Kuajiriwa walimu kunaleta tumaini

29Nov 2017
Mhariri
Nipashe
Kuajiriwa walimu kunaleta tumaini

Kauli ya serikali ya juzi kwamba inatarajia kuajiri walimu 13,700 wa shule za msingi na sekondari ndani ya mwezi ujao inatia matumaini kwa jamii katika kipindi ambacho Sera ya Elimu Bila Malipo inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Kauli ya serikali ya juzi kwamba inatarajia kuajiri walimu 13,700 wa shule za msingi na sekondari ndani ya mwezi ujao inatia matumaini kwa jamii katika kipindi ambacho Sera ya Elimu Bila Malipo inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Serikali ilisema mjini Dodoma kuwa itaajiri walimu hao, ili kuziba mapengo yaliyoachwa na watumishi walioondolewa kutokana na vyeti feki na msako wa watumishi hewa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya juzi, serikali itaajiri walimu 2,700 wa shule ya msingi na sekondari wakati wowote kuanzia siku hiyo.

Aidha, serikali ilisema kabla ya kufika mwisho wa mwaka huu, itakuwa imeajiri walimu wengine 11,000 ambapo katika idadi hiyo, 7,000 watakuwa wa shule za msingi na 4,000 kwa ajili ya shule za sekondari.

Kama ambavyo tumeshasema, Nipashe, ahadi hii ya serikali inatia matumaini kwa jamii katika kipindi ambacho Sera ya Elimu Bila Malipo inakabiliwa na changamoto mbalimbali. 

Lakini pia kutolewa kwa ajira ni habari njema miongoni mwa jamii baada ya kusikia taarifa za kusikitisha kwamba nchi ilikuwa na watumishi 19,000 waliokuwa ama na vyeti feki au hewa ambao uhakiki uliwabaini na kuwaondoa hatimaye.

Tuchukue nafasi hii, Nipashe, kuipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuwa na ujasiri na kumudu kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti feki katika utumishi wa umma.

Na tunaipongeza serikali pia, Nipashe, kwa kumudu kuanza kuajiri tena muda mfupi baada ya zoezi hilo kukamilika kama kunavyoelezwa na walimu watarajiwa karibu 14,000 hao.

Na kwa kuwa serikali imeahidi kukamilisha zoezi hilo katika kipindi cha siku 32 zijazo, pasingekuwa na habari njema ZAIDI za kufunga mwaka katika sekta ya elimu kuliko hizo. 

Pasingekuwa na habari njema zaidi za kufunga mwaka katika sekta ya elimu kuliko hizo, tunasema Nipashe, kwa sababu itakumbukwa Mei 13, mwaka huu, wakati akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka huu wa fedha, mjumbe wa kamati hiyo, Hussein Bashe, alibainisha changamoto kadhaa zinazoukabili utekelezaji wa Sera ya Elimu Bila Malipo, mojawapo ikiwa ni upungufu wa walimu.

Bashe ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), alisema kamati hiyo ilibaini Tanzania inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa walimu 182,899 wa shule za msingi na 69,794 wa shule za sekondari.

Kimsingi, kwa hesabu hizo za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii serikali bado ina safari ndefu ya kumaliza kabisa tatizo hilo.

Tunafahamu Nipashe, kuwa katika mwaka wa fedha na zaidi kidogo uliopita, serikali ilitoa jumla ya Sh. bilioni 37 kwa ajili kuimarisha shule 148 kwa kuzijengea mabweni ya wasichana na wavulana, kwa kuwa changamoto katika sekta ya elimu ni nyingi.

Lakini bado tuchukue fursa hii, Nipashe, kuishauri kutilia mkazo utoaji ajira zaidi za walimu kadri uwezo wa kiuchumi utakavyoruhusu ili matumaini haya yanayochomoza kisekta yawe na matokeo makubwa na kuondoa nakisi inayoonyeshwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Habari Kubwa