Kuwadhibiti wapigadebe wa mabasi mikoani jambo jema

28Jun 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kuwadhibiti wapigadebe wa mabasi mikoani jambo jema

MAENEO mengi ya stendi za mabasi yaendayo mikoani na maeneo mengine yamekuwa yakisababisha usumbufu mkubwa kwa abiria.

Usumbufu huo umekuwa ukisababishwa na mawakala wa kampuni za mabasi na watu wengine ambao wanakaa vijiweni kufanya kazi ya upigadebe kwa ajili ya kujipatia kipato.

Mawakala na wapigadebe wamekuwa wakibughudhi abiria na watu wengine ambao ni wapita njia kwa njia mbalimbali zikiwamo kuwapigia kelele za kuwaita, kuwafuata nyuma, kuwapokea mizigo kwa nguvu ili kuipeleka katika ofisi za kampuni za mabasi husika na mambo mengine ambayo ni usumbufu na kero.

Kibaya zaidi ni kuwa kuna watu wanaojifanya mawakala wa kampuni hizo wanaosimama mitaani wakiwa na vitabu vya tiketi za mabasi, hivyo kuna baadhi ya abiria wanapewa risiti feki na matokeo yake kuwatapeli fedha zao.

Kuna matukio kadhaa ambapo baadhi ya abiria wanakatiwa tiketi zikionyesha namba za viti, lakini baadaye abiria hao hujikuta wakikosa viti kutokana na basi kujaa licha ya kuwa wanakuwa wameshalipia.

Stendi ya Ubungo jijini Dar es Salaam kwa mfano, imekuwa ni kero kwa abiria na wapita njia kutokana na vitendo vya bugudha kutika kwa mawakala na wapigadebe hao. Hali hiyo pia ni sugu katika stendi ya mabasi ya Nyegezi jijini Mwanza.

Kipindi cha mwisho Desemba hadi Januari hali huwa mbaya zaidi kutokana na vyombo vya usafiri hususan mabasi kutokidhi mahitaji.

Mazingira hayo yasiyo rafiki ya utoaji wa huduma za usafiri yamekuwa yakitishia usalama wa wasafiri na mali zao, na ndiyo maana yamekuwa yakilalamikiwa.

Pamoja na kuputa muda mrefu bila hatua kuchukuliwa na mamlaka husika, lakini hatimaye zimesikika taarifa zinazotia moyo; kwamba hatua zimeanza kuchukuliwa kudhibiti hali hiyo.

Serikali ilitangaza jana kuwa imeandaa mfumo rasmi wa kielektroniki katika ukataji tiketi za abiria wa mabasi yanayofanya safari zake mikoani utakaowaondoa rasmi wapigadebe na mawakala wa mabasi nchini.

Aidha, mfumo huo utaanza kutumika kwa majaribio katika njia itakayoainishwa na unataanza kutumika nchi nzima Septemba mwaka huu na baadaye kwenye mabasi ya mjini (daladala).

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Kamwelwe alisema katika kuzishughulikia changamoto zilizopo katika sekta ya usafiri wa mabasi nchini, serikali kupitia Taasisi ya Udhibiti wa Usafiri Nchikavu (LATRA) na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Takwimu (NIDC) wameandaa mfumo huo ili kuzipatia majibu.

Alisema mfumo huo umetengenezwa ili kuboresha utoaji wa huduma za usafiri kwa abiria na kuwaondolea kero ya ulanguzi wa nauli ambao unafanyika katika mazingira ambayo siyo rasmi kutokana na kukosekana kwa taarifa sahihi.

Alisema changamoto hizo huwaathiri watumiaji wa huduma hasa katika kipindi chenye mahitaji makubwa ya usafiri ambapo fedha nyingi za abiria huchukuliwa na mawakala au wapigadebe nje ya nauli halisi inayotakiwa.

Pia, alisema kwa kuzingatia mahitaji ya wadau mbalimbali, mfumo huo itakuwa na taarifa zote muhimu zinazoweza kutumiwa na taasisi mbalimbali kama vile Latra, Polisi, Mamlaka ya Mapato (TRA), Uhamiaji, vyuo vya elimu ya juu na watafiti.

Tunaipongeza serikali kwa kuona changamoto hiyo na kuja na suluhisho, hivyo ni matumaini yetu kuwa wananchi sasa watapata huduma bora za usafiri bila usumbufu.

Tunatarajia mfumo huo utaandakiwa vizuri bila kusababisha usumbufu na mkanganyiko kwa wasafiri.

Habari Kubwa