Kwanini shule zisianzishe miradi ya kujitegemea?

27Jan 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kwanini shule zisianzishe miradi ya kujitegemea?

WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Tandale Magharibi jijini Dar es Salaam, wameripotiwa na Nipashe kuwa wamekwama kutumia vyoo vipya kutokana na ukosefu wa maji.

Hawawezi kutumia vyoo hivyo vya kusukumwa kwa maji kwa vile yako ndani ya kisima na ili kuyapata ni lazima kutumia pampu za umeme kuyasukuma yaingie kwenye mapipa.

Hali hiyo inasababisha wakose vyote maji na vyoo vya kisasa. Kwa sasa shule ina malimbikizo ya deni la umeme la Sh.  milioni 3.6 wanalodaiwa na Tanesco.

 

Kukosekana umeme kunawafanya wanafunzi zaidi ya 1,195, kutumia vyoo vya zamani ambavyo si rafiki tena ni salama.

Wanafunzi hao licha ya kupokea fedha za ruzuku zinazotolewa kila mwezi na serikali, shule yao haiwezi kulipa deni hilo wala kugharamia umeme kwa kuwa ruzuku hiyo haina bajeti ya kulipia nishati.

Suala la shule kushindwa kulipia gharama za umeme huenda haliko Tandale pekee  ni jambo linalowezekana kusumbua shule nyingine nyingi za umma za msingi na sekondari.

Kama tatizo ni kukosa fedha za kulipia nishati hiyo, huu ndiyo wakati wa serikali kuziruhusu shule hizo kuanzisha miradi itakayoziwezesha kujitegemea na kugharamia mahitaji kama  umeme.

Ni suala linaloweza kupata ufumbuzi iwapo shule zitaruhusiwa kutumia ardhi yake kuweka vitega uchumi kama kuanzisha maduka ya shule ya kuuza daftari, kalamu, vitabu na mahitaji yote ya wanafunzi ili fedha inayopatikana itumiwe kulipia gharama zisizolipwa na ruzuku ya elimu.

Ni wakati pia wa kuangalia namna ya  kujenga migahawa itakayokodishwa kwa mama na babalishe ambao wataandaa vyakula, vitafunwa na vinywaji na kuwauzia wanafunzi na katika fedha wanazopata pia walipe kodi kiadogo kuongeza pato la shule. 

Katika ardhi za shule, serikali iruhusu kuwe na miradi kama mashine za kurudufu (fotokopi), kuchapa,  ziwe na miradi ya kupiga wanafunzi picha za vitambulisho, ziwe na miradi ya kuuza karatasi  kwa ajili ya majalada ya madaftari na hata kuwa na mashine na gundi za kuunganisha vitabu vilivyochakaa au kuchanika.

Aidha, ni wakati wa kufikiria uwezekano wa maduka ya shule yanayoshona na kuuza sare za wanafunzi kuanzia mavazi ya shule kama sketi na shati au suruali au kaptula, nguo za  michezo, soksi, viatu, masweta na mabegi.

Mahitaji kama haya yakinunuliwa kwenye maduka ya shule au kukiwa na mafundi wa shule wanaoshona nguo hizo shule inaweza kujiongezea kipato na kuwa na fedha za kugharamia umeme na mahitaji mengine.

  Shule nyingine zinaweza kuwa na miradi kama mashine za kusaga na kukoboa nafaka. Hasa zile zilizoko vijijini. Fedha zinazokusanywa ziiingie kwenye mifuko ya shule kusaidia kuongea mapato.

Ni wakati wa kujiongeza ili kuondokana na changamoto kama hiyo ya Shule ya Msingi Tandale Magharibi ambayo imeshindwa kutumia vyoo kisa ina deni la Tanesco.

Iwapo wanafunzi wananunua huduma na bidhaa mbalimbali kutoka kwenye maduka yaliyoko mitaani inakuwaje washindwe kuyapata mahitaji hayo ndani ya shule zao?

Ni wakati wa kujiongeza na kutafuta mbinu za ujasiriamali wa kuendesha shule ili kuwaondolea adha wanafunzi ambao wanastahili pia kuwa na maji safi na salama ya kunywa lakini pia kuwa na vyoo safi vinavyotumia maji ya kuwasaidia kunawa na kuepukana na magonjwa.

NI vyema serikali ikaangalia upya mbinu za kuziwezesha shule kujitegemea kama ambavyo  ilikuwa ikifanyika miaka ya zamani wakati wa enzi za mafunzo ya miradi ya kujitegemea.

 

Habari Kubwa