Kutumia majanga kujinufaisha sawa na kufurahia vifo

19Mar 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kutumia majanga kujinufaisha sawa na kufurahia vifo

WAKATI huu ambao dunia unakabiliwa na tishio kubwa la ugonjwa wa corona, kuna Watanzania kadhaa ambao wanafurahia, na kukitumia tishio hilo kuwa fursa kwao.

Watu hawa ambao ni wafanyabiashara, badala ya kutoa mchango wao na kushirikiana na Watanzania wenzao kuhakikisha kuwa tishio hilo halisababishi maafa nchini, wao wanapandisha bei ya vifaa ambavyo vinatumika kujikinga na maambukizi mara dufu.

Walianza kupandisha bei baada ya vifaa hivyo kama maji tiba (sanitizer) na ‘mask’ mara dufu baada ya kusikia wananchi wakihamasishwa na kuhimizwa kuvitumia kwa lengo la kukabiliana na kusambaa kwa ugonjwa huo ambao unasababishwa na virusi.

Kitendo hicho kimewaathiri watu wengi kutokana na kushindwa kumudu, huku wakiiomba serikali kuchukua hatua za haraka dhidi ya ulanguzi unaofanywa na wauzaji wa vifaa hivyo.

Katika maduka kadhaa ambayo yalitembelewa na waandishi wetu jijini Dar es Salaam kwa mfano wilayani Ubungo, maski moja ilikuwa ikiuzwa kwa gharama ya Sh. 5,000 kutoka Sh. 500, huku maji-tiba (sanitizer) yakiwa yameadimika madukani.

Mmoja wa watoa huduma kwenye duka la dawa eneo la Kimara Baruti, alisema maski hizo zimeadimika dukani kwa sababu wafanyabiashara kutoka China hawajaleta nchini.

Alisema gharama imepanda sana kwa kuwa kabla hazijaadimika, walikuwa wanauza moja kwa Sh. 500, lakini sasa wanauziwa boksi zima kwa Sh. 80,000 badala ya Sh. 5,000 , huku ndani na ndani zinawekwa 50.

Katika duka lingine kwenye eneo hilo, mfanyabiashara wa duka la dawa alisema wananunua maski kutoka kwa watu binafsi ambao wanawauzia kuanzia Sh. 60,000 hadi Sh 100,000 kwa boksi moja.

Kuhusu maji-tiba alisema bidhaa hiyo imeadimika madukani kote, hivyo gharama zake nazo zitakuwa zimeongezeka kwa wauzaji ambao watakuwa nazo.

Alisema awali walikuwa wanauza maji-tiba yenye ujazo wa milimita 25 kwa 250, lakini kwa sasa yanauzwa kwa Sh 5,000.

Sisi Nipashe tunalaani vitendo hivi vya kihuni vya kupandisha bei vinavyofanywa na baadhi ya wauzaji wa vifaa hivyo, kwa kuwa ni kutothamini utu na thamani ya binadamu badala yake kujali fedha na maslahi binafsi.

Tunachokiona ni kuwa watu hao wanatumia majanga kama fursa ya kujinufaisha, huku wakifurahia kuona binadamu wenzao wakipoteza maisha ili waendelee kuuza vifaa hivyo kwa bei ya juu kutokana na kuongezeka mahitaji.

Kimsingi, misingi ya soko huria hairuhusu soko kuingiliwa, ikiwamo serikali kuweka bei elekezi za bidhaa na huduma kwa lengo la kuliacha lijiendeshe lenyewe.

Hata hivyo, katika mazingira yetu, baadhi ya wafanyabiashara wanakiuka misingi hiyo kwa kupandisha bei ovyo badala ya kuacha mahitaji (demand) kutegemeana na usambazaji (supply).

Kutokana na hali hiyo, tunaona kwamba ipo haja kwa sasa kwa serikali kuingilia kati kwa muda ili kuweka mambo sawa.

Ndio maana tunaunga mkono hatua ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ya kuwataka wafamasia wote nchini kuchangamkia fursa ya kutengeneza vifaa vya kujikinga kama maji-tiba na maski za kuziba pua na mdomo ili kuvisambaza maeneo yote nchini.

Habari Kubwa