La biashara ya watoto lifuatiliwe kwa karibu

09Sep 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
La biashara ya watoto lifuatiliwe kwa karibu

JUZI Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, lilieleza kuwakamata watu wawili kwa tuhuma za kuwatorosha watoto 11 wenye umri wa miaka 10 na 14, kwenye maeneo mbalimbali na kuwasafirisha kwenda kuwauza kwa wafugaji ili wakatumikie kuchunga mifuko.

Watuhumiwa hao walikamatwa Septemba 5, mwaka huu na kubainika kuwa baadhi ya watoto walitoroshwa kutoka kwa wazazi wao na wengine wale wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Alisema watuhumiwa hao walikuwa wanauza watoto hao kwa wafugaji walioko wilayani Mbarali kwa gharama kati ya Sh. 25,000 hadi 30,000, na kwamba kabla ya kuwauza waliwatumikisha kwenye shughuli za uzalishaji wakati wakiendelea kutafuta wateja wa kuwauzia.

Aidha, baadhi ya watoto walisema walichukuliwa kwa kushawishiwa na wengine walichukuliwa kwa nguvu na kusafirishwa kwa kutumia pikipiki kwenda maeneo, ambayo watuhumiwa walikuwa wanawahifadhi.

Hili ni tukio moja kati ya mengi ambayo hujitokeza kwa watoto kupotea na kwenda kutumikishwa kwenye maeneo mbalimbali, ikiwamo shughuli za nyumbani, kutumikishwa kingono ambazo ni kinyume cha sheria ya mtoto.

Tukio hili linatoa picha halisi ya uwajibikaji wa wazazi katika kulinda na kutunza watoto wao kwa kuhakikisha wapata mahitaji ya msingi, ikiwamo elimu na siyo kutumikishwa kwenye migodi, nyumbani, sehemu za starehe na kwingine ambako hawastahili kuwapo.

Unapotazama luninga ya ITV kila siku jioni utaona idadi ya wazazi ndugu na jamaa wanaotangaza kupotelewa kwa watu mbalimbali, hasa watoto ambao wengine huwapata, lakini wengine hawaonekani kabisa.

Tukio hili na mengine yanakumbusha wajibu wa wazazi kutunza watoto wao kufuatilia kwa karibu mienendo yao, ikiwamo maendeleo ya kitaaluma kama wanafika shuleni au la.

Kuna tatizo kubwa la baadhi ya wazazi kuzaa watoto na kukwepa jukumu la malezi kwa wengi kujilea wenyewe au kukosa msingi wa malezi kiasi kwamba ni rahisi kuchukuliwa na yeyote kama ilivyotokea wa watoto 11 walioibiwa na kwenda kuuzwa.

Kwa sasa matukio ya utapeli na kuiba watoto yanaongezeka kwa kuwa wanaofanya hivyo wanatengeneza mazingira ya kujipatia fedha huku watoto wakiumia kisaikolojia na kiafya.

Hii ni biashara haramu ya kusafirisha binadamu ambayo kimsingi hairuhusiwi kwa mujibu wa sheria za nchi, lakini inatuma salamu kuwa kuna tatizo kubwa hasa malezi na hali ngumu ya uchumi kwa baadhi ya wananchi.

Kwa mtazamo wetu ni muhimu kila mmoja akatimiza wajibu wake kwa ambaye ni mzazi au mlezi kumleta mwanaye ipasavyo, ikiwamo kufuatilia kwa karibu maisha yake kuliko kuacha kujilea, ili kuwa na vijana sahihi kwa taifa la kesho.

Watoto hao walitakiwa kuwa shuleni na siyo kwenda kutumikishwa, lakini ni muhimu vyombo vya dola vikafanya uchunguzi wa kina kwenye maeneo mengine kama ya mgodi ambalo kuna watoto wengi wanatumikishwa kwa ujira mdogo badala ya kwenda shuleni.

Kwa mjini ikiwamo Dar es Salaam watoto wanatumika kuongoza ombaomba au kutumwa na wazazi wao kuomba au wanaosha vioo vya magari katika maeneo ya Makutano ya barabara za Mwenge na Salenda, na mbaya zaidi wengine ni watoto chini ya miaka nane.

Kwa mtazamo wetu ni muhimu sana jamii pia ikashiriki malezi ya watoto hao kwa kuwa wapo ambao wako kwenye mazingira magumu siyo kwa kupenda bali ni kwa sababu wazazi wamewatelekeza au wamefariki na kukosa mtu wa kuwatimizia mahitaji ya msingi kama ada na chakula.

Habari Kubwa