Klabu zitangulize maslahi ya wachezaji dirisha hili

01Aug 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Klabu zitangulize maslahi ya wachezaji dirisha hili

RASMI dirisha kubwa la usajili kwa klabu za Tanzania Bara kuelekea msimu ujao limefunguliwa leo Agosti Mosi na litadumu hadi mwishoni mwa mwezi huu, kabla ya msimu mpya kuanza katikati ya mwezi ujao.

Kufunguliwa kwa dirisha hilo ni nafasi pekee kwa klabu hususan za Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na la Pili kuboresha vikosi vyao ama kuvisuka upya kabla ya msimu mpya kuanza.

Tayari baadhi ya klabu zimeshaanza kuhusishwa na wachezaji kadhaa kutoka ndani na nje huku wengine wakifunguliwa milango ya kutokea kwa klabu zao kutangaza hazitahitaji huduma zao msimu ujao.

Hata hivyo, tunatambua katika dirisha hili kama yalivyo mengine, wapo wachezaji wataachwa kutokana na mikataba yao kumalizika ama watatemwa kwa sababu ya viwango vyao kushuka, ili kutoa nafasi kwa nyota wapya ambao klabu husika zinaamini wanaweza kuzisaidia kutimiza malengo yao ya msimu ujao.

Lakini kutemwa kwao hakuwezi kuwa safari ya mwisho kwao kisoka kwani upo msemo wa wahenga usemao "ukisema wa nini, mwenzako anajiuliza atampata lini" na unaweza kuonekana hufai hapa ila kwingineko ukawa lulu.

Katika hilo, tunaushahidi wa kutosha kwa baadhi ya wachezaji ambao wamewahi kuonekana hawafai na kutemwa, lakini baada ya kwenda kwingineko wakang'ara na baadaye kusajiwa tena na klabu zilizowatema awali, hivyo kutufanya kuendelea kuamini "kumpiga chura teke ni kumuongezea mwendo".

Kwa mantiki hiyo, wachezaji watakaotemwa hawana budi kutambua hayo ndiyo maisha ya soka na kinachotakiwa ni kupambana zaidi kwa klabu mpya zitakaowasajili ili kuthibitisha ubora wao.

Aidha, tunafahamu wazi zipo klabu ambazo zimetega mitego yao zikisubiri wachezaji watakaotemwa hususan kutoka kwa klabu kubwa ili ziwasajili jambo ambalo Nipashe tungependa kuona klabu zote zikitangulia kwanza kutangaza wachezaji zinaowatema kabla ya kuanza kusajili wapya ili kuwapa fursa ya kujiweka sokoni mapema.

Hatutarajii kuona wachezaji wakutemwa katika dirisha hili wakiwa wa mwisho kutangazwa baada ya klabu husika kufanya usajili kwa kuwa kufanya hivyo ni kutowatendea haki.

Lakini pia kufunguliwa kwa dirisha hili kubwa ni wakati muafaka kwa wachezaji ambao walikuwa hawapati nafasi katika vikosi vya kwanza kuomba kuondoka ili kuokoa viwango vyao na vipaji kwa ujumla.

Tunatambua wapo wachezaji ambao walishawishika kusajiliwa na baadhi ya klabu kutokana tu na kuahidiwa dau kubwa ama kufuata mapenzi yao kwa klabu, na baadaye kujikuta wakisugua benchi katika kila mechi ama kuishia kupata nafasi chache dimbani wakitokea benchi.

Hivyo, wachezaji kama hawa, hawana budi kuomba kuondoka ama kutolewa kwa mkopo badala ya kuendelea kusugua benchi ama kusubiri kucheza wakitokea benchi katika kila mechi jambo ambalo linashusha viwango vyao.

Hivyo, hatutarajii kuona kunakuwa na klabu zitakazowabania wachezaji ambao hawapati nafasi wakitaka kuondoka ama kuwatoa kwa mkopo kama wanamalengo nao kwa baadaye.

Tunayasema hayo kutokana na kutambua kuwa soka kwa sasa ni biashara na ajira kubwa na kwa wachezaji hiyo ni sehemu ya maisha na ndiyo kila kitu kwao katika kuendesha maisha yao ya kila siku.

Lakini pia, matarajio yetu ni kuona usajili wa dirisha hili kanuni na sheria zikifuatwa hasa wachezaji kuepuka kujisajili mara mbili, lakini kwa klabu zikitanguliza mbele maslahi yao kwa kuwasikiliza maoni yao hususan wale wasiopata nafasi katika kikosi cha kwanza.

Habari Kubwa