Kwa mtindo huu, hatuwezi kufika mbali


05Sep 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kwa mtindo huu, hatuwezi kufika mbali


MARA kwa mara Shirikisho la Soka Tanzania - TFF limekuwa likilalamikiwa na wadau mbalimbali wa soka kutokana na linavyotekeleza majukumu yake.


Imekuwa ni jambo la kawaida kwa mamlaka hiyo ya kuratibu na kusimamia mchezo wa soka kufanya mambo yanayohitaji utaalamu bila kuzingatia mahitaji husika.
Juzi shirikisho hilo lilifanya jambo lingine la ajabu baada ya kumteua Sebastian Nkoma kuwa Kocha Mkuu wa timu ya soka Taifa ya Wanawake wa Tanzania Kilimanjaro Queens.


Sambamba na uamuzi huo, pia waliteuliwa wachezaji wa kuunda kikosi hicho kwa ajili ya kushiriki michuano ya Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati yatakayoanza Septemba 11, nchini Uganda.

Kinachoshangaza ni kwamba, timu imeteuliwa kwenda mashindano ya kimataifa wakati Ligi ya Soka ya Wanawake bado hata haijaanza.

Tunajiuliza, hii TFF yenye wataalamu wa ufundi wanawezaje kuamua kuipeleka timu kwenye mashindano kwa kuokoteza wachezaji.
Nipashe, tunaamini timu bora ya taifa huundwa kutoka kwenye ligi bora na siyo kwa mtindo wa kuokoteza wachezaji.
Je, uteuzi wa wachezaji hao ulizingatia ubora upi kama hata ligi ambayo ndiyo kitovu cha uteuzi bado haijaanza.

Kocha huyo amewaona wapi wachezaji hao waliowachagua na kuwaaminisha Watanzania kuwa ndiyo bora kuliko wengine wakati hakuna mashindano yoyote yaliyowashindanisha?

Iko hivi, hata kwenye timu za taifa za soka la wanaume, makocha kuchagua wachezaji kutokana na kuwaona kwenye klabu zao zikicheza.

Wale walioonekana kufanya vizuri ndiyo wanaounda kikosi cha timu ya taifa.

Lakini hali ni tofauti kwa Kilimanjaro Queens yetu inayokwenda kwenye mashindano yenye taswira ya kimataifa kwa wachezaji wa kuokoteza.

TFF isijione kama ina dhamana yenye sura binafsi katika uteuzi wa timu za taifa, kwa sababu timu haziendi kwenye mashindano ya kimataifa kwa mwamvuli wa TFF, bali nchi.


Mafanikio ya soka siyo jambo la mara moja. Kwamba, kwa sababu tu tumepewa mwaliko basi tunakwenda kwenye mashindano bila maandalizi.
Aibu yoyote inayopata timu ya taifa kwenye mashindano, siyo mzigo wa TFF bali taifa.


Sasa leo hii timu yetu ikifanya vibaya kwenye mashindano na kuitia aibu nchi, TFF watatueleza nini?
Je,watakuwa tayari kusema kwamba timu haikuwa na maandalizi? Je, kama haikuwa na maandalizi kulikuwa na sababu gani ya kwenda kushiriki?

Suala la kuanza kwa Ligi ya Soka wanawake limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu, lakini utekelezaji wake umeonekana kuwa hafifu.

Suala la kuanzishwa kwa ligi ya wanawake lilikuwapo muda mrefu na kama utekelezaji wake ungefanyika mapema, bila shaka leo hii tungepeleka timu yenye wachezaji walioiva kwa mashindano.
Lakini kwa sababu TFF imemezwa na utamaduni wa kufanya mambo katika mtindo 'bora liende', haitashanga kuona vijana wetu,dada zetu, mabinti zetu wakirudi na aibu tutakayoshindwa kuificha.

Habari Kubwa