Kongole Simba kwa hili la kituo cha afya

09Dec 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kongole Simba kwa hili la kituo cha afya

KLABU ya Simba imekamilisha awamu ya kwanza ya mradi wake wa ujenzi wa viwanja viwili vya mazoezi katika eneo la Bunju jijini Dar es Salaam na Jumamosi ilivikabidhi kwa mashabiki na wanachama wao.

Viwanja hivyo ambavyo ni cha nyasi bandia na asili, tayari vinaweza kuanza kutumika na klabu hiyo imeelezwa inaweza kuanza kuvitumia rasmi kuanzia leo.

Hakika hiyo ni hatua ya kupongezwa kwani ni miaka 83 sasa tangu klabu hiyo ilipoanzishwa mwaka 1936 na imekuwa ikifanya mazoezi katika viwanja vya kukodi, lakini sasa imetoka huko na inamulika mbele zaidi.

Kwa mujibu wa uongoziwa klabu hiyo, wamekuwa wakitumia kiasi cha Sh. 300,000 hadi 500,000/- kila siku kwa ajili ya kukodi tu viwanja vya kufanyia mazoezi.

Kwa mantiki hiyo, Simba ilikuwa ikitumia si chini ya Sh. milioni tisa kwa ajili ya kukodi tu viwanja vya kufanyia mazoezi ambazo wanakwenda kuzioko kufuatia kukamilisha viwanja vyake vya mazoezi Bunju.

Hata hivyo, mradi huo ambao umetekelezwa na Mwekezaji wao, Mohamed "Mo" Dewji kwa zaidi ya asilimia 90, lengo la kukabidhiwa kwa mashabiki na wanachama wa klabu hiyo ni ili sasa kuwataka kuunganisha nguvu kuweza kuchangia kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa matofali na mambo mengine.

Hivyo, ni wakati sasa kwa wanachama, mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kuunganisha nguvu ili kuweza kufikia malengo hayo na wote kuwa sehemu ya mafanikio ya klabu hiyo ambayo imeingia katika mfumo wa uendeshwaji wa hisa.

Mbali na hatua hiyo Simba iliyofikia, imeeleza mradi huo ni sehemu tu kati ya miradi mingine mikubwa wanayotarajia kuitekeleza katika eneo hilo la Bunju.

Mradi mwingine unaoelezwa kutarajiwa kufanywa katika eneo hilo ambalo tayari pia ujenzi wa vyumba vya kubadilishia kwa wachezaji umekamilika, ni hosteli ya kisasa kwa ajili ya timu ya wakubwa na ile ya vijana ambao utaanza mara moja huku Mo akiahidi kuchangia Sh. milioni 500 kati ya bilioni mbili zinazohitajika ili kuukamilisha.

Lakini kubwa kuliko yote ambalo limelifurahisha Nipashe ni mpango wa ujenzi wa kituo cha afya katika eneo hilo ulioelezwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa klabu hiyo, Asha Baraka wakati wa kutambulisha viwanja hivyo kwa wanachama na mashabiki juzi.

Kwa mujibu wa mjumbe huyo, klabu hiyo imeona kuna haja ya kujenga kituo cha afya katika eneo hilo, na si tu kwa ajili ya kuleta karibu huduma ya matibabu kwa wachezaji wao bali kurejesha huduma kwa jamii kwa kuwahudumia wakazi waliopo jirani na uwanja huo.

Haya ndiyo maendeleo Nipashe inayotamani kuona yakitokea katika soka letu, na tunaamini hatua hiyo itaigwa na klabu nyingine za Tanzania ambazo zinatamani kufikia mafanikio hayo.

Tunatumai kuona pia hilo likifanyika kwa Azam katika Uwanja wao wa Chamazi na klabu nyingine, lakini pia likiingizwa kwenye mipango ya Yanga ambayo imepewa eneo la kujenga uwanja Kigamboni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Lengo letu ni kuona Watanzania hawaishii tu kutumia fedha zao kwa ajili ya kulipa viingilio uwanjani, bali pia wakinufaika kwa kupata huduma za kijamii kama hiyo ya kusogezewa kituo cha afya karibu kutoka kwa klabu hizo.

Mwisho tunaiomba Simba na klabu nyingine nchini ziendelee kubuni miradi ambayo kwa namna moja ama nyingine itanufaisha na jamii inayoizunguka katika maeneo husika.

Habari Kubwa