Kushuka bei ya mafuta kulete nafuu

06Jan 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kushuka bei ya mafuta kulete nafuu

JANA Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ilitangaza bei mpya za petroli, ambayo imeshuka kati ya Sh. 4 hadi 35 na dizeli Sh. 43 hadi 67 kwa Bandari ya Dar es Salaam.

Bei hizo zinashuka kutoka Sh. 2,510 kwa lita moja ya petroli ambayo sasa itauzwa Sh. 2,501, huku bei ya dizeli kupungua kutoka Sh. 2,325 hadi 2,234.

Kwa Bandari ya Tanga bei ya petroli itashuka kutoka Sh. 2,521 hadi 2,525, huku Bandari ya Mtwara kutoka 2,569 hadi 2,534.

Kwa upande wa bei ya dizeli kwa Tanga itapungua kutoka Sh. 2,413 hadi 2,369, Bandari ya Mtwara ikiwa ni kutoka Sh. 2,423 hadi 2,425 huku bei ya mafuta ya taa ikipanda kwa Sh. 99.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Godfrey Chibulunje, alisema bei za mafuta zingepungua zaidi iwapo thamani ya Dola za Marekani isingeongezeka dhidi ya Shilingi ya Tanzania.

Kwa sasa Dola ya Marekani inanunuliwa kwa Sh. 2,314.23 ikiwa ni ongezeko la asilimia moja kutoka Sh. 2,300.88, huku tozo za taasisi za serikali zilizopunguzwa Oktoba mwaka jana zilisaidia kupunguza bei ya mafuta kwa kati ya Sh. 23 na 31 kwa lita kutegemeana na aina ya mafuta.

Kushuka kwa bei hizi ni habari njema kwa Watanzania kwa kuwa mafuta yalisababisha mfumuko wa bei kwenye bidhaa nyingi kiasi cha wengi kushindwa kumudu.

Kwa sasa bei za vyakula na bidhaa nyingine zimepanda na zilikuwa zinaendelea kupanda na sababu kubwa inayotajwa ni kupanda kwa bei ya mafuta, sasa imeshuka tunatarajia kuona mabadiliko kwenye bei hizo.

Kwenye ujenzi kinachoelezwa kupanda kila siku ni chuma kiasi cha nondo ya milimita 12 iliyokuwa inauzwa Sh. 19,000 mwaka jana, sasa inauzwa Sh. 27,000 ikiwa ni ongezeko la Sh. 7,000 kwa moja, haya ni maumivu makubwa kwa wanaojenga sasa.

Mafuta ya kupikia ya alizeti lita tano yamefika Sh. 36,000 huku lita moja ikiuzwa Sh. 9,000, hali hii sio nzuri kwa sababu hata bidhaa za sokoni kama maharagwe, mahindi, mchele, unga na vinginevyo muhimu kwa maisha ya kila siku vimeongezeka bei na wote sababu kubwa ni kupanda kwa gharama za usafiri kutoka shambani hadi sokoni.

Bei zinapopanda anayeumia ni mwananchi wa kawaida kabisa ambaye atajikuta anatumia fedha nyingi huku hali yake ikiendelea kuwa duni, atashindwa kutimiza mahitaji ya msingi kwa kuwa kipato kinakuwa kile kile licha ya ongezeko la gharama.

Lakini ni muhimu mamlaka za serikali kufuatilia bei za bidhaa mbalimbali hasa za vyakula na ujenzi ambazo kila uchao zinazidi kupaa na wanaoumia ni wengi kwa kuwa ni lazima watu wale.

Tunaamini kushuka kwa bei za mafuta kutaonyesha ahueni kwa wananchi na lazima kuwe na ufuatiliaji wa karibu kwa kuwa wengi wanalangua bidhaa ili kujipatia faida, lakini wanaoumia ni wananchi, kwamba kuanzia wasafirishaji washushe gharama za usafiri ili wauzaji wa bidhaa wafanye hivyo.

Ufuatiliaji wa karibu utasaidia kuwatambua walanguzi ili kuchukua hatua madhubuti mapema, kwa kuwa lengo ni kumwezesha mwananchi wa kawaida kumudu maisha yake huku akiendelea kulipa kodi.

Tayari wananchi wamebanwa kwenye tozo mbalimbali kwenye kulipia umeme, miamala ya simu, anaponunua mafuta ya petroli na dizeli, pia kwenye bidhaa kuna kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), zote hizi ni mzigo kwa mwananchi hivyo ni lazima tuone ahueni kwake ili gharama za maisha zishuke.

Habari Kubwa