Kuzingatia mwongozo mpya corona muhimu

27Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kuzingatia mwongozo mpya corona muhimu

SERIKALI imekuja na mwongozo mpya wa kupambana na virusi vya corona, huku ikipiga marufuku mikusanyiko mikubwa ya kijamii, zikiwamo sherehe, shughuli za kisiasa na kidini isiyo ya lazima.

Katika taarifa yake kwa umma, Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana na afya za Watanzania, Prof. Abel Makubi, alisema, marufuku hiyo inakuwapo hadi ugonjwa huo utakapodhibitiwa na taarifa kutolewa rasmi.

Serikali inasema inachukua hatua hiyo, kutokana na mwenendo wa ugonjwa huo nchini, na kwamba kamati ya wataalamu imeainisha maeneo mahususi yanayohitajika kutiliwa mkazo kupitia afua za kupunguza msongamano katika jamii, ili kukata mnyororo wa maambukizi katika ngazi ya kaya na jamii.

Kwa mujibu wa Prof. Makubi, mwongozo huo utawawezesha wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii na kubadili tabia zao huku wakizingatia mbinu za kujikinga na corona, kwa kupata elimu ya kutosha na kujiwekea utaratibu wa kudhibiti ugonjwa kutokusambaa kwenye jamii.

Mwongozo huo unalenga maeneo yenye mikusanyiko ya watu, hasa ya huduma za kijamii, kibiashara, kiuchumi, kiofisi, ambayo ni mojawapo ya vyanzo vya kusambaa kwa maambukizi katika jamii.

Kwingine ni katika vituo vya mabasi, ambapo mwongozo unaelekeza uongozi wa vituo hivyo, kusimamia uwapo wa vifaa vya kunawia maji tiririka na kuhakikisha abiria wote wananawa mikono.

Wamiliki wa vyombo vya usafiri nao wanatakiwa kuweka vitakasa mikono katika vyombo hivyo na kusimamia uvaaji barakoa, huku wale wanaohitaji kufanyika shughuli za mikusanyiko wakitakiwa kuomba vibali maalum.

Sisi tunaunga mkono juhudi hizo za serikali, na tunaushauri umma wa Watanzania kuuzingatia, kwani uzoefu unaonyesha kuwa tangu kutangazwa kwa wimbi la tatu la corona, baadhi ya watu hawajachukua tahadhari zozote.

Kuanzia katika vyombo vya usafiri na hasa daladala, abiria wanajazana kupita kiasi, hawavai barakoa, kwenye vituo hakuna maji wala vitakasa mikono, na hata baadhi ya kumbi za starehe hali ni ile ile.

Tunadhani hali hiyo ya baadhi ya watu kutokuwa makini na ugonjwa huo, aidha inatokana na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu madhara ya corona, au wanafanya makusudi.

Lakini pamoja na yote hayo, njia ambayo tunaamini inaweza kusaidia, ni kuendelea kutolewa kwa elimu ili jamii ibadilike, kwani kumekuwapo na elimu nyingi ambazo hutolewa mitaani na watu wasio wataalamu wa afya.

Kwa hali kama hiyo, wakati mwongozo ukiwapo, tunadhani ni wakati mwafaka wa kutolewa kwa elimu hiyo kwa wingi, ili kuwabadilisha Watanzania ambao bado hawaamini kuwapo kwa ugonjwa huo nchini ili wachukue tahadhari.

Lakini tungeshauri kuongezwa kwa magari ya abiria hasa maeneo ya mijini kama Dar es Salaam ambako abiria wamekuwa wakijazana katika daladala kupita kiasi kutokana na uhaba wa usafiri.

Kutokana na mwongozo kuelekeza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha mabasi ya usafiri wa umma yanapakia abiria kulingana na idadi ya viti pasipo kusimama, tunashauri kuongezwa kwa mabasi ya abiria.

Habari Kubwa