Kupatikana hati ardhi h’shauri habari njema

24Jun 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kupatikana hati ardhi h’shauri habari njema

JUZI Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, aliagiza kutolewa kwa hati miliki ya ardhi ndani ya wiki moja, baada ya mwananchi kukamilisha taratibu zote muhimu.

Waziri huyo alisema hati hizo zinapaswa kutolewa kwenye halmashauri ambazo wananchi wamelipia gharama za kupatiwa hati, ili kuondoa usumbufu na gharama kufuatilia hati kwenye ofisi za ardhi za mikoa.

Waziri Lukuvi aliongeza kuwa tangu kufunguliwa kwa ofisi mpya ya ardhi mkoa wa Tanga, hati zaidi ya 300 zimeandikwa na kusajiliwa kwenye mkoa na kusisitiza kuwa, uanzishwaji ofisi za ardhi kwenye mikoa siyo tu utaondoa usumbufu wa kufuatilia hati bali utapunguza pia migogoro ya ardhi.

Kabla ya mabadiliko, wananchi walitakiwa kufuatilia hati kwenye ofisi za kanda ambazo zipo mbali, jambo ambalo lilichelewesha upatikanaji wa nyaraka hiyo muhimu kwa umiliki wa ardhi.

Kutokana na hali hiyo idadi ya wananchi waliomudu gharama za kufuatilia hati ni chache, na wale zilizobakia walipata matatizo mbalimbali na kujicheleweshea maendeleo.

Urasimu katika sekta ya ardhi ulisababisha urasimishaji wa ardhi kuchelewa hadi pale serikali ilipoamua kurahisisha na sasa kumekuwa na hati za makazi zilizowezesha kuongeza thamani ya ardhi.

Sekta hiyo huko nyuma ilitawaliwa na rushwa kiasi cha mwenye nguvu ya fedha alifanya awezalo kupora haki ya maskini, huku kukiwa na ushiriki mkubwa wa watumishi wa idara hiyo, jambo ambalo liliwaweka wananchi katika maumivu na mahangaiko makubwa.

Waziri huyo ameeleza bayana kuwa utaratibu wa sasa hati za maeneo husika zinapokamilika halmashauri husika izifuate kwa Msajili wa Hati azifuate katika ofisi ya ardhi mkoa badala ya wananchi kuzifuata mkoani.

Tunapongeza hatua hii kwa kuwa sasa inakwenda kutoa ahueni kubwa kwa wananchi ambao licha ya kupitia misukosuko kwa ajili ya kupata hati miliki, lakini bado walilazimishwa kusafiri mbali na kutumia fedha kupata hati husika.

Pia, kupatikana kwa hati na leseni za makazi kumeongeza thamani ya ardhi na sasa mmiliki anaweza kupeleka hati yake kwenye taasisi ya fedha na kupata mkopo utakaomwezesha kuwekeza kwa ajili ya maendeleo ya sasa na yajayo.

Kipindi cha nyuma, wananchi wengi hususan maskini hawakukopesheka kwa kuwa hawakuwa na hati ya kuweka kama dhamana ili waaminiwe, lakini kwa sasa kupitia hati na leseni hizo wanakopesheka, na itapunguza au kumaliza migogoro ya ardhi.

Hii ni hatua kubwa na ambayo imeiwezesha serikali kupata mapato kutokana na makazi ambayo zamani haikukusanywa kwa kuwa maeneo husika yalikuwa hayajapimwa na kupewa hati au leseni.

Baada ya kauli ya Waziri, kinachotarajiwa ni utekelezaji kwa kuhakikisha mwananchi anapata hati kwenye halmashauri na kusiwe na ubabaishaji wowote au kujenga mazingira ya ugumu ili mwananchi atoe rushwa.

Kwa wakati huu, wananchi wanapaswa kuitumia vyema fursa hii kwa kuhakikisha kila mtu anafuatilia na kuchukua hati yake, hivyo kufikia malengo husika.

Tunaipongeza wizara, lakini ufuatiliaji ni muhimu sana kuhakikisha hati zinapatikana katika ngazi hiyo na kwa wakati mwafaka, kwa kuwa kuongea au kuagiza huwa ni jambo moja, lakini utekelezaji ni jambo jingine ambalo huhitaji msukumo mkubwa.

Lakini pia, taasisi za fedha zinapaswa kupokea hati hizo na kujiridhisha nazo kisha kutoa huduma ya mikopo kwa mujibu wa taratibu zao, hivyo kuwawezesha kusonga mbele kimaisha kwa kuwa watawekeza kibiashara, makazi na mengineyo.

Kutokana na hatua hii, sasa tunaweza kusema kuwa serikali inaonyesha kwa vitendo ahadi zake za kuwajali wanyonge kwa kuhakikisha wanapata huduma muhimu, ambazo humo nyuma ilikuwa ndoto kuzipata, hususan hati ardhi

Habari Kubwa