La Magomeni Kota liwe mwendelezo wananchi kufikiwa

03Sep 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
La Magomeni Kota liwe mwendelezo wananchi kufikiwa

MASUALA muhimu na kugusa jamii moja kwa moja ikiwamo makazi, afya, ardhi, elimu hayaepukiki kwa mtu wa kipato chochote.

Kutokana na hilo, serikali huzingatia kero kadhaa na kuzitafutia ufumbuzi ambao huibuka kwenye maeneo hayo, ili jamii husika kuishi salama na kwa utulivu.

Makazi ya wakazi takribani 644 wa zilizokuwa  Kota za Magomeni, ambazo zilibomolewa miaka kadhaa kupisha ujenzi wa makazi bora, wamepata matumaini mapya, baada ya kuahidiwa kuhamia kwenye makazi mapya, Oktoba mwaka huu.

Kikao cha hivi karibuni kati ya viongozi wa wakazi hao pamoja na wa serikali, kilitokana na mkutano wa wakazi hao kukutana Jumapili wiki iliyopita kujadili hatima yao, huku wakimwomba Rais Samia Suluhu Hassan kutoa neno kuwahusu wao.

Walimwomba rais atoe neno kutokana na kuwapo taaarifa mbalimbali ambazo ziliripotiwa awali kwamba wakazi watakaohamia makazi mapya ni 300 pekee na sio 644.

Kwenye mkutano wakazi hao walidai kwamba licha ya ujenzi wa majengo kuushuhudia kukamilika siku ya wao kuhamia zilizidi kusogezwa mbele kila uchao, na kwamba baadhi yao wanaishi kwa ndugu, jamaa na wengine wakipanga.

Jambo la kufurahisha ni kuona serikali inakuwa sikivu kwa kuchukua hatua haraka za kufuatilia na kuamua wakazi hao wahamie kwenye makazi hayo mwezi ujao.

Uongozi wa wakazi hao juzi ulisema kuwa mkutano wa Jumatatu kati yao na viongozi wa serikali ulikuwa wa manufaa, kutokana na ulileta matokeo chanya na serikali kusikia kilio chao.

Ni mkutano uliokuwa na manufaa kwa kuwa umewarejeshea faraja wakazi hao, ambao walikaa muda mrefu bila kilio chao kupatiwa ufumbuzi. Tunaamini kwamba ahadi hiyo itatekelezwa, hivyo kukidhi matarajio yao ya kuhamia kwenye makazi mapya mwezi ujao, huku ujenzi ukiendelea kukamilishwa kwenye maeneo madogo hususan kukamilisha ufungaji wa transifoma na mita za Luku kwenye kila ‘appartment’.

Nipashe tunaipongeza serikali kwa kusikia kilio cha wakazi 644, kwa kuzingatia kwamba kwa vyovyote vile nyuma yao wapo wanaowategemea kwenye familia zao ambazo huishi nao kwenye makazi.

Ikumbukwe kwamba kabla ya suala hili kupatiwa ufumbuzi, wakazi hao walipata wakati mgumu, baada ya kutokea utata wa idadi ya wakazi waliokuwa na haki ya kupata makazi hao.

Wakazi hao walilalamikia taarifa walizokuwa wakipewa na baadhi ya mamlaka kwamba waliokuwa na haki ya kupata nyumba hizo ni 300 badala ya 644 kama walivyoahidiwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Hayati Dk. John Magufuli.

Hili ni moja kati ya changamoto ambazo wananchi hukumbwa nazo kwenye maeneo tofauti nchini, zinazosubiri hatua kama hii, ambayo serikali imechukua kuokoa wakazi hawa.

Nipashe, inaunga mkono katika hatua ambazo serikali huchukulia mara moja ili kuwaondolea kero wananchi na migogoro ambayo pengine ingeepukika awali, iwapo utatuzi ukiwa wa mapema.

Yapo mengi katika sekta tofauti ikiwamo, ardhi huduma za upatikanaji umeme, maji, elimu bora ambayo yanasubiriwa kutatuliwa na kuwapa ahueni wananchi.

 
 

Habari Kubwa