Kufutwa agizo la Mwakyembe kuwe somo kwa viongozi wote

19Mar 2017
Mhariri
Nipashe Jumapili
Kufutwa agizo la Mwakyembe kuwe somo kwa viongozi wote

RAIS John Magufuli alilazimika kuingilia kati na kufuta mara moja agizo la uzuiaji ufungishaji ndoa kwa watu wasio na vyeti vya kuzaliwa ifikapo Mei Mosi, 2017 lililokuwa limetolewa na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrisson Mwakyembe.

Rais alichukua hatua hiyo baada ya kuona kuwa agizo hilo halina tija kwa taifa, hasa kutokana na ukweli kwamba Watanzania wengi hawana vyeti vya kuzaliwa na hivyo amri hiyo ingewapa wakati mgumu.

Magufuli aliwataka Watanzania waendelee kuoana kwa namna waliyozoea na kwamba, agizo hilo halipo.

Awali, wakati akitangaza agizo hilo, Mwakyembe alidai kwamba Serikali imechukua hatua hiyo kwa nia ya kuhakikisha kwamba taifa linaondokana na sifa ya kuwa nchi mojawapo yenye watu wachache zaidi walio na vyeti vya kuzaliwa.

Kwa mujibu wa Mwakyembe, wananchi wa Tanzania Bara walio na vyeti vya kuzaliwa ni takribani asilimia 12 tu, hivyo ikizidiwa kwa mbali na visiwa vya Zanzibar ambavyo raia wake walio na vyeti hivyo ni asilimia 75.

Kwa sababu hiyo, Mwakyembe aliibuka na hoja kwamba, ni lazima sasa kupiga marufuku ufungishaji ndoa kwa watu wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa kwa sababu shughuli hiyo huambatana na matumizi makubwa ya fedha ilhali gharama ya cheti cha kuzaliwa ni Sh. 3,500 tu.

Kufuatia tangazo hilo, mijadala mingi iliibuka. Wengi walikuwa ni kama hawaamini kile alichokiagiza Mwakyembe.

Kwa ujumla, ilielezwa kwamba agizo hilo halitekelezeki kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo ukweli kwamba suala la ndoa haliana uhusiano wa moja kwa moja na vyeti vya kuzaliwa.

Pia tangazo hilo la Mwakyembe lilionekana kuwa halitekelezeki kwa sababu, kama alivyosema mwenyewe, ni Watanzania wachache tu wenye vyeti vya kuzaliwa na hivyo kuzuia ndoa kwao ni kwenda kinyume cha maslahi ya wengi.

Hakika, kama ilivyo kwa wengine, sisi pia tunaunga mkono uamuzi wa Rais Magufuli kufuta agizo la Mwakyembe. Ni uamuzi sahihi kwa sababu alichokiagiza waziri, hata kama ni kwa nia nzuri, lakini ni wazi kwamba hakina maslahi kwa taifa.

Ni agizo lisilotekelezeka pia kwa sababu suala la ndoa ni la watu binafsi, lenye kuhitaji maelewano tu baina ya wawili wapendao

Hata hivyo, Nipashe tunaona kuwa tukio hilo, la amri ya waziri kufutwa hata kabla ya kuanza kwa utekelezaji wake, linapaswa kuwa funzo kwa kila kiongozi.

Kwamba, waongeze umakini katika kujiridhisha na kila jambo kabla ya kulitangaza kwa umma. Kinyume chake, viongozi wa aina hiyo wataonekana kuwa ni ‘wakurupukaji’.

Na upo uwezekano pia wa kile wanachokiagiza kutenguliwa na mamlaka zao za uteuzi kama ilivyotokea kwa Mwakyembe

Mawaziri na viongozi wengine waepuke tabia iliyojitokeza kwa kasi hivi karibuni ya kutoa maagizo na amri zenye kuashiria kwamba wakati mwingine hukurupuka. Kwa mfano, yapo maeneo ambayo baadhi ya viongozi wa kisiasa wamedaiwa kutoa amri za kutaka kuwawajibisha watumishi wakiwamo wakurugenzi, ilhali ikifahamika wazi kwamba kisheria, viongozi hao hawana mamlaka hayo.

Ni kawaida pia hivi sasa kusikia kuwa katika baadhi ya maeneo, watu huzuiwa kutumia vyombo vya moto ifikapo saa 12:00 jioni, lengo likielezwa kwamba ni kuimarisha ulinzi na usalama.

Amri nyingi za aina hiyo huibua utata wa kisheria usiokuwa na sababu na pia kukiuka baadhi ya haki za msingi za binadamu.

Katika taifa letu ambalo huheshimu misingi ya utawala bora, mambo hayo hayapaswi kuachwa yaendelee kutokea kupitia ndimi za viongozi ‘wakurupukaji’ .

Kwa kutambua yote hayo, ndipo sisi tunaposisitiza kwamba tukio linalohusiana na amri ya Mwakyembe lisipite burebure tu. Bali, liwe somo pia kwa viongozi wengine.

Habari Kubwa