Kwa nini madarasa yakoseshe watoto kidato cha kwanza?

18Dec 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kwa nini madarasa yakoseshe watoto kidato cha kwanza?

TAARIFA kuwa wanafunzi 74,166, sawa na asilimia 8.9 ya waliofaulu mtihani wa taifa wa darasa la VII mwaka huu, hawajapangiwa shule katika awamu ya kwanza kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwakani kutokana na uhaba wa madarasa, ni za kusikitisha.

Ni masikitiko, lakini ndio ukweli, kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Selemani Jafo, alipotoa taarifa hiyo jana jijini Dodoma na kufafanua kuwa kati yao, wavulana ni 34,861 na wasichana ni 39,305.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya na wa mikoa kuhakikisha wanasimamia kwa karibu ujenzi wa vyumba vya madarasa ili ukamilike kabla ya Februari 28, mwakani.

Jafo alisema mahitaji ya vyumba vya madarasa ni 1,480 ambavyo vinatakiwa ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi hao waliokosa nafasi katika awamu ya kwanza.

Jafo alisema amefanya ziara katika maeneo mbalimbali na kukuta ujenzi unaendelea kwa kasi na sehemu nyingi walichelewa kutokana na kipindi ambacho saruji iliadimika, lakini baada ya serikali kuingilia kati, kwa sasa saruji ipo na ifikapo Februari 28 mwakani, wanafunzi wote watajiunga na masomo yao ya kidato cha kwanza.

Kwamba wanafunzi waliokosa nafasi awamu ya kwanza watapangiwa shule katika awamu ya pili kadri mikoa na halmashauri zitakavyoendelea kukamilisha ujenzi vyumba vya madarasa na madawati.

Licha ya hatua alizozitangaza Waziri Jafo, kwa upande wetu tunaona kuwa suala la wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha tano kuchelewa kujiunga na shule wanazopangiwa kutokana na ukosefu wa vyumba vya madarasa na madawati limekuwa likijirudia kila mwaka.

Hali hiyo inaweza kutafsiriwa kuwa inatokana na kutokuwapo kwa maandalizi ya mapema ya kuwapo kwa miundombinu hiyo wakati kila mwaka idadi ya wanafunzi wa kujiunga na vidato hivyo inakuwa inajulikana mapema.

Suala zina la waliofaulu kukosa madarasa au madawati, hivyo kuchelewa kupangiwa nafasi awamu ya pili lina athari kadhaa kwao na kwa Taifa.

Mosi, wanaweza kujikuta wanakosa kujiamini katika masomo kutokana na kupelekwa haraka ili kuwafikia walioanza kusoma awamu ya kwanza.

Pili, ujenzi wa miundombimu hususan madarasa unapofanyika kwa mtindo wa zimamoto (haraka bila maandalizi ya kutosha) unaweza kutofikia viwango kutokana na kulipua, hivyo baada ya muda mfupi kukuta majengo hayo yanakosa uimara.

Wanafunzi 74,166 waliokosa nafasi awamu ya kwanza kutokana na uhaba wa madarasa ni wengi sana, hivyo tunaishauri serikali kuandaa mkakati maalum ambao utakuwa endelevu katika kulitafutia tatizo hili ufumbuzi.

Kwa mtazamo wetu, serikali hainabudi kuangalia uwezekano wa kuwashirikisha wadau katika kuchangia kwa njia mbalimbali, zikiwamo harambee kwa ajili ya ujenzi wa vyimba vya madarasa.

Tunasema hivyo tukiwa na uhakika kwamba wadau wengi wataguswa kusaidia kwa kuwa suala la elimu ya watoto linamgusa kila mmoja. Hii inathibitishwa na jinsi wadau walivyojitoa kuchangia madawati baada ya serikali kuanzisha na kuratibu mchakato huo.

Vilevile, tunawashauri Waziri Jafo na mwenzake wa Elimu. Prof. Joyce Ndalichako, kuketi pamoja na wataalamu wa kuona ni namna gani ya kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo hili ili lisiathiri maendeleo ya taaluma ya watoto wetu katika elimu ya sekondari.

Kwa kuwa serikali imedharimia kwa dhati kutoa elimu bure ya msingi hadi kidato cha nne, tunaamini kuwa ukosefu wa madarasa hautakwamisha tena watoto kuingia kidato cha kwanza kwa wakati mwafaka.

Habari Kubwa