Klabu zikidhamiria zitatufikisha pepo ya soka tunayoitamani

06Mar 2017
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Klabu zikidhamiria zitatufikisha pepo ya soka tunayoitamani

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara wa 2016/2017 unaelekea ukingoni ambapo timu shiriki zimebakiza mechi si zaidi ya saba kumaliza michezo yao yote.

Katika michezo ya mwisho mwa wiki iliyopita kuna mambo mengi yamejionyesha ambayo yanatoa taswira kuwa klabu zetu zenyewe ndizo zenye maamuzi ya kuifanya ligi yetu kuwa ya namna gani.

Ni wazi klabu kama zinakuwa na maandalizi ya kutosha na wachezaji wakatimiziwa mahitaji yao basi inaweza kuwa yenye upinzani mkubwa kuondoa daraja la timu vibonde.

Jumamosi ya juzi tumeshuhudia mchezo wa kusisimua wa Ligi Kuu baina ya Simba waliokuwa wenyeji wa Mbeya City ya jijini Mbeya.

Katika mchezo huo, Mbeya City walionyesha kweli ni timu iliyojipanga na wachezaji wakijitolea lolote linawezekana ndani ya dakika 90 za mchezo.

Mbeya City ilicheza soka safi na kufanikiwa kuwabana kwa muda mrefu Simba waliokuwa wamepewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo.

Nipashe inaamini kama klabu hiyo na nyingine zingekuwa na morali wa aina hiyo katika mechi zote, ni wazi mpaka sasa tusingejua timu gani inaelekea kutwaa ubingwa na zipi zinaelekea kushuka daraja kama ilivyo sasa.

Mpaka kufikia leo Jumatatu, tayari mashabiki na wadau wa soka hapa nchini wameshaona mwelekea wa ubingwa msimu huu ambapo mbio hizo zimebaki kwa ‘wababe’ wawili, Simba na Yanga.

Ni vyema klabu nyingine zichukulie kila mchezo ni mgumu na muhimu kwao, ziachane na kukamia timu kubwa huku zikilegeza kamba zinapokutana na timu nyingine zaidi ya Simba na Yanga.

Nipashe inaipongeza Mbeya City kwa soka safi walilolionyesha juzi, lakini pia ni vyema juhudi walioionyesha kwenye mchezo huo ikaendelea kwenye mechi nyingine zilizobaka kabla ya ligi kumalizika.

Tatizo linalozisumbua klabu zetu, ni kuona kuzifunga klabu za Simba na Yanga ni sawa na kuchukua ubingwa, jambo hilo ndilo linaloziponza timu na kujikuta zinazidiwa katika mbio za ubingwa na timu hizo ikiwa ni pamoja na Azam.

Msimu huu unaelekea ukingoni, klabu zijitathmini mara baada ya ligi kumalizika na kuanza mipango kwa ajili ya msimu ujao, lakini pia zifahamu ligi si kuzifunga Simba na Yanga peke yake. Ili timu ifanye vizuri ni vyema na ni lazima iweke mikakati ya kuibuka na ushindi katika kila mchezo.

Sisi tunalichukulia soka Mbeya City ililoonyesha katika mechi dhidi ya Simba kama mfano, ikiwakilisha klabu nyingine zilizofanya hivyo kwenye michezo yao.

Mashabiki na wadau wa soka wanataka kuona Ligi yetu inakuwa yenye msisimko na ushindani mkubwa na kulifanya jambo hili kutimia, kazi hiyo haipaswi kufanywa na Shirikisho la soka Tanzania (TFF) peke yake, bali hata klabu zina nafasi kubwa ya kuifanya ligi yetu kuwa yenye ushindani na mvuto wa hali ya juu.

Tunaamini kama klabu zitaacha kuzikamia klabu za Simba na Yanga peke yake, na kuchukulia kwa uzito sawa mechi zote kwenye Ligi Kuu, basi siku si nyingi tutafika pepo ya soka tunayoitamani kila uchao.

Habari Kubwa