Kwa hili la upotoshaji katika vitabu serikali usilifumbie macho

14May 2017
Mhariri
Nipashe Jumapili
Kwa hili la upotoshaji katika vitabu serikali usilifumbie macho

WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na mafunzo ya Ufundi, imewasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka ujao wa fedha na kama ilivyo ada, wabunge wamechangia ili kuhakikisha sekta ya elimu kwa ujumla inaboreshwa.

Miongoni mwa mambo yaliyochangiwa katika mjadala wa wizara hiyo ni kuibuka kwa vitabu vyenye makosa ya kimaudhui ambazo vimeshasambazwa na kuanza kutumika katika shule mbalimbali.

Kutokana na kuwapo kwa dosari hiyo, wabunge wametaka serikali kusimamia suala hilo kwa kuwa linaweza kuwa chanzo cha upotoshaji wa masuala nyeti yanayohusu taifa na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Kwa mujibu wa wabunge hao, makosa hayo kwenye vitabu yamesababisha ubora na viwango vya vitabu hivyo kuwa duni na hata kuweka mazingira ya elimu inayotolewa kuwa katika hali ya shaka.

Kwa mantiki hiyo, wabunge wametaka serikali kuhakiki wataalamu walioko katika Taasisi ya elimu Tanzania ambayo ndiyo inatoa ithibati ya vitabu vinavyotumika katika ngazi mbalimbali za elimu.

Wakichangia bajeti hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2017/18, walisema vitabu
vinavyotengenezwa vipo chini ya kiwango na vimekuwa vinamakosa hali inayosababisha elimu inayotolewa kuwa duni.

Baada ya Mbunge wa Songwe, Philipo Mulugo (CCM) kuibua suala hilo, James Mbatia (Vunjo- NCCR Mageuzi), ameitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya watu ambao wanataka kuangusha elimu nchini, kwa kuwa bila kuwa na vitabu bora ni vigumu kufikia malengo ya yaliyowekwa katika maendeleo ya elimu.

Mbatia hakuishia hapo tu kwani alisema kuendelea kujitokeza kwa kasoro hizo alizoziita za makusudi katika elimu, kunatokana na serikali kutochukua hatua dhidi ya maazimio mbalimbali yakiwamo ya Bunge. Alitoa mfano wa suala la matatizo ya elimu aliloliibua mwaka 2013 lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika.

Jambo hili la matatizo ya elimu linapaswa kuchukuliwa kwa umakini mkubwa kwani linaweza kusababisha matatizo makubwa kwa kizazi cha Tanzania miaka mingi ijayo. Makosa hayo, ambayo yana upotoshaji wa hali ya juu, kama baadhi yalivyoainishwa na wabunge, ni hatari kwa maendeleo ya nchi.

Ieleweke kwamba watunzi wa vitabu wanapowapotosha watoto, ni dhahiri kwamba vinaupotosha ulimwengu mzima. Mfano wa upotoshaji huo ni baadhi ya maandiko yaliyodai kuwa Mlima Kilimanjaro uko Kenya.

Kwa mfano huu pekee, ni jambo la kujiuliza ni mamilioni mangapi ya watu duniani yamedanganywa na kuaminishwa kuwa Kilimanjaro iko Kenya?

Kama wahenga wasemavyo ni heri kuzuia kuliko kutibu, sasa ni wakati mwafaka kwa serikali kupitia taasisi zilizopewa mamlaka ya kuratibu mitaala la elimu na maandishi kudhibiti ubora wa vitabu ili kuepusha upotoshaji unaoweza kujitokeza ndani ya jamii.

Kwa changamoto zilizoainishwa na wabunge wetu, ni imani kwamba serikali itachukua hatua za kupiga marufuku vitabu hivyo vinavyopotosha ambavyo vimesambazwa na kuanza kutumika katika ngazi mbalimbali za elimu.

Sambamba na hilo, jamii ina imani kuwa watu waliodiriki kupotosha umma kupitia maandiko hayo watachukuliwa hatua zinazostahili.