Kongole Samia, tujengee mifumo na taasisi imara

29Jun 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kongole Samia, tujengee mifumo na taasisi imara

Rais Samia Suluhu Hassan, ametimiza siku 100 madarakani akiwa ni rais wa kwanza mwanamke Afrika Mashariki na Kati.

Ndani ya siku 100 ameonyesha uwezo mkubwa wa utendaji kazi katika kuleta umoja wa kitaifa kwa vitendo, ikiwamo kuweka wazi juu ya uwapo na utayari wa serikali kushughulikia ugonjwa wa corona, kwa kuunda kamati ya kitaalamu kuishauri serikali ambayo ilishatoa ushauri wake.

Pia, ameshalieleza taifa kuwa corona ipo na kila mmoja anapaswa kuchukua tahadhari kwa kuvaa barakoa, kuepuka misongamano, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka na kutumia vipangusa mikono.

Rais amekutana na makundi mbalimbali kama wazee, wanawake, vijana, Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wahariri wa Habari Tanzania na kote huko walitoka na kicheko kwa kuwa kero za msingi zimeshughulikiwa na zinaendelea kushughulikiwa.

Lakini amefanikiwa kuimarisha diplomasia ya nje ikiwamo kwenda kuhutubia Bunge la Kenya na kueleza umuhimu wa kuendelea kushirikiana na jinsi nchi hizo zinavyotegemeana katika mambo mengi, pia amehudhuria vikao vya kimtandao na moja kwa moja na wakuu wa taasisi za kimataifa, mabalozi na marais. Yote hiyo ni katika kuendelea kuonyesha nafasi ya Tanzania katika muktadha tofauti tofauti.

Eneo lingine ni usawa wa kijinsia, ambao aliahidi kuongeza idadi ya wanawake kwenye nafasi za maamuzi, na hilo limedhihirika kwenye uteuzi wa Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu Wakuu wa Wilaya, na hasa kuzingatia mambo ya msingi ya Muungano hasa kwa wizara ambazo zinahitaji uteuzi wa pande zote, na tunaamini idadi itazidi kuendelea kwa nafasi zilizosalia.

Eneo lingine ni la kodi, ambalo aliweka wazi kuwa hatakubali kodi ya dhuluma na baada ya muda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitangaza kufungua akaunti za wafanyabiashara zilizokuwa zimeshikiliwa.

La muhimu ni kwenye utawala wa sheria, ambao tumeona jitihada za kumaliza na kufutwa kesi ambazo zimekaa muda mrefu bila kukamilia, huku muhimili wa Mahakama unatenda kazi zake kwa ufanisi na sasa haki inatamalaki.

Mifano michache ni uamuzi wa Mahakama ya Rufani kuamuru serikali kurejesha fedha walizotozwa faini viongozi wa chama kimoja cha siasa, na jana kada wa chama hicho, aliachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya na kuachiwa kwa Mashekhe wa Uamsho 36.

Tunauthubutu wa kusema tunamshukuru Mungu kwa ajili yake na tunampa hongera kwa kuliongoza taifa kwa umahiri mkubwa, ambao umeleta tumaini na faraja baada ya msiba mzito wa Rais wa awamu ya tano, Hayati Dk. John Magufuli, kuondoa hofu ya kuongozwa na mwanamke na kuendelea kujenga ujasiri kuwa wanawake wanaweza, kubwa ni kuwaamini na kuwapa nafasi.

Pamoja na mafanikio hayo, sasa tunapenda kuona ikijengwa mifumo na taasisi imara, ili mazuri yanayoonekana na kufurahiwa na Watanzania yabaki kwenye mifumo hata akija kiongozi mwingine hawezi kubadili na nchi itakuwa na mwendelezo.

Nchi zilizoendelea zimewekeza kwenye taasisi na mifumo imara na siyo mtu imara, kiasi kwamba hata alivyoondoka kiongozi, hakuna kinachoharibika.

Pia, kilio cha Katiba Mpya kimekuwa cha muda mrefu na mwaka 2014 Bunge Maalum la Katiba ambalo Rais Samia alikuwa Makamu Mwenyekiti, lilikamilisha Katiba Pendekezwa, lakini wapinzani walisusia mchakato na kutoka nje ya Bunge na kutaka rasimu ya wananchi iheshimiwe.

Pamoja na mazuri mengi, ni muhimu kilio hiki kikategewa sikio kwa kuwa mchakato ulishaanza na ulitafuna mabilioni ya Watanzania, lakini Katiba iliyopo sasa ni ya miaka 44, kuna mambo yanahitaji marekebisho kwa kuzingatia mabadiliko mengi na ongezeko la watu.

Kongole rais na endelea kudumisha furaha ya Watanzania kwa kutatua kero za msingi, ili watu wafurahie na kujivunia kuzaliwa na kuishi nyumbani na moja kwa moja watakuwa wazalendo na kukipenda cha chao kwa kuwa wananufaika.

Habari Kubwa