Klabu zakumbushwa Fair Play lala salama Ligi Kuu

23May 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Klabu zakumbushwa Fair Play lala salama Ligi Kuu

RAIS John Pombe Magufuli juzi alitangaza rasmi kufungua michezo yote hapa nchini kuanzia Juni Mosi, mwaka huu.

Kauli hiyo inaashiria kurejea kwa michezo yote iliyokuwa imesimama tangu Machi 17, mwaka huu ili kupisha maambukizo ya virusi vya ugonjwa wa corona (COVID 19).

Hata hivyo, inaonekana kama Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ni maarufu nchini ndio pekee ilisimama, lakini ukweli zilisimama pia ligi nyingine ikiwamo Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili, Ligi ya Wanawake na mashindano ya Kombe la FA.

Ligi Kuu ndiyo inayotoa wawakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Kombe la FA hutoa mwakilishi wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Pia Ligi Kuu Zanzibar ambayo hutoa wawakilishi wa mashindano hao ya kimataifa yanayoandaliwa na kusimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na ligi nyingine ndogo zinazochezwa visiwani humo, pia zilisimamishwa kwa sababu ya kujikinga na ugonjwa huo ambao umeua maelfu ya watu duniani.

Kurejea kwa ligi hizo sasa kunatoa taswira kuwa bingwa atakayepatikana au atakayetangazwa atakuwa ni yule aliyefanya vizuri zaidi uwanjani na si mezani kama baadhi ya mataifa yalivyoamua kumaliza msimu wa 2019/20.

Kauli ya JPM ni dhahiri sasa inategua kitendawili cha timu zipi zinastahili kwenda kupeperusha bendera ya Tanzania katika mashindano ya kimataifa kwa mujibu wa kanuni zilizopitishwa na kukubaliwa na klabu zote.

Lakini mbali na viongozi walivyokuwa wanaumiza kichwa kuhusiana na wawakilishi hao watakavyopatikana endapo ligi hizo hazitarejea na kumalizika kama zilivyotarajiwa, pia kulikuwa na hoja mbalimbali kuhusiana na timu zitakazoshuka daraja.

Wadau wengi walionekana kutoa ushauri katika kuteua wawakilishi wa nchi watakaokwenda kushiriki kwenye mashindano yanayoandaliwa na CAF, lakini wakitaka kuzionea huruma zile zinazotakiwa kushuka daraja kwa kueleza, timu zote ziendelee.

Hata hivyo wadau hao hao wanasahau pia katika ligi za madaraja ya chini, kuna klabu ambazo zinatakiwa kupanda daraja ikiwamo Gwambina FC ya jijini Mwanza, hata ikifungwa kwenye mchezo wake wa mwisho, haitaathiri nafasi yake ya kuwania kupanda daraja, kwa sababu tayari ilikuwa imeshamaliza kampeni yake.

Nipashe inapenda kulipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na vyama vingine mbalimbali vya michezo kwa kuwa watulivu na kutochukua uamuzi wowote wa haraka katika kumaliza msimu huu na badala yake vilikuwa vikifanya kazi karibu na serikali kufahamu tathmini ya Covid 19 ilivyofikia.

Tunapenda kuwakumbusha mashabiki wote kuendelea kufuata maelekezo yatakayotolewa na wataalamu wa afya wakati ligi na michezo hiyo itakaporejea ili kudhibiti maambukizo ya ugonjwa huo uliotikisa dunia.

Ikumbukwe mbali na michezo kusaidia kuimarisha afya zetu, hutoa ajira kwa mamia ya wachezaji pamoja na wadau wengine ambao shughuli zao hutegemea mechi na mashindano mbalimbali.

Tunawakumbusha ili bingwa apatikane kwa haki pamoja na timu zitakazoshuka daraja, haki inatakiwa kutawala na kuonekana kwa vitendo kwenye mechi zote zilizobakia.

Usimamizi huo ufanyike katika mechi zote na si uangalizi wa kiwango cha juu na usionekana pale vigogo, Simba na Yanga watapokuwa uwanjani. Haki sawa kwa timu zote za Ligi Kuu Bara.

Watanzania tunatakiwa kuendelea kuwa wasikivu kama Rais Magufuli alivyotamka kwa kuhakikisha michezo inarejea na afya za wananchi wote zinaendelea kuimarika wakati wote.

Habari Kubwa