi sita kumalizika.

Hayo yote yakihusishwa na tetesi za Simba kumtaka mchezaji huyo, kimsingi Nipashe hatuegemei upande wowote, kwani tunahitaji kuona suala hilo likimalizwa kwa kufuata kanuni na pande zote zikiridhika kwa uamuzi utakaochukuliwa bila kuonewa.

Misimu iliyopita tulifurahishwa na namna kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima, na mshambuliaji mzawa, Ibrahim Ajibu baada ya kumaliza mikataba yao kwenye timu zao wakiruhusiwa kuondoka bila mvutano, awali Ajibu akitoka Simba kwenda Yanga kabla ya kurejea tena huku Niyonzima naye akitoka Yanga na kutua Simba kabla ya kutoka na kurejea tena, hicho ndicho tunachotaka kukiona na si hili la Morrison kwa sasa.

Kimsingi katika kipindi kama hiki cha dirisha la usajili, ndicho cha mavuno kwa wachezaji kwa kujiingizia mamilioni ya fedha pale wanaposaini mikataba mipya kwenye timu zao au wanazohamia, hivyo klabu zisiwaharibie kwa sababu soka ni maisha yao na wachezaji nao wanapaswa huheshimu mikataba yao.

Habari Kubwa